Tabasamu larejea kwa Mwalimu Lyuvale, aliyepata ajali akienda benki

Mufindi. Tabasamu limerejea machoni mwa Mwalimu Silvester Lyuvale (52) wa Shule ya Msingi Kinyanambo, Halmashauri ya Mji Mafinga, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa.

Furaha hiyo imekuja baada ya wadau mbalimbali kuguswa na hali yake na kumchangia kiti cha kutumia umeme na miguu bandia, hatua zitakazomwezesha kutembea tena na kutekeleza majukumu yake kama mwalimu.

Mwalimu huyo anasema Aprili 21, 2019, inabaki kwenye kumbukumbu kwa sababu ndiyo siku aliyopata ajali iliyosababisha akatwe miguu yote miwili na kumuachia ulemavu wa kudumu.

Kabla ya kupata ajali hiyo, Lyuvale alikuwa Ofisa Elimu wa Kata ya Wambi, lakini ajali hiyo ilibadili kabisa mwenendo wa maisha yake.

Hata hivyo, simulizi yake iliyoandikwa na kuchapishwa na Mwananchi Digital na Gazeti la Mwananchi, Machi 12 na 13, 2025, yenye kichwa cha habari “Safari ya benki ilivyomuacha na ulemavu wa kudumu mwalimu”, imesaidia kurudisha matumaini kwa mwalimu huyo.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Awali, mwalimu huyo alisimulia namna alivyoipata ajali hiyo kwa kugongwa na gari. Alisema siku hiyo alitoka nyumbani kwake kwenda benki kuchukua fedha za malipo ya wafanyakazi wa shambani kwake.

Alisema kabla ya kutoka nyumbani, alikokuwa akinywa juisi ya embe iliyoandaliwa na mkewe, hakuimaliza, akaamua kuifunika akiamini muda si mrefu angerudi na kuja kuinywa.

Hata hivyo, alisema juisi ile ilibaki kwenye glasi kama ilivyo, naye akaishia kupata ajali baada ya pikipiki aliyokuwa akiendesha kugongwa na gari.

Alisema baada ya ajali alihisi maumivu makali, lakini hakutambua kuwa atapoteza miguu yote miwili.

“Baada ya ajali nilipoteza fahamu. Wasamaria wema walinipeleka Hospitali ya Mji Mafinga, siku hiyo hiyo nikahamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Iringa. Ilikuwa kati ya saa tatu na saa nne asubuhi,” alisema.

Alisema alipatiwa matibabu kwa mwezi mmoja, akakatwa mguu mmoja, na hali bado haikuwa nzuri.

“Nilitakiwa kuhamishiwa hospitali nyingine. Nikapelekwa Hospitali ya Ikonda, wilayani Makete, mkoani Njombe. Nilitibiwa, nikaambiwa natakiwa kukatwa mguu mwingine, na ule uliokatwa katika Hospitali ya Rufaa Iringa nao unatakiwa kurudiwa kukatwa,” alisema.

Baada ya kukatwa miguu yote miwili, alisema alipata nafuu, akarudi nyumbani.

Alisema alipokatwa mguu wa kwanza hakuwa akijitambua, lakini wa pili madaktari walimwambia ataweza kutembea kwa kutumia miguu ya bandia.

“Nilipokea hali hii kwa sababu tangu niliposema huu mguu wa pili pengine unaweza kunisaidia, walisema nao umeharibika. Mfupa ulikuwa na ukungu mweusi ndani.

“Kwa mapenzi nikasema, ‘Mungu, kwa sababu umeniokoa siku ile, basi naomba hata huu ukatwe tu, ilimradi niweze kuendelea vizuri.’ Nashukuru hadi sasa naendelea vizuri; sijapata shida yoyote tangu nilipokatwa, miaka sita sasa imepita,” alisema mwalimu huyo alipozungumza na Mwananchi awali.

Simulizi hiyo iliyodokezwa hapo juu ilisomwa na kuwagusa Watanzania wengi, ambao jana walijitokeza kumsaidia.

Akizungumza na Mwananchi jana, Jumamosi Mei 17, 2025, nyumbani kwake, Mwalimu Lyuvale amesema shukrani zake za dhati ziende kwa Gazeti la Mwananchi na mitandao yake ya kijamii kwa kuchapisha habari yake.

“Nashukuru sana. Matunda yake yameonekana baada ya kufika na kuandika habari yangu. Watanzania walisoma, wameguswa na mimi kwa namna ya kipekee. Wamejitokeza kunisaidia kiti mwendo cha kutumia umeme pamoja na miguu ya bandia,” amesema Lyuvale.

Amesema walimu wenzake na wakuu wa shule za sekondari ambao alifanya nao kazi walikuwa na taarifa za ajali yake, lakini hawakufahamu alipo au changamoto alizokuwa akipitia, ikiwamo matumizi ya kiti cha kawaida. Habari hiyo ilipoonekana ndipo walifahamu yuko wapi na anafundisha shule gani pale Mafinga.

Miongoni mwa watu walioguswa na habari ile na ikamsukuma atoe msaada ni Mhandisi Agustino Masoi, ambaye ameiambia Mwananchi kuwa baada ya kupata taarifa zake, aliamua kumnunulia Lyuvale kiti mwendo kinachotumia umeme.

Huku akikionyesha kiti hicho kwa tabasamu, Lyuvale amesema: “Mnakiona hapa. Kwa sasa naenda shuleni mwenyewe, nafundisha, nakurudi. Siiti tena bajaji kwa ajili ya kunirudisha nyumbani kwangu.”

Amesema Mhandisi Masoi pia alimpatia fedha taslimu Sh10 milioni kwa ajili ya matibabu na kuchongewa miguu saidizi wakati akipata huduma katika Hospitali ya KCMC, mkoani Kilimanjaro.

Mbali na Masoi, Mwalimu Lyuvale ametoa shukrani pia kwa Chama cha Kulinda na Kutetea Haki za Walimu (Chakuhawata) Mafinga, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Mufindi, maofisa elimu kata nchini, Mbunge wa Mafinga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi, pamoja na Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Dorothy Kobero, kwa msaada wao.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Afurahia kurejea kufundisha

Lyuvale amesema kazi ya ualimu aliipenda tangu akiwa shule, hivyo ajali aliyoipata ilimuumiza mara mbili.

Amesema aliumia kwa maumivu ya majeraha, lakini pia aliumia sana kila alipofikiria kwamba ajali imekatisha ndoto ya kazi aliyoipenda tangu akiwa kijana mdogo.

“Furaha yangu imepitiliza hadi nashindwa cha kusema… Nilikuwa nashindwa hata kuinua miguu yangu, lakini hata wewe umeona nasimama na kutembea. Sina cha kusema bali Mungu awabariki,” amesema Mwalimu Lyuvale.

Amesema jambo la msingi kwake kwa sasa ni kufanya kazi kwa juhudi na bidii na kuendelea kuwaombea waliofanikisha kurejesha tabasamu lake.

Amesema baada ya msaada huo, sasa anarejea tena kazini akiwa na nguvu na ari kubwa ya kufanya kazi.

Hata hivyo, ameomba wadau wasimchoke ili afanye kazi yake ya kufundisha vizuri zaidi. Ameomba kusaidiwa meza ya kutembea au kiti cha kutembea ili anapofundisha awe amesimama kwa muda mrefu.

Kuhusu kazi yake ya awali ya kugonga kokoto kujikimu, amesema kwa sasa hataifanya tena, bali ataajiri vijana.

Mke asimulia

Christina Nyakunga, mke wa Mwalimu Lyuvale ambaye wana watoto watano, ameelezea furaha yake baada ya kuona mumewe akitembea tena.

Amesema anashindwa cha kusema kutokana na furaha kubwa na amewashukuru wote waliochangia kumwezesha mumewe kutembea tena.

Akizungumza kwa niaba ya maofisa elimu kata nchini, Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Elimu Kata Tanzania (Umekta), Mkoa wa Iringa, Laurent Mwilafi amesema baada ya kupata taarifa za Lyuvale, maofisa elimu kata nchini walikubaliana kuweka utaratibu wa kumchangia ili apate chombo cha usafiri.

Kati ya halmashauri 184 nchini, 177 zilichangia, sambamba na wadau wengine wakiwamo mlezi wa Maofisa Elimu Kata Taifa, Suzan Nusu. Kutokana na michango hiyo, Umekta ilifanikiwa kununua pikipiki ya magurudumu matatu (Guta) yenye thamani ya Sh7.2 milioni.

Amesema pia chama kimemchangia Sh10 milioni.

“Tumefanikiwa leo (jana) kumkabidhi Mwalimu Lyuvale pikipiki ya magurudumu matatu (Guta), pamoja na stakabadhi ya benki ambayo tumemuwekea Sh10 milioni kwenye akaunti yake.”

Amelishukuru pia Gazeti la Mwananchi kwa kuguswa na kuamua kuchapisha habari ya mwalimu huyo, ambayo imezaa matunda ya kupatiwa msaada wa hali na mali.

Maofisa elimu wajitokeza kutoa msaada

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Elimu Kata ya Mwandiga kutoka Mkoa wa Kigoma, Khadija Takota amesema lengo la kufika Mafinga ni kuungana na maofisa elimu wengine waliofika kumsaidia mwenzao.

Amesema habari ya Lyuvale iliwashtua, hasa baada ya kuona akigonga kokoto kutokana na ulemavu alioupata.

“Jambo hili linasikitisha. Kama kiongozi na mwananchi, kiukweli niliumia sana baada ya kuona taarifa hiyo. Sisi kama maofisa elimu Mkoa wa Kigoma tuliungana na maofisa elimu wa kata nchi nzima kuhakikisha tunamchangia mwalimu huyu kwa hali na mali,” amesema Khadija.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa walemavu wa CWT Wilaya ya Mufindi, Chrisantus Bakana amesema CWT awali ilimnunulia Lyuvale kiti cha kawaida miaka sita iliyopita, ambacho alikitumia hadi mwaka huu alipoleta ombi la kiti kingine baada ya cha zamani kuchoka.

Amesema CWT ilitenga bajeti ya Sh300,000 kwa ajili ya kununua kiti kipya. Bakana amesisitiza nguvu ya kalamu, huku akisema habari iliyochapishwa na Mwananchi ilisomwa nchi nzima na kusaidia walimu kutoka mikoa mbalimbali kumpigia simu na kuulizia namna ya kumchangia mwalimu huyo.

“Leo ninayo furaha kuona ndugu yetu ana furaha, kwa sababu mara ya kwanza nilivyokuja na kumkuta anagonga kokoto, alionekana si mwalimu tena… alikuwa akionekana ni mwalimu aliyekata tamaa,” amesema Bakana, huku akisisitiza kuwa waandishi wa habari ni watu muhimu katika jamii yoyote ile.

Awali, Katibu wa Chakuhawata wilayani Mafinga, Fabian Sanga alisema walikuwa wanafahamu changamoto aliyokuwa akipitia Lyuvale, hali iliyowasukuma kumchangia Sh500,000.

“Habari hii inaonyesha nguvu ya vyombo vya habari katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii. Tabasamu la Mwalimu Lyuvale ni ushuhuda wa mshikamano huu,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *