Mambo yanayowaathiri wanawake kwenye malezi

Dar es Salaam. Malezi ni jukumu la baba na mama. Mtoto anayelelewa kwa uwiano mzuri na baba na mama anakuwa mbali sana kimakuzi,  kimaendeleo na  kihisia tofauti na yule ambaye amekosa upande mmoja.

Pamoja na ukweli huu, wanawake wanabaki kuwa viungo muhimu sana kwenye malezi ya watoto.

Mtoto aliyekosa malezi ya mama anaweza kuwa tofauti sana na yule ambaye ameyapata malezi hayo.

Kutokana na mabadiliko ya maisha, yapo mambo mengi yanayoathiri ubora wa namna kina mama wanavyolea watoto wao. Hapa ninakuchambulia kwa kina mambo matatu muhimu.

Kumbukumbu za maisha ya awali

Utakubaliana na mimi kwamba wengi wetu tumepitia katika maisha ambayo yanaacha vitu vya kukumbukwa ndani yetu. Bahati mbaya baadhi ya vitu hivyo ni vyenye maumivu na machungu.

Kuna uwezekano mama mwenye mtoto au watoto akawa aliwahi kuteswa, kunyanyaswa, kutengwa, kubakwa, kusingiziwa, kusemwa vibaya, kutokubaliwa na ndugu au wakwe zake.

Mwanamke huyu anaweza kujitahidi sana kusahau mambo haya yenye hisia za machungu lakini ukweli ni kwamba kusahau kabisa sio rahisi.

Hisia hizi zinaweza kuathiri jinsi anavyo walea watoto wake. Anaweza kuwa mkali kupitiliza, au kuongea kikatili na watoto, au kutokuwa na ukaribu au urafiki na watoto wake.

Baadhi ya kumbukumbu zinaweza kumfanya asiwe mwenye kujali au asiye na upendo.

Ukiona kumbukumbu za zamani zinakutesa na kuathiri uwezo wako wa kulea watoto wako, jitahidi kufanya  mambo yanayokupa furaha na kutokumbuka yale yanayokuumiza muda wote.

Machungu, usumbufu wa ndoa na uhusiano

Kama tujuavyo ndoa nyingi zina changamoto. Unaujua ukweli pia kwamba kati ya mwanaume na mwanamke, kiumbe mwanamke huongozwa zaidi na hisia kuliko mwanaume.

Chochote chenye furaha kwenye uhusiano huinua moyo wake na kumfanya kujihisi aliyefanikiwa kuliko wote na chochote chenye machungu na karaha kumuumiza na kumfungulia milango yote ya chuki ndani yake.

Huwa nawaambia wanandoa, mwanamke aliyeumizwa hisia kamwe hawezi kuwa mlezi mzuri wa watoto wake, kwa sababu, hisia za machungu ni ngumu sana kuzizuia zisivuje na kuwaathiri watoto pamoja na wengine wanaomzunguka.

Baadhi ya mazingira ya kwenye uhusiano na ndoa ambayo yanaweza kuhusika kumpa usumbufu wa hisia mwanamke ni pamoja na kutokupata penzi alilotarajia kutoka kwa huyo waliyependana. Mabadiliko ya tabia ya mpenzi wake, ugomvi wa mara kwa mara kwenye ndoa, purukushani za mmoja kutokuwa mwaminifu na matarajio makubwa yasiyo halisi.

Wako wanawake ambao nimezungumza nao wakati wa ushauri wanasema ili kukabiliana na maumivu haya ya hisia kutoka kwenye ndoa,  wanaamua kujizamisha kwenye kuwa “bize” na kazi, biashara au majukumu mengine ili wasimkumbuke huyo mume wala kukumbuka usumbufu yake.

Wengine wamejiingiza kwenye makundi ya marafiki na hata ulevi. Yote haya yanawafanya watoto wanaolelewa na mama huyu kutelekezwa na kutojaliwa inavyopaswa.

Athari za kisaikolojia na hata kiafya ni kubwa kwa watoto wanaoishi katika mazingira haya. Ushauri hapa ni kujaribu kutafuta kuyazungumza yote yanayoleta shida kwenye uhusiano badala ya kuyafukia au kuyafunika huku mmoja anaumia na kuwaathiri watoto.

Kukosekana kwa urafiki na ukaribu wa kihisia baina ya mama na mtoto

Ni ukweli usiopingika kwamba kati ya baba na mama kwenye malezi, kwa familia nyingi mama huwa karibu zaidi na watoto kuliko baba.

Na hata kama baba yuko karibu zaidi bado utakuta anayetumia muda mrefu zaidi na watoto ni mama.

Kwa ukweli huu, endapo kuna kitu chochote kile ambacho kitamtenga mama huyu na watoto kwa muda mrefu,  basi ni wazi kabisa madhara makubwa ya kihisia, kisaikolojia na hata kiafya yanaweza kuonekana kwa watoto wake.

Baba anaweza asiwe na muda sana na watoto wake lakini madhara yake huwezi kuyalinganisha na mama asipokuwa na muda na watoto wake.

Baadhi ya mambo ya kawaida tu, tena mambo ya kila siku kwenye maisha yetu ambayo yanaweza kumkosesha mwanamke muda, ukaribu au urafiki na watoto wake ni pamoja na shughuli na “ubize” wa kila siku bila kuangalia uhitaji wa watoto.

Pia, tabia ya kumezwa sana na teknolojia pamoja na mitandao. Unakuta mama ana makundi ya “whatsapp” mengi na kote anataka kushiriki na asipitwe na chochote. Ni ngumu kabisa kuwa na ukaribu na mtoto katika hali hii.

Watoto nao pia wana kiu ya kuwa na muda na mama, hata kama hawana kitu cha kufanya au kuongea. Ule muda wa kuwa nao tu una manufaa makubwa sana kwao. Muda wa kucheza nao, kujibu maswali yao, kutaniana nao, kuwaangalia wakicheza wenyewe.

Vyote hivi huongeza urafiki baina ya mtoto na mama na kwa upande mwingine madhara ni makubwa pale ukaribu huu unapokosekana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *