
Mwanza. Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) imewataka wananchi na wadau wa maendeleo nchini Tanzania kujenga utamaduni wa kusoma ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa na ofisi hiyo inapobaini udhaifu, mapungufu na ubadhirifu kwenye taasisi na miradi.
Akizungumza leo Jumamosi Mei 17, 2025 wakati wa mafunzo maalumu kwa asasi za Kiraia mkoani Mwanza kuhusu ripoti za ukaguzi wa serikali za mitaa na ukaguzi wa ufanisi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya CAG, Focus Mauki amesema kuna haja ya jamii kuondoa dhana Serikali haifanyii kazi taarifa na mapendekezo ya CAG.
“Ukisoma ripoti hizi unaona zina muundo tofauti. Zipo zinazotoa mapendekezo mapya ya CAG, na zipo zinazonyesha hatua za utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa kwenye ripoti zilizopita…kwa hiyo kusema hakuna utekelezaji si sahihi,” amesema Mauki.
Amebainisha kazi ya CAG imeelezwa wazi kwenye Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo jukumu lake ni kufanya ukaguzi angalau mara moja kwa mwaka, ingawa hufanya zaidi na kuwasilisha ripoti hizo serikalini.
“Baada ya ripoti kuwasilishwa, Serikali huipeleka Bungeni ambako kamati husika za Bunge ndizo zinazowaita maofisa masuuli na kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo. Kwa hiyo mfumo wa uwajibikaji upo. Serikali ipo, Bunge lipo, na wadau mna jukumu la kufuatilia pia,” amesema.
Mshiriki wa mafunzo hayo, Kisiel Wambura amependekeza taarifa za CAG zisibaki kwenye mikono ya taasisi za kiraia pekee, bali ziwasilishwe kwa wananchi kupitia majukwaa ya kijamii kama vile matamasha na makongamano ya wazi.
“Nia ni kuwafikia wananchi moja kwa moja, wajue ripoti hizo zinasema nini kutoka kwa ofisi ya CAG yenyewe,” amesema.
Naye, Josephine Mihama amesisitiza umuhimu wa kuwasilisha taarifa hizo kwa lugha rahisi na kwa njia zinazowafikia wananchi wa kawaida, hususani vijijini na kwenye mbao za matangazo.
“Tumeona Serikali inawajibika na mapendekezo ya CAG yanafanyiwa kazi, na hii inawafanya watumishi wa umma kuboresha huduma wanazotoa. Tukipeleka taarifa hizi kwa lugha rahisi hadi ngazi za mitaa, tutajenga imani kwa Serikali na kuongeza ushirikiano kwenye ukusanyaji wa mapato,”amesema Mihama.
Huku, akipongeza hatua ya NOAT kuchapisha taarifa hizo kwa lugha ya Kiswahili, amesema usambazaji wa taarifa za CAG kwa uwazi na lugha inayoeleweka unasaidia kuongeza uelewa wa umma kuhusu matumizi ya fedha za umma, na hivyo kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na wananchi katika kusimamia maendeleo na ukusanyaji wa mapato.