Dar es Salaam. Biashara ya majeneza inazidi kushika kasi nchini, huku ikiibua sintofahamu na hofu kwa wananchi, namna inavyouzwa karibu na zilipo hospitali, hali inayoondoa matumaini kwa wagonjwa.
Majeneza, licha ya kuwa na faida kwa jamii katika kumsitiri marehemu, lakini hali ya kuwekwa karibu na zilipo hospitali imekuwa ikivuta hisia za wengi, huku baadhi wakiihusisha na biashara ya watumishi wa hospitali.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini pia uwepo wa biashara hiyo katika mikoa tofauti ikiwamo Jiji la Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha, Dodoma na Morogoro, ambapo majeneza huuzwa jirani na hospitali.
Hata hivyo, wapo baadhi ya viongozi wa Serikali ambao walishaingilia kati, ambapo Novemba 2024, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, alipiga marufuku biashara hiyo kwenye maeneo ya hospitali.
Chacha alisema si jambo sahihi majeneza kuuzwa hadharani na kutaka yatengwe maeneo maalumu kwa ajili ya biashara hiyo, ikiwa ni kuondoa hofu kwa wagonjwa na wafanyabiashara hao.
Nchini Kenya, Gavana wa Trans Nzoia, Patrick Khaemba, aliwahi kubainisha namna ambavyo biashara za huduma za mazishi zinatakiwa kuwekwa umbali wa kilomita mbili kutoka hospitali.
Alielezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa maduka yanayouza majeneza na vifaa vingine vya mazishi karibu na hospitali.
“Biashara ya huduma za mazishi karibu au ndani ya hospitali huathiri kupona kwa wagonjwa,” alisema.
Huko Zambia, biashara ya kuuza majeneza karibu na hospitali ilitakiwa kuondoshwa maeneo hayo, wakishauri biashara hiyo kuhamishiwa karibu na maeneo ya makaburi.

Meya wa mji wa Lusaka, Miles Sampa, alisema wauza majeneza watahamishwa maeneo ya makaburini iwapo hawataondoka wenyewe kwa hiari katika maeneo ya jirani na hospitali.
Hali ilivyo nchini
Katika hospitali nyingi ikiwamo Muhimbili, biashara ya majeneza inafanyika mita chache kutoka geti kuu la kuingia hospitali.
Mbali na Muhimbili, uchunguzi wa Mwananchi umebaini pia biashara hiyo inafanyika jirani na Hospitali ya Amana ya Dar es Salaam, Tumbi ya Kibaha mkoani Pwani na kwenye hospitali nyingine nyingi katika mikoa tofauti nchini.
Baadhi ya wananchi wanaamini biashara ya majeneza jirani na hospitali inachangia kuwapa msongo wa mawazo wagonjwa wengi.
Wanasema hali hiyo inawasababishia wakati mgumu pia, wengi wao hushindwa kupata nafuu pale wanapokuwa wanaendelea kupatiwa matibabu, huku wakichungulia majeneza.
Wanashauri biashara ya majeneza iwe na maeneo maalumu na isiwe jirani ya hospitali, ambako huko wagonjwa wanaamini wanakwenda kupona na si kukutana na mazingira yanayoashiria kifo.
“Mgonjwa anapokuja hospitali, anachokitarajia ni kupata ahueni ya maradhi yanayomsumbua. Inapotokea akakutana na majeneza, wapo ambao akilini mwao wanaanza kufikiria kifo,” anasema Mathayo Magoti.
Neema Msuya anasema, pamoja na kwamba kifo ni kitu ambacho hakiepukiki kwa binadamu, lakini kuna mazingira ambayo hakutakiwi kumjenga mtu picha ya kuogofya kuhusu jambo hilo.
Alphonce Karama anasema zipo hospitali, biashara hiyo imekuwa ikifanyika jirani na wadi za wagonjwa, hali ambayo inatia hofu kwa mgonjwa.
“Iliwahi kunitokea nimelazwa, kwenye mita kadhaa kutoka wadi niliyopo biashara ya majeneza inafanyika. Nilikosa amani, ilikuwa nikifumba macho nahisi na mimi nipo kwenye jeneza.
“Nilikosa imani ya kupona, siku waombolezaji walipokuja kununua jeneza, tena la mgonjwa ambaye tulikuwa wadi moja, nilifikiria zaidi kuhusu kifo badala ya uponaji siku hiyo,” anasema.
Familia ya Raphael John yenyewe inaeleza namna baba yao alivyogoma kutibiwa na kutaka arudishwe nyumbani baada ya kupata hofu alipoona biashara ya majeneza ikiendelea mita 200 kutoka hospitalini.
Marietha Msilanga anasema aliona majeneza yakiuzwa jirani na hospitali, hali ile ilimpa woga na kuhisi mwisho wake umefika.
“Nilipata ajali, nikiwa kwenye maumivu makali napelekwa hospitali (alilitaja), niliona nje kidogo ya fensi ya hospitali kuna majeneza yanauzwa. Hali ile iliniogofya na kuhisi nipo ndani ya jeneza.
“Hali hiyo ilinitesa kwa muda, kwani kuna nyakati nilijikuta nipiga kelele peke yangu kutokana na kile nilichokiona,” anasema shuhuda huyo.
Naye Yusuph Mchonga, mkazi wa Igunga Tabora, anasema biashara ya jeneza karibu na hospitali inaweza kutengeneza mazingira ya watoa huduma kutenda visivyo ili wafanyabiashara hao wapate pesa.
“Siwezi kusema ipo, lakini kwa mazingira hayo mfanyabiashara anaweza kufanya ukaribu na daktari kwamba ‘biashara ngumu, fanya unavyoweza ili tupate riziki’. Nashauri watafutiwe sehemu yao,” anasema Mchonga.
Kwa nini biashara hiyo hospitali?
Baadhi ya wauza majeneza waliozungumza na Mwananchi wanasema biashara ya majeneza ni kama biashara nyingine, inaweza kufanyika katika eneo lolote rafiki.
Wanasema kuna mazingira yanawalazimisha wengine kuifanya hospitali kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa muktadha wa eneo rafiki zaidi kwa biashara.
“Kama ambavyo mtu anaweka biashara fulani sehemu fulani akiamini ndipo inauzika, lakini uharaka wa kupata huduma hiyo na hii ndivyo inavyokuwa kwetu,” anasema Lyimo Lyimo.
Anasema unapokuwa na biashara hiyo jirani na hospitali, kupata wateja wengi pia ni rahisi tofauti na ukiweka pembezoni, ambavyo inaweza kufanya gharama kuwa kubwa za kupata jeneza.
Matiko Masegenya anasema biashara hiyo kama nyingine imekuwa ni mkombozi na moja ya njia kuu ya wao kuingiza kipato kama zilivyo biashara nyingine.
“Miaka ya nyuma ilikuwa ngumu kidogo kuzoeleka, ukionekana unauza majeneza hata watu wanakuogopa. Hivi sasa imezoeleka na ni kitu cha kawaida,” anasema Masegenya.
Masengenya aliyedumu kwenye biashara hiyo kwa zaidi ya miaka 20 sasa, anasema biashara hiyo jirani na hospitali ni rahisi kupata wateja na kwamba wengine hawaishii kununua jeneza tu, bali kutaka huduma nyingine kwa marehemu.
“Hiyo ndiyo advantage (faida) ya kupata eneo la biashara hii jirani na hospitali. Tunafuata wateja walipo, lakini inawaondolea gharama za ziada kutafuta huduma kutoka hospitali,” anasema.
Wagonjwa huathirika kisaikolojia
Mwanasaikolojia, Charles Kalungu, anasema kitaalamu kuna kitu kinaitwa phobophobia, ambayo hali hiyo inakwenda kusababisha kitu kinaitwa taphophobia.
“Taphophobia ndiyo inasababisha hofu ya mtu kuhisi kama anazikwa akiwa hai. Hii huwatokea baadhi ya watu pale anapoona jeneza ilhali ni mgonjwa,” anasema.
Anasema mtu huyo huingiwa na wasiwasi unaosababisha atengeneze hisia zisizo na uhalisia na kupata hali ya kukosa utulivu.
“Hizi taphophobia kila mtu huwa nazo, japo inategemea na aina ya wasiwasi. Hata hivyo, kinachopelekea hiyo hali ni taarifa alizonazo kuhusu tukio la kifo.
“Huwezi kuogopa bila kuwa na taarifa za hicho kitu unachokiogopa. Mfano mtu akiingia mochwari, akajua ni chumba cha kuhifadhia maiti, ile hali ya wasiwasi itampata.
“Akitazama mazingira ya hicho chumba na kuwa na hofu huenda zamu yake imekaribia. Hivyo ndivyo inavyokuwa hata kwa mgonjwa kutazama jeneza akiendelea na matibabu,” anasema.
Anasema kumbukumbu za mtu huyo humfanya moja kwa moja kujifunza kuogopa kwa kushuhudia vitu ambavyo taarifa zake anazisikia.
“Pia kuna kitu kinaitwa taphophobia. Hii inafanana na fobia inaitwa claustrophobia, husababisha mtu kuogopa akipita eneo la vichochoro, anaogopa kufunga mlango akiwa chumbani au kuogopa kupanda lifti na kuwa na wasiwasi,” anasema.
Nini wafanye?
Kalungu anasema, kwa mtu ambaye ana kihoro cha kifo, anapaswa kusaidiwa kufanya mazoezi ya kupumua ambayo yatamsaidia kupunguza kupaniki.
“Ikiwezekana azoee kwenda kwenye hayo maeneo, maana wapo wengine hata hawezi kuhudhuria mazishi.

“Vilevile kuna programu maalumu ya ku-modify mawazo ya mtu ili kumwezesha kutafsiri tafsiri mpya ya vitu,” amesema.