Sita wafariki dunia kwa kufukiwa na kifusi mgodini, 11 waokolewa

Shinyanga. Wachimbaji sita wamefariki dunia kwa kufukiwa na kifusi ndani ya mgodi wa dhahabu uliopo katika Kijiji cha Mwakitolyo wilayani Shinyanga.

Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia Mei 17, 2025 wakati wachimbaji hao walipokuwa wakiendelea na kazi katika mgodi wa dhahabu unaomilikiwa na wawekezaji kutoka Chin,a ambapo wachimbaji 11 wameokolewa wakiwa hai na kuwahishwa  Hospitalini ya Mkoa wa Shinyanga kwa matibabu.

Akizungumza eneo la tukio leo Jumapili Mei 18, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amesema kati ya majeruhi 11 wanaopatiwa matibabu, mmoja tayari ameruhusiwa baada ya afya yake kuimarika na wengine 10 wakiendelea na matibabu.

Macha amesema miili ya watu watano iliopolewa jana na mwili mmoja umeopolewa leo, hivyo jumla ya miili iliyoopolewa kuwa sita.

Amesema askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga wanaendelea kushirikiana na wananchi katika shughuli ya uokozi.

Hadi sasa, bado haijajulikana kwa usahihi idadi ya watu waliokuwa ndani ya mgodi huo wakati ajali hiyo inatokea.

Kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchimbaji madini nchini, kila mtu anayeingia ndani ya mgodi anapaswa kuandikishwa jina, na haijafahamika mara moja ni kwa nini imekuwa vigumu kujua idadi halisi ya walioingia mgodini siku ya ajali.

Kutokana na hali hiyo, RC Macha ameagiza uokozi uendelee hadi watakapojiridhisha hakuna aliyeachwa chini ya kifusi. Mashine za kufukua udongo (Eskaveta) zinaendelea kufukua maeneo yanayodhaniwa kuwa na watu.

Endelea kufuatilia tovuti na mitandao ya Mwananchi kwa taarifa zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *