Shida Simba ilikuwa hapa

Berkane, Morocco. Mabao mawili yaliyofungwa ndani ya dakika 15 za kwanza na RS Berkane katika mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Simba jana jijini Berkane yanaweza kuonekana yameiweka timu hiyo ya Morocco katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.

Hata hivyo, kiuhalisia shughuli huenda isiwe rahisi kwa mabingwa hao watetezi katika mechi ya marudiano na huenda ikakutana na matokeo ya kushangaza na wakajikuta wanapoteza taji lao mbele ya Simba ikiwa wataichukulia kiwepesi mechi ya marudiano itakayochezwa Jumapili, Mei 25 mwaka huu.

Kama Simba itarekebisha mapungufu kadhaa ambayo iliyaonyesha kwenye mchezo uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane, inayo nafasi ya kupindua meza kibabe na kumaliza kwa heshima mashindano hayo kwa kutwaa taji.

Shida ilikuwa hapa

Kabla ya mchezo huo wa kwanza, kocha wa Simba, Fadlu Davids aliwaonya wachezaji wake kuwa wanapaswa kuwa na umakini na tahadhari ya hali ya juu dhidi ya RS Berkane hasa katika dakika 20 za kwanza.

Inawezekana labda onyo hilo la Davids halikuwaingia vizuri wachezaji wa Simba na ndani muda uleule aliowapa tahadhari kuwa wawe makini, wakaruhusu nyavu zao kutikiswa mara mbili.

Mapungufu kadhaa yalionekana kuwa sababu ya Simba kuruhusu mabao ya mapema na la kwanza ni wachezaji kupoteza mipira katika maeneo hatarishi jambo lililowapa fursa RS Berkane kuwaadhibu na kuumaliza mchezo mapema.

Kulionekana kama baadhi ya wachezaji wa Simba hasa wa safu ya ulinzi ya Simba walianza mchezo wakiwa hawajiamini na hilo likasababisha wakose utulivu walipokuwa na mpira na walijikuta katika wakati mgumu zaidi pale mstari wa mbele wa RS Berkane ulipowafuata kwa kasi na nguvu kubwa ili kujaribu kuwatengenezea presha na wasiwasi.

Udhaifu mwingine wa Simba ulikuwa ni kuachia mianya mingi kwa wapinzani wao lakini pia baadhi ya wachezaji wa Simba hawakuwa na msaada katika kuutafuta mpira pindi walipoupoteza au ulipokuwa katika umiliki wa RS Berkane.

Kasoro nyingine ya Simba juzi ilikuwa ni kujaribu mara kwa mara kutengeneza mitego ya kuotea ambayo hata hivyo mingi ilivunjwa na safu ya ushambuliaji ya Berkane.

Chunga sana hawa

Mchezo wa marudiano nyumbani, Simba inapaswa kujiandaa kikamilifu kukabiliana na baadhi ya nyota wa RS Berkane ambao kwa kiasi kikubwa ndio walichangia kuiamua mechi ya kwanza.

Kiungo wa ulinzi kutoka Senegal, Mohamed Camara ndiye anaonekana kuwa moyo wa RS Berkane kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupora mipira na kuichezesha timu.

Camara ameonyesha uwezo mkubwa wa kupiga pasi na kuisukuma timu mbele na ndiye amekuwa akitumika kunyong’onyesha viungo wa timu pinzani.

Mchezaji mwingine ambaye inapaswa kuwa makini naye ni kiungo mshambuliaji Yassine Labhiri ambaye ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho na ana uamuzi wa haraka pindi awapo na mpira mguuni.

Historia haiongopi

Sio mara moja Simba ilifanikiwa kupindua matokeo na kusonga mbele kwenye mashindano ya klabu Afrika huku ikiwa imepoteza kwa mabao mawili au zaidi katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano.

Mwaka 1979, Simba ilifanya maajabu ya kuitupa nje Mufulila Wanderers ya Zambia kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-4 ambao ulipatikana katika namna ya kipekee na ya kushangaza.

Katika mchezo wa kwanza, Simba ilipoteza kwa mabao 4-0 nyumbani Dar es Salaam na katika mchezo wa marudiano uliochezwa Zambia, Simba ikaibuka na ushindi wa mabao 5-0.

Msimu huu wenyewe, kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba ilipindua meza mbele ya Al Masry ya Misri na kupata ushindi wa mikwaju ya penalti 4-1.

Katika mchezo wa kwanza huko Misri, Simba ilifungwa mabao 2-0 na mechi ya marudiano Dar es Salaam ikapata ushindi kama huo uliofanya mechi hiyo iamriwe kwa mikwaju ya penalti iliyoipa ushindi.

Vigogo wafunguka

Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu ametamba kuwa wanayo nafasi ya kupata matokeo mazuri nyumbani na kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.

“Tunakwenda kujipanga kwa mechi ya nyumbani. Haya ya leo yamekwisha na sasa tunahamishia nguvu yetu katika mechi ya marudiano tuweze kufanya vizuri na kutimiza lengo letu,” alisema Mangungu.

Kwa upande wa kocha wa Simba Fadlu Davids yeye alisema anaamini kila kitu kinawezekana kwenye mchezo wa pili kama wachezaji wake watazingitia kile ambacho wamefanya mazoezini.

“Hakuna kinachoshindana kwenye soka, kinachotakiwa ni wachezaji wangu kuelewa na kufuata kile ambacjho tunafundishana mazoezini.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *