
BERKANE: KATIBU mkuu wa zamani wa Simba, Hassan Hassanoo ametazama vizazi vitano tofauti vya Simba vilivyotikisa kimataifa, lakini amekichagua cha sasa kuwa bora zaidi.
Hassanoo amesema alikiona kizazi kilichofika hatua ya nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika 1974, kilichotinga fainali ya Kombe la CAF 1993, kilichoingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2003, kilichotinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2018/2019 na 2020/2021 na hiki cha sasa kilichoingia fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Akilinganisha vizazi hivyo, Hassanoo alisema cha sasa kiko vizuri zaidi kwa vile kinaundwa na wachezaji wenye ubora wa hali ya juu na wanaofanyia vyema kazi majukumu wanayopewa na benchi la ufundi.
“Hiki kizazi cha sasa ni kizazi bora zaidi kati ya vyote vilivyowahi kuitumikia Simba. Sisemi kwamba hivyo vya nyuma havikuwa bora ila hiki cha sasa ni kizuri zaidi,” alisema.
“Hilo linachangiwa na ukweli kwamba kizazi hiki kimejengwa kwa kutumia makosa na udhaifu wa vizazi vya nyuma, hivyo kimerekebisha mengi ambayo yalitufanya tusifikie kile tulichokuwa tunakitarajia.”
Hassanoo alisema kingine ambacho kinafanya kizazi cha sasa akione kitaifikisha Simba katika nchi ya ahadi ni ubora wa benchi la ufundi chini ya kocha Fadlu Davids.
“Tuna mwalimu bora sana ambaye yeye na wasaidizi wake wanaifundisha timu kisasa na mbinu zake zimekuwa nzuri. Ni kocha ambaye anajua timu icheze vipi na kwa wakati gani,” alisema Hassanoo.
Kiongozi huyo zamani amewaomba mashabiki wa Simba kuendelea kukisapoti kikosi chao kwani kinaonyesha mwanga wa kutamba kwa muda mrefu katika mashindano ya klabu Afrika na mengine ya ndani.