
Dodoma. Usemi wa siku ya kufa nyani miti yote huteleza unaakisi namna Amos Nyamanga alivyojikuta akiongezewa kifungo hadi cha maisha jela alipokata rufaa kupinga kifungo cha miaka 30 jela.
Mara zote mshtakiwa anapokata rufaa kwenda mahakama ya juu zaidi kupinga adhabu aliyopewa na mahakama ya chini, anatarajia kupata ahueni, ikiwamo kuachiwa huru lakini si kwa Nyamanga aliyejikuta adhabu ikiongezwa.
Awali, mwaka 2022 Nyamanga alitiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya Dodoma kwa kosa la kumlawiti mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14, akakata rufaa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma, iliyobariki kifungo hicho.
Hakuridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu akakata rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania, akiegemea sababu 19 kuishawishi mahakama imwachie huru, badala yake ameongezewa kifungo na kuwa cha maisha jela.
Hukumu hiyo ilitolewa Mei 15, 2025 na jopo la majaji Winfrida Korosso, Sam Rumanyika na Abdul-Hakim Ameir Issa, ambao waliitupa rufaa ya mrufani, wakaenda mbali zaidi na kuongeza kifungo hadi cha maisha jela.
Tukio la ulawiti
Ushahidi wa upande wa Jamhuri ulieleza Aprili 12, 2021, Nyamanga alimlawiti mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 katika Kijiji cha Sasajila wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma kinyume cha kifungu 154 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Mrufani alikuwa akiishi na mtoto huyo ambaye ni mpwa wake kama mfanyakazi wa nyumbani hadi siku ya tukio alipoamua kumrudisha kwa wazazi wake, lakini njiani alimpeleka kwenye pagale na kumlawiti kisha kumuonya asiseme.
Mtoto alipofika nyumbani, alimweleza kila kitu mama yake, ambaye naye alimweleza mume wake aliyetoa taarifa polisi. Mtoto alipelekwa Hospitali ya Mvumi ilikothibitishwa ameingiliwa kinyume cha maumbile.
Nyamanga alitiwa mbaroni na polisi na kuhojiwa akakiri kutenda kosa lakini wakati wa usikilizwaji wa kesi alikana na kupinga ushahidi wa shahidi wa nne kuwa ulikuwa wa uongo na wa kujikanganya.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama ya Wilaya Dodoma iliona upande wa Jamhuri ulithibitisha shitaka pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo, hivyo kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela.
Hakuridhika na hukumu akakata rufaa Mahakama Kuu Dodoma akitegemea hukumu itabatilishwa na kuachiwa huru, lakini haikuwa hivyo kwani ilibariki kifungo ndipo akenda Mahakama ya Rufaa.
Hoja za rufaa, majibu ya DPP
Akiwakilishwa na wakili Ezekiel Mwakapeje, mrufani alidai ushahidi wa mtoto ulikuwa na dosari na ulipaswa kufutwa kwa sababu wakati akitoa ushahidi alikuwa na umri wa miaka 14, lakini hakula kiapo kwa mujibu wa sheria.
Hoja nyingine ni kuwa akili na uwezo wake haukupimwa kabla ya kuanza kutoa ushahidi na hakutoa ahadi ya kusema ukweli na si uongo kama inavyotakiwa katika kifungu cha 127(2) cha Sheria ya Ushahidi ya mwaka 2022.
Kuhusu hoja ya tatu na ya nane ambazo ziliwasilishwa kwa pamoja, Mwakapaje alieleza mrufani alipelekwa mahakamani Juni 7, 2021 bila maelezo yoyote, hilo likionyesha tukio hilo halikuwapo au halikuripotiwa kabisa.
Alisema maelezo ya onyo ambayo mrufani aliyaandika polisi Aprili 13, 2021 yalikiuka sheria ya ushahidi na kuiomba mahakama kupuuza maelezo hayo na kuona kuwa hoja hizo mbili zina mashiko na wamwachie huru mrufani.
Akijibu hoja hizo, wakili Kulwa alisema kesi ya upande wa mashtaka ilithibitishwa pasipo kuacha shaka na kuongeza kuwa, ingawa mwathirika alikuwa na umri wa miaka 14 hakula kiapo, lakini alitoa ushahidi baada ya kuahidi kusema ukweli.
Wakili alisema mtoto huyo alitoa ushahidi kwa usahihi na kwa umakini na kueleza kuwa ingawa hati ya mashtaka haikuonyesha umri wake, hiyo ilimnufaisha mrufani ndiyo maana alifungwa kifungo cha miaka 30 badala ya maisha.
Kuhusu kuchelewa kufikishwa mahakamani, wakili Kulwa alisema wakati wa usikilizwaji wa kesi, mrufani alipata fursa ya kuwahoji mashahidi lakini alishindwa kufanya hivyo na kueleza hata maelezo ya onyo aliyokiri, aliyatoa kwa hiyari.
Hukumu ya majaji
Baada ya kusikiliza hoja 19 za rufaa na za Jamhuri kuzipinga, majaji wa Mahakama ya Rufaa wamesemwa wajibu wao ni kupima kama kesi ya upande wa Jamhuri ilithibitishwa ama la na wataanza na hoja ya tatu ya rufaa.
Majaji wamesema kuna hoja kuwa maelezo ya onyo ambayo mshtakiwa alikiri kutenda kosa yalichukuliwa kimakosa, lakini wanaona mrufani alikamatwa mara tu baada ya tukio Aprili 12, 2021 na kupelekwa polisi na kuandika maelezo Aprili 13.
“Maelezo yake aliyatoa siku moja tu baada ya kukamatwa. Hata hivyo, alifikishwa mahakamani siku 25 baadaye yaani Mei 7, 2021,” imeeleza hukumu ya majaji na kuongeza:
“Tunakubaliana na wakili Mwakapeje kwamba mrufani hakuandika maelezo ndani ya saa nne tangu kukamatwa. Malalamiko yake yana mashiko. Zaidi kukosekana kwa maelezo kwa nini ilichukua siku 25 kumfikisha kortini.
“Hata hivyo, utetezi wa mrufani kuwa alikuwa amelewa haukuwa na msaada kwake. Hivyo alijutia. Mrufani alikuwa hakatai kutenda kosa lakini alidai ni kutokana na mazingira ya ulevi. Utetezi huu haukukidhi vigezo vya utetezi,” imeeleza hukumu.
Kuhusu Jamhuri kuthibitisha shtaka, majaji wamesema kosa la ulawiti lilithibitishwa vizuri kwa sababu kuingiliwa kulithibitishwa na daktari na ushahidi wa mrufani mwenyewe ulioana na ule wa mtoto aliyelawitiwa.
Majaji wamesema hata umri wa mtoto ambao ni kigezo muhimu ulithibitishwa na mama yake ambaye alieleza alizaliwa mwaka 2007 na alikuwa kama mjomba wake, mrufani alipaswa kufahamu umri ambao ulikuwa miaka 14.
Kuhusu adhabu, majaji wamesema wanakubaliana na hoja za wakili Kulwa kuwa mrufani alipewa adhabu isiyostahili na kutumia mamlaka waliyonayo kama Mahakama ya Rufaa kubadili kifungo hicho kutoka miaka 30 hadi maisha jela.