Ofisa tabibu, mmiliki wa zahanati mbaroni tuhuma wizi wa vifaatiba

Mwanza. Polisi mkoani Mwanza linawashikilia na kuwahoji watu wawili akiwemo ofisa tabibu wa Hospitali ya Wilaya ya Sengerema, Nyanda Thomas (35) kwa tuhuma za kuiba vifaatiba vyenye thamani ya zaidi ya Sh28.5 milioni katika hospitali hiyo.

Mtuhumiwa mwingine ni mfanyabiashara na mmiliki wa Chuo cha Afya na Zahanati binafsi iitwayo ELABS iliyopo wilayani humo, Novart Felician (36).

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa leo Jumamosi Mei 17, 2025 imesema tukio la wizi lilitokea Aprili 4, 2025 saa 2 asubuhi katika hospitali hiyo iliyopo mtaa na kata ya Mwabaluhi.

Amesema baada ya tukio hilo kuripotiwa katika kituo cha polisi, jeshi hilo lilianza upelelezi na kufanya ufuatiliaji wa kina na ilipofika Mei 15, 2025 saa 4 asubuhi lilifanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wakiwa na vifaa hivyo.

Ametaja vifaa tiba vilivyoibiwa ni vifaa vitano vya kufuatilia mapigo ya moyo ya mtoto akiwa tumboni, komputa moja, kifaa cha kurekebisha mapigo ya moyo, mashine mbili za kuingiza maji mwilini, vifaa viwili vya kutoa dawa kwa njia ya mvuke, pampu mbili za sindano na mashine nne za kupima shinikizo la damu.

“Aliyeanza kukamatwa alikuwa ni Nyanda baada ya kumhoji ikabainika ni kweli alihusika na wizi wa vifaa hivyo…lakini katika ufuatiliaji wetu tuliweza kubaini pia vifaa hivyo vingine vilikuwa vimeuzwa kwa mfanyabiashara na mmiliki wa zahanati,” amesema Mutafungwa.

“Watuhumiwa hawa wote wameshakamatwa na sasa uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea. Tunaendelea kufuatilia tukio hilo ili kuwabaini washiriki wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha tukio hilo la kiharifu ingwa vile vifaa vyote vilivyotajwa kuibiwa na uongozi wa hospitali hiyo jeshi la polisi limefanikiwa kuvikamata,” amesema.

 Amesema jeshi hilo litakapokamilisha uchunguzi wake, watuhumiwa  watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo huku akiwataka wafanyakazi wa hospitali kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa kuzingatia maadili yao kwa kutojihusisha na wizi unaorudisha nyuma jitihada za Serikali za kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *