
Dar es Salaam. Wakati mwaka 2024 ukitajwa kwa kuvunja rekodi katika uwekezaji tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), viwanda, usafirishaji, majengo ya biashara, mawasiliano na kilimo ndiyo sekta zilizovutia wawekezaji wengi zaidi.
Maeneo hayo matano pekee yalibeba mtaji wa Sh21.36 trilioni kati ya Sh24.66 trlioni ziliwekezwa katika mwaka mzima wa 2024 huku miradi ikifikia 901 kutoka 207 mwaka 2020.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na TIC hivi karibuni viwanda ndiyo sekta kinara kwa kuvuta uwekezaji ambapo zaidi ya Sh10.79 trlioni ziliwekezwa katika kipindi hicho ikifuatiwa na sekta ya usafirishaji iliyochukua mtaji wa Sh3.59 trilioni.
Sekta namba tatu ilikuwa majengo ya biashara ambayo ilichukua Sh3 trilioni, mawasiliano mtaji wa Sh2.14 trilioni na kilimo kikibeba mtaji wa Sh1.82 trilioni.
Hata hivyo, licha ya Kilimo kushika namba tano kati ya sekta zilizopata uwekezaji mkubwa lakini ndiyo kinaongoza kwa kuzalisha ajira nyingi.
Kilimo kinatarajiwa kuzalisha ajira 125,760 kati ya ajira 212,293 zinazotarajiwa kuzalishwa pindi miradi yote 901 iliyowekezwa katika mwaka 2024 itakapoanza kufanya kazi.
Hiyo ni sawa na kusema asilimia 59.2 ya ajira zote zilizotarajiwa zilitoka katika kilimo huku sekta ya viwanda iliyoongoza kwa kubeba mtaji mkubwa ikitarajiwa kutengeneza ajira 45,883, usafirishaji ajira 18,780, mejengo ya biashara ajira 7,415 na utalii ajira 6,949.
Wakulima wanasemaje
Akizungumzia suala hilo, Maganga Masumbuko ambaye ni mkulima kutoka mkoani Mbeya amesema sekya hiyo inahitaji kutupiwa jicho zaidi kwani ndiyo inayoajiri watu wengi kuliko eneo lingine lolote.
“Huku hihitaji elimu kubwa bali kujua msimu gani mzuri unapaswa kupanda, mbegu kuendana na eneo na ukipata eneo lenye mifumo ya umwagiliaji ndiyo umefanikiwa kabisa kimaisha tofauti na maeneo mengine,” amesema Masumbuko.
Anasema licha ya kutopewa uzito na kutajwa katika mijadala mbalimbali kama ilivyokuwa sekta nyingine kama utalii ambayo imeundiwa hadi mkakati lakini wakulima wameendelea kuajiri idadi kubwa ya watu na sasa kile wanachokizalisha kimekuwa chanzo cha fedha za kigeni kuja Tanzania.
“Tunauza mchele, mahindi na mazao mengine nje unaweza kuona ni fursa kiasi gani tuliyonayo, nadhani ni wakati sasa kilimo kiongezewe nguvu zaidi ili hivyo viwanda tunavyoona wanawekeza vipate malighafi za kutosha kuzalisha bidhaa zao, isijekuwa viwanda vipo kwetu malighafi watafute nje ya nchi kwa sababu sisi hatuzalishi kiasi cha kutosha,” amesema.
Alitumia nafasi hiyo kuhamasisha uwezekazi zaidi hasa katika miundombinu ya umwagiliaji ili wakulima waache kutegemea misimu ya mvua jambo ambalo litafanya hata wale wanaotegemea ajira za sekta hiyo kuwa na misimu ya kuingiza kipato.
Hili linasemwa wakati ambao Serikali iliweka malengo ya kufikia hekta 1,200,000 za kilimo cha umwagiliaji ifikapo mwaka huu ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha sekta ya kilimo na kuongeza tija.
Hilo lilienda sambamba na uwekezaji katika miundombinu ya maji ambapo mabwawa 100 yanatarajiwa kujengwa huku sambamba na kuchimba visima 150 katika kila halmashauri ili kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji na kuongeza uzalishaji wa kilimo.
Kwa upande wake, Sabinus Waniu kutoka Morogoro amesema ni vyema kuwapo kwa mkakati wa kuhakikisha mazao yanayozalishwa yanaendana na uwekezaji unaofanywa na viwanda.
“Ifanywe tathmini kama wanazalisha siagi basi watu waambiwe karanga kiasi gani inahitajika, kama mvinyo watu waambiwe zabibu kiasi gani zinahitajika ili malghafi zisikosekane, viwanda vikafanya kazi chini ya kiwango na hivyo ndiyo tija katika kilimo inaweza kuonekana na watu wengi zaidi kuajiriwa,” amesema Waniu ambaye ni mkulima.
Katika uchumi
Mtaalamu wa uchumi, Profesa Aurelia Kamuzora amesema kilimo na viwanda ni kama yai na kuku akiwa anamaanisha kuwa ni ngumu kutenganisha vitu hivyo viwili ukiwa unataka kuendelea.
Amesema kilimo ni kama yai ambalo linamuhitaji kuku ambaye ni viwanda ili aweze kuliboresha na kupata kifaranga kipya (bidhaa).
“Kilimo kinahitaji sana viwanda katika uongezaji wa thamani ili kufanya kilimo kuoekane katika kuchangia pato la taifa na sasa kila mwekezaji anapokuja anaanzisha kiwanda ambacho kitategemea malighafi za kilimo hivyo ni vyema nguvu zaidi ziongezwe,” amesema Profesa Kamuzora.
Amesema ni vyema sasa hata wakulima waanze kuonekana kama wawekezaji kwa sababu ndiyo wanafanya viwanda viwepo na kuanza kubadili mtazamo na kuanza kuwatambua wakulima kama wawekezaji ili kuwaongezea morali ya kuzalisha zaidi.
“Kukua kwa kilimo kunajionyesha katika viwanda vinavyotegemea malighafi kutoka sekta hiyo,” amesema.
Uboreshaji wa miundombinu na mazingira ya kilimo nalo ni jambo ambalo liligusiwa tena ikiwemo kuwapa mbegu bora ili kuhakikisha wanalima kwa kiwango kikubwa.
Wakati haya yakisemwa, Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji alipokuwa akiwasilisha bajeti yake ya mwaka 2025/2026 alisema moja ya jambo watakalolifanya mwaka ujao wa fedha ni kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kazi.
“Pia ofisi ya mipango na uwekezaji itaenedelea kuandaa Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II) ili kujumuisha maeneo mapya yaliyojitokeza na yanayoendelea kujitokeza kutokana na mabadiliko ya uchumi wa dunia na teknolojia,” alisema Mkumbo.
Hayo yanaenda sambamba na kuratibu na kusimamia uwekezaji katika Kanda Maalum za kiuchumi na kongani za viwanda.
Mikoa vinara kwa uwekezaji
Kwa mujibu wa TIC mkoa wa Dar es Salaam ndiyo ulioongoza kwa kupata miradi mingi ya uwekezaji huku mtaji wa Sh11.74 trilioni ukielekezwa katika jiji hilo la biashara.
Pwani ilipata uwekezaji wa Sh3.30 trilioniRuvuma Sh1.59 trilioni, Mwanza Sh1.54 trilioni na Morogoro ikipata mtaji wa Sh1.18 trilioni.
Kwa upande wa nchi vinara, China ndiyo ilishika namba moja kwa kuleta fedha Tanzania ambapo katika uwekezaji wa moja kwa moja waliwekeza Sh2.80 trilioni huku miradi ya ubia nchi hiyo ikileta mtaji wa Sh5.61 trilioni.
Vietnam ilikuwa nchi ya pili kwa kuleta mtaji wa Sh2.08 trilioni, Mauritius ilileta Sh2.06 trilioni, Jumuiya za falme za kiarabu Sh1.87 trilioni na Umoja wa ulaya ukiweka mtaji wa Sh1.04 trilioni.