Waziri Mkuu wa Tripoli atoa wito kwa makundi yenye silaha kuungana na serikali

Waziri Mkuu wa Libya anayeungwa mkono na Umoja wa Mataifa siku ya Jumamosi ametoa wito kwa makundi yenye silaha kujihusisha na “taasisi za serikali” baada ya siku kadhaa za mapigano makali mjini Tripoli na maandamano ya kumtaka ajiuzulu.

Imechapishwa:

Dakika 3 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

“Tutawakaribisha wale wote ambao watachagua kusimama na serikali,” Waziri Mkuu Abdulhamid Dbeibah amesema katika hotuba ya televisheni.

“Tutawaweka kando wale wanaotumia ubadhirifu na ufisadi. Lengo letu ni Libya isiyo na wanamgambo na ufisadi.”

Siku kadhaa za mapigano katika mji mkuu huo zimehusisha kundi lenye silaha lenye mafungamano na serikali yenye makao yake makuu mjini Tripoli dhidi ya makundi ambayo kundi hilo limekuwa kikitaka kusambaratisha.

Libya imegawanyika kati ya serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli, inayoongozwa na Dbeibah, na utawala hasimu wa mashariki unaodhibitiwa na familia ya mbabe wa kivita Khalifa Haftar.

Nchi hiyo ya Afrika Kaskazini imesalia na mgawanyiko mkubwa tangu uasi wa waka 2011 ulioungwa mkono na NATO ambao ulimwondoa na kumuua kiongozi wa muda mrefu Moamar Kadhafi.

Mapigano ya hivi majuzi yamesababisha vifo vya takriban watu wanane, umesema Umoja wa Mataifa, wakati mamlaka bado haijatoa hesabu rasmi.

Mapigano hayo yalichochewa na mauaji ya Abdelghani al-Kikli, mkuu wa kitengo cha Msaada na Utulivu (SSA), aliyeuawa na Brigedi ya 444 inayoungwa mkono na Dbeibah.

Wimbi la pili la mapigano lilihusiha Brigedi ya 444 dhidi ya kundi jingine, kikosi cha Radaa, ambacho kinadhibiti maeneo ya mashariki mwa Tripoli na taasisi kadhaa muhimu za serikali.

Na msururu wa maagizo ya viongozi yalikuwa yakitaka kusambaratishwa kwa Radaa na kufuta makundi mengine yenye silaha yenye makao yake makuu mjini Tripoli, ukiondoa Brigedi ya 444.

Hotuba ya hivi punde zaidi ya Dbeibah ilihusu hasa Radaa, kundi linalodhibiti sehemu za mashariki mwa Tripoli.

“Jaribio la kuzusha mfarakano kati yetu na Souq al-Joumaa (ngome ya Radaa) litashindwa,” Dbeibah amesema, akikiri “kosa la pamoja” alipozungumzia “mapigano katikati ya Tripoli katika vitongoji vilivyojaa raia”.

Alisema kuwa mshirika wa SSA “amechukua udhibiti wa benki sita, na wale waliothubutu kumpinga wametoweka,” akitaja hasa ukatili wa mpwa wa Kikli, ambaye hivi karibuni “aliua watu kumi kwa damu baridi.”

Mshirika mwingine wa SSA, Ousama Al Masri Nejim, anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa kumtesa na kumbaka msichana mdogo, Dbeibah alisema.

“Kwa mara ya kwanza, ninaweza kuwaambia kuwa unaweza kutumaini kuwaondoa wanamgambo,” Dbeibah alisema, akiahidi kuwaondoa “wale wanaotanguliza uhujumu na ufisadi”.

Hata hivyo wakaazi wa Tripoli wameingia mitaani kwa siku mbili mfululizo, wakitaka Dbeibah ajiuzulu baada ya mapigano hayo mabaya.

Takriban watu 500 waliandamana siku ya Jumamosi baada ya maelfu ya waandamanaji wengine wanaoipinga serikali kukusanyika katika uwanja wa Mashujaa katikati mwa Tripoli siku ya Ijumaa kabla ya kuandamana kuelekea ofisi ya Waziri Mkuu.

Maandamano ya Ijumaa yalikuwa yamefuatwa na afisa mmoja wa polisi kupigwa risasi na washambuliaji wasiojulikana alipokuwa “akilengwa wakati akiilinda” ofisi ya Dbeibah, kulingana na serikali.

Tripoli iliona dalili za hali ya kawaida siku ya Ijumaa, na safari za ndege zilianza tena, maduka yakifunguliwa na watu wakirejea kazini.

Lakini pamoja na hayo, hali ya kisiasa katika mji mkuu imeendelea kuwa tete.

Vyombo vya habari vya ndani viliripoti mwishoni mwa Ijumaa kwamba mawaziri sita na naibu mawaziri kutoka baraza la mawaziri la Dbeibah wamejiuzulu. Ni wawili tu waliothibitisha kuondoka kwao.

Mabaraza kadhaa ya manispaa magharibi mwa Tripoli yalionyesha kuunga mkono maandamano hayo ya kutaka Dbeibah ajiuzulu.

Khaled al-Mishri, mkuu wa Baraza Kuu la Nchi katika mji mkuu, alisema ameanza mazungumzo na bunge lenye makao yake mashariki mwa nchi “kumchagua mtu wa kitaifa kuunda serikali mpya”.

Dbeibah, wakati huo huo, alikutana na wazee wa makabila katika mji mkuu siku ya Jumamosi na kusema serikali yake “inajaribu kujibu haraka” kuhusu matukio ya hivi majuzi katika jiji hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *