
LEO, JUMAPILI Yanga inacheza na JKT Tanzania mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga huku dakika 90 zikikamilika kutakuwa na mambo matatu yamepatiwa majibu.
Mchezo huo uliopangwa kuanza saa 10:00 jioni, unawakutanisha mabingwa watetezi Yanga wanaolisaka taji hilo kwa mara ya nne mfululizo, inakutana na JKT Tanzania inayolifukuzia kwa mara ya kwanza.
Jambo la kwanza linalotarajiwa kutokea leo ni kwamba JKT Tanzania ikishinda itaivua ubingwa Yanga na kuisogelea tiketi ya kimataifa.
Ishu ya pili Yanga ikishinda maana yake ni rasmi itaihakikishia Azam kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao kwani hadi sasa haina uhakika kutokana na nafasi yake kwenye ligi.
Mwisho kabisa, ni timu gani kati ya Yanga na JKT Tanzania itakubali kupoteza kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo msimu huu kwani hadi zinafika hapo, zimeshinda mechi zao zote za hatua zilizopita.
Mechi hii inakumbushia mara ya mwisho zilipokutana katika Ligi Kuu ambapo zilitoka suluhu (0-0), kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam ikiwa ni ya kwanza kwa Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa.
Yanga ilianza michuano hii ya FA hatua ya 64, kwa kuichapa Copco FC ya Mwanza mabao 5-0, kisha ikakutana na Coastal Union hatua ya 32 na kuiondosha kwa kuifunga 3-1 na kutinga 16 bora ikaenda kuitoa Songea United ya Ruvuma kwa kichapo cha mabao 2-0.
Hatua ya robo fainali, Yanga ikakutana na Stand United inayoshiriki Ligi ya Championship na kuichapa mabao 8-1, huku nyota wa timu hiyo, Stephane Aziz KI akifunga ‘Hat-Trick’.
Kwa upande wa JKT Tanzania, ilianzia pia hatua ya 64 bora kwa kuitoa Igunga United ya Tabora kwa mabao 5-1, kisha ikaing’oa Biashara United inayoshiriki Ligi ya Championship ikiifunga 2-1, ikafuzu 16 bora na kuiondosha Mbeya Kwanza kwa mabao 3-0.
Katika hatua ya robo fainali, kikosi hicho cha maafande kikafuzu na kwenda nusu fainali baada ya kutumia vyema Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ambao ndio wa nyumbani kufuatia kuichapa Pamba Jiji inayoshiriki Ligi Kuu Bara kwa mabao 3-1.
Timu itakayoshinda mchezo huu itamsubiria mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya Simba na Singida Black Stars zitakazokutana Mei 28, 2025, kwenye Uwanja wa Tanzanite kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara.
Katika timu zote nne zilizofuzu, ni Yanga na Simba zilizotwaa ubingwa wa michuano hiyo tangu msimu wa 2015-2016, jambo linalosubiriwa kuona kama kuna nyingine itauvunja mwiko huo na kuandika rekodi mpya, au miamba hiyo itaendeleza ubabe.
Tangu michuano hiyo iliporejea msimu wa 2015-2016, Yanga ndio timu inayoongoza kwa kuchukua ubingwa huo mara nyingi zaidi, baada ya kufanya hivyo mara nne, ikifuatiwa na wapinzani wao wakubwa Simba, waliolichukua taji hilo mara tatu.
Mbali na Yanga na Simba zilizochukua ubingwa tangu msimu wa 2015-2016, timu nyingine ni Mtibwa Sugar na Azam FC ambazo zote tayari zimetolewa, jambo linalosubiriwa kuona kama JKT Tanzania au Singida Black Stars zitajiandikia rekodi mpya.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi alisema licha ya ugumu anaoenda kukutana nao, ila mojawapo ya malengo makubwa ya kikosi hicho ni kufuzu hatua ya fainali na kwenda kutetea tena ubingwa wa michuano hiyo.
“Mchezo wa hatua ya nusu fainali dhidi ya JKT Tanzania ni mgumu na wa aina yake, lakini mchezo wa aina hii matokeo yake lazima ni ushindi tu, tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunasonga mbele na kufika kwenye hatua ya fainali.
“Tutamkosa Yao (Kouassi Attohoula) na Boka (Chadrack) ambao bado wanaendelea na matatibu ya majeraha pamoja na Mwamnyeto (Bakari) ambaye ana adhabu, wachezaji wengine wote wapo kwenye hali nzuri,” alisema Hamdi.
Kwa upande wa Kocha wa JKT Tanzania iliyowahi kutwaa kombe hilo ikifahamika kwa jina la JKT Ruvu mwaka 2002, Ahmad Ally, alisema lengo ni kuchukua ubingwa huo ili kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, licha ya ubora wa wapinzani wao.