Kibano chaja usajili wahudumu wa mabasi

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imeanza ukaguzi wa utekelezaji wa sheria na kanuni kwa watoa huduma wa usafiri wa mabasi ya masafa marefu, ikiwa ni sehemu ya kusimamia usajili na uthibitishaji wa wahudumu wa vyombo vya moto vinavyotoa huduma kibiashara.

Hatua hiyo inatekelezwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)(e) cha Sheria ya Latra, Sura ya 413 na kanuni ya 22(9) ya Kanuni za Leseni za Usafirishaji wa Abiria na kanuni ya 20(1)(d) ya Kanuni za Usajili na Uthibitishaji wa Madereva wa magari ya biashara, zote za mwaka 2020.

Katika taarifa iliyotolewa leo Mei 17, 2025 na Msemaji wa Latra, Salum Pazzy kuanzia Juni 2, 2025, adhabu zitaendelea kutolewa kwa mabasi yatakayobainika kuajiri wahudumu ambao hawajasajiliwa, licha ya kutolewa kwa muda wa kutosha wa maandalizi.

“Julai, 2023 tulizindua mafunzo kwa wahudumu wa mabasi na Agosti 14, 2024 tulitangaza Desemba 31, 2024 kuwa mwisho wa watoa huduma kutumia wahudumu wasiosajiliwa,” amesema.

Pazzy amesema wamiliki na wahudumu wanatakiwa kuhakikisha wanawasilisha maombi ya usajili kupitia tovuti ya rmims.latra.go.tz au kufika ofisi yoyote ya Latra iliyo karibu nao wakiwa na nakala ya cheti cha mafunzo na namba ya Kitambulisho cha Taifa (Nida).

Amesema mafunzo hayo ya muda mfupi hutolewa na taasisi zenye vibali vya Serikali zikiwamo Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), na Chuo cha Ufundi Arusha.

Latra imesisitiza lengo la hatua hiyo ni kuongeza usalama, nidhamu na ufanisi katika sekta ya usafirishaji nchini, huku ikiendelea kutoa elimu kwa wadau wote wa sekta hiyo ili kuhakikisha utekelezaji wa sheria unafikiwa kwa mafanikio.

Kauli ya Taboa

Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kimesema kimeanza mazungumzo na Latra kwa lengo la kuongezwa muda wa utekelezaji wa utoaji mafunzo kwa wahudumu wa mabasi ili kuepusha adhabu zinazoweza kutolewa kwa kutokamilisha masharti hayo mapema.

Akizungumza na Mwananchi, Msemaji wa Taboa, Mustafa Mwalongo amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wahudumu wote wanapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo muhimu.

“Hili jambo ni jipya na wahudumu wapo wengi wanaotakiwa kusoma. Kwa hiyo tumeanza kufanya mazungumzo na mamlaka ili kutuongezea muda kabla ya kuanza kutoa adhabu,” amesema.

Selina Mselemu, mhudumu katika kampuni ya mabasi yanayofanya safari kati ya Dar es Salaam na Mbeya, amesema mafunzo yameanza kuleta mabadiliko chanya katika tasnia ya usafirishaji, kwani yanawapa ujasiri na dhamira ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

“Hii imesaidia ile tabia ya mwenye gari kukufukuza kazi muda wowote kupungua, kwa sababu anajua si kazi nyepesi kupata mhudumu kama ilivyokuwa awali, alikuwa na uwezo wa kuchukua hata ndugu yake kutoka kijijini na kumuweka,” amesema.

Agosti 26, 2023 Gazeti la Mwananchi na mitandao yake ya kijamii liliripoti kuhusu adha wanazopitia wahudumu kwenye mabasi.

Katika ripoti hiyo maalumu, baadhi ya wahudumu (makondakta) wanawake walieleza licha ya mafanikio wanayopata kupitia kazi hiyo, pia wamekuwa wakinyanyaswa kutokana na kutokuwapo mikataba, pia kulipwa ujira usiotosheleza hata mahitaji yao wawapo safarini.

Wapo waliolalamika kushushwa kwenye basi pasipo sababu za msingi, baadhi wakishushwa hata maeneo ya porini.

Novemba 12, 2024 katika hafla ya ugawaji wa kadi kwa wahitimu wa mafunzo ya huduma katika vyombo vya usafiri, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile aliiagiza Latra kusimamia jambo hilo kuhakikisha wamiliki wa mabasi wanazingatia utaratibu wa utumishi na ajira nchi.

“Lakini hili ninaweza kusema ni aibu kwetu kama Latra mnaweza kuwa na taarifa za mtu mwenye chombo akamshusha muhudumu njiani akaendelea kufanya shughuli zake nadhani inabidi tujitafakari,” alisema.

Kihenzile aliwataka Latra kufuatilia na kukomesha vitendo vya namna hiyo kwani havikubaliki duniani wala mbinguni, akihoji mtu akishushwa njia na akidhurika inakuwaje.

Mwenyekiti wa Bodi ya Latra, Ahmed Mohamed Ame katika mkutano huo alisema hadi kufikia Oktoba, 2024 zaidi ya wahudumu 750 wamepatiwa mafunzo na wahudumu 174 wamekidhi vigezo na kusajiliwa Latra.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *