Simba kuisubiri CAF hatima ya uwanja wa fainali

Dar es Salaam. Baada ya mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kuchezwa kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane ambapo imetoka kushuhudiwa wenyeji RS Berkane wakiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba, kumekuwa na sintofahamu juu ya uwanja utakaotumika katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Tanzania.

Awali Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilionyesha kuwa mchezo wa pili wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika utachezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ambao ulitumika katika mchezo wa nusu fainali uliozikutanisha Simba na Stellenbosch ya Afrika Kusini baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kuwa katika marekebisho.

Taarifa hiyo ya CAF kuishauri Simba kucheza mechi hiyo ya mkondo wa pili dhidi ya RS Berkane visiwani Zanzibar ilileta sura tofauti kwa viongozi pamoja na mashabiki wa timu hiyo kwani mipango yao ilikuwa ni kucheza kwenye Uwanja wa Mkapa unaochukuwa mashabiki 60,000 tofauti na ule wa New Amaan Complex unaobeba mashabiki 15000 pekee.

Hata hivyo, Simba ilikuwa imeshaanza kuuza tiketi za mchezo huo ambao waliamini utafanyika kwenye Uwanja wa Mkapa, Da r es Salaam ambapo mpaka sasa jumla ya tiketi 20000 zimenunuliwa kwa ajili ya mtanange huo wa fainali.

Baada ya mchezo wa jana kumalizika nchini Morocco, Naibu Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ameeleza kuwa suala la Uwanja wa Benjamin Mkapa tayari wamelifanyia kazi ili kuhakikisha mechi inachezwa kwenye Uwanja huo.

“Tunawasubiri CAF watuambie kwa sababu wao wanaamini uwanja ni mzuri kuchezeka isipokuwa kama kutakuwa na mvua kubwa, kwa hiyo sisi tumewapa ushahidi ikiwamo ripoti ya idara ya hali ya hewa kuonyesha tarehe 24, 25 na 26 hakuna mvua isipokuwa tarehe 26 asubuhi ndo mvua nyepesi nyepesi itanyesha.

“Kwa hiyo naamini watakapotoa maamuzi wataturuhusu kutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Kimsingi kama Simba Uwanja wao wa nyumbani ni Benjamin Mkapa kama hauruhusiwi ilibidi waulizwe Simba wanataka kucheza wapi ndio maana CAF hawakuandika kwamba mchezo uende Zanzibar kwenye Uwanja wa Amaan, wameandika wanashauri mchezo uende Zanzibar.

“Kwa hiyo tunaamini watakuja kufanya ukaguzi wa mwisho waturuhusu tutumie dimba lile na ikishindikana watawapa Simba nafasi ya kuamua mchezo uende wapi na Simba wataona ni wapi wataupeleka mchezo huo,” amesema Hamis Mwinjuma, Naibu Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mchezo wa fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika umepangwa kufanyika Mei 25 mwaka huu ambapo Wekundu wa Msimbazi watakuwa nyumbani kuikabili RS Berkane ambayo inaongoza kwa mabao 2-0.

Katika mchezo wa marudiano Simba itahitaji kulazimika kupata ushindi wa mabao 3-0 ili kubeba ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwakwe wakati RS Berkane wakihitaji sare ya aina yoyote ili kubeba taji hilo kwa mara ya tatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *