
Arusha. Mchungaji wa Kanisa la Huduma ya Kristo lililopo Mtaa wa FFU Kata ya Muriet mkoani Arusha, Steven Jacob (35), aliyetekwa na watu wasiojulika alipotoka nyumbani kwake asubuhi ya Mei 16, 2025 amesimulia alivyookolewa na walinzi wa mashamba ya ngano.
Akizungumza akiwa kanisani leo Jumamosi Mei 17, 2025 amedai watu waliomteka walijitambulisha kwake kuwa maofisa wa polisi lakini hawakumuonyesha vitambulisho wakidai wanampeleka kituo kikuu cha polisi.
Amesema kutokana na namna walivyomchukua alielewa ametekwa kwani hawakuwa na vitambulisho na hawakutaka amuage mtu, badala yake walimchukua na kumfunga vitambaa viwili usoni na pingu mikononi, ndipo alipopiga kelele kuwa anatekwa, kisha watu hao wakamrusha kwenye gari na kuondoka naye kwa kasi.
Awali, Jacob Gumbo, baba mzazi wa Steven, ambaye ni balozi wa nyumba 10 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na jirani ambaye alishuhudia tukio hilo, walisema waliomteka walikuwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser lisilokuwa na namba za usajili.
Walisema mchungaji huyo alikokotwa kwa nguvu, huku akipiga kelele kwamba anatekwa kisha akatupwa kwenye gari lililoondoka eneo hilo kwa kasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia tukio hilo simu yake iliita bila kupokewa na hata ujumbe mfupi wa maneno (sms) aliotumiwa haukujibiwa.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amesema tukio hilo linafanyiwa upelelezi wa kina kujua undani wake na chanzo chake.
“Tumeshaanza uchunguzi wa tukio la kijana kuchukuliwa na hao watu na tayari tuko hatua nzuri, tutawajulisha kitakachoendelea,” amesema Mkude.
Kumekuwa na kilio kuhusu matukio ya utekaji nchini, la hivi karibuni likiwa la kutekwa mwanaharakati na kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdude Nyagali ambaye kwa siku 16 sasa hajapatikana.
Mdude alivamiwa na kupigwa nyumbani kwake mtaa wa Iwambi, jijini Mbeya na watu wanaodaiwa kuwa askari polisi Mei 2, 2025. Jeshi la Polisi katika taarifa baada ya tukio hilo lilisema linafanya uchunguzi.
Simulizi ya Steven
Mchungaji huyo amedai waliomteka walimpeleka hadi eneo la West Kilimanjaro wilayani Siha mkoani Kilimanjaro ambako walichukua simu zake za mkononi wakimtaka afute picha mjongeo (video) alizokuwa amepandisha kwenye mtandao wa Youtube.
“Naomba nisiongee mengi kwa sababu ni ishu za mtandao nilizo post Youtube. Baada ya kunipiga na kuchukua baadhi ya maelezo ambayo nafikiri nisingependa kuyaongea, baada ya pale nikasikia kama wananipeleka mahabusu ila haikuwa hivyo, wakanipeleka porini West Kilimanjaro.
“Walivyotaka nifute video kwa bahati mbaya bando lilikuwa limeisha, ikabidi wafanye mpango wapate bando, wakasema wawili au mmoja abaki na mimi halafu wengine wakatafute bando ili nifute video,” amesema.
Mchungaji huyo amesema watu hao walimwambia alale chini wakamkanyaga shingoni, mmoja akawaambia wenzake wanamuachaje hapo.
Amesema mambo mengine hawezi kuzungumza zaidi ila walimuacha wakaondoka na simu yake.
“Walivyoondoka nikaanza kubiringita na kutembea kwa magoti hadi barabarani nikafika barabarani pakatokea bodaboda alivyoona ile hali akapita. Lori la mafuta nalo likaogopa.
“Wakaja watu wanaolinda tembo wasiingie kwenye mashamba, nikajitambulisha mimi mtumishi wa mtandaoni nimetekwa nimetupwa huku nisaidieni, mmoja alikuwa mwoga kesi isije kuhamia kwao, ila wakanisaidia. Nikaomba simu ili niwajulishe watu niko hai,” amesema.
Mchungaji huyo amesimulia: “Walinipeleka kwenye kambi yao na baadaye wakaniambia wale watu wamerudi kule kama wanamtafuta, wakafanya mpango nikatolewa nikaenda sehemu nyingine, naomba mengine nisiongee.”
Amedai waliomteka wamempiga kwa rungu sehemu mbalimbali, zikiwamo nyayo na makalio.
“Walinipiga nikajua itakuwa mwisho ila namshukuru Mungu nimerudi salama, nina maumivu makali hata kutembea siwezi,” amesema.
Amesema kwa sasa hawezi kuzungumza masuala mengi kuhusu tukio hilo ila anachojua ni unabii aliopandisha kwenye mtandao wa Youtube.
“Waliniuliza nani yuko nyuma yako nikawaambia video zinaeleza mimi ni mtafsiri wa ndoto baada ya hapo kingine ambacho nikaulizwa kwa nini usiende kwa wahusika moja kwa moja, nikawaambia mazingira ya kuona waheshimiwa ni magumu na mtumishi wa Mungu ukitumwa na Mungu unahakikisha umemfikia mhusika,” amesema.
“Nilishawahi kufanya hayo 2014 ikashindikana nilishawahi kufanya hivyo Chadema nikapeleka ujumbe umfikie aliyekuwa mwenyekiti, ile kitu ikawa hivyo na matukio yakawa mabaya kwamba hapa patakuwa na hivi na hivi,” amedai
Kwa mujibu wa mchungaji huyo, hakuona haja ya kukamatwa kwa namna hiyo na kama kuna tatizo wangempigia simu angekwenda kwani usajili wa kanisa ni kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani.
“Nisingekataa kwani mimi siyo mtu mbaya ni mtu mwema na ni mtumishi wa Mungu, natumika kusaidia watu na Serikali kwa ujumla kupitia kipawa changu ambacho Mungu amenipa.
“Niseme ukweli wangekuwa na nia ya kuniua wangeniua na nafikiri hivyo, lakini waliopiga kelele mitandaoni nahisi imenisaidia kidogo,” amesema.
Taarifa za awali
Mwenyekiti wa Mtaa wa FFU, Veronica Guta akizungumzia tukio hilo amesema jana Mei 16, saa mbili asubuhi alipigiwa simu na majirani wakidai mtoto wa balozi ametekwa.
“Nilikuja hadi eneo la tukio nikapata taarifa hizo, juhudi za kumtafuta zinaendelea,” amesema.
Kauli ya mzazi
Gumbo, baba mzazi wa Steven amesema akiwa nyumbani, mwanaye alimpigia simu akamweleza kuna wataalamu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani wanakwenda kukagua kanisa ili kuwapatia cheti cha usajili.
“Hiki cheti tuliomba siku nyingi lakini hatukupewa, nashangaa leo ghafla mwanangu anasema kuna watu wanakuja kukagua kanisa ili watupe cheti, nilimuuliza unawajua akasema ndiyo wamejitambulisha hivyo, nikakubali,” amesema na kuongeza:
“Baada ya muda kweli wakaja watu wawili mwanamke aliyejitambulisha Jackline Lyimo na mwanamume aliyesema anaitwa Ramadhani, wakawa wanakagua kanisa na kupiga picha za video na za mnato, kisha wakaondoka kwa miguu.”
Amesema baada ya watu hao kuondoka yeye aliingia ndani na baada ya saa mbili mwanaye alipanda gari akitaka kuondoka, lakini kabla ya kufika mbali na uwanda wa nyumbani, akazuiwa kwa mbele na gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye rangi nyeupe.
“Majirani wanasema walishuka watu wawili wakawa wanaongea naye taratibu kabla ya kumtoa kwenye gari na kuanza kumburuza, ndipo akaanza kupiga kelele: ‘Natekwaa… natekwaa… jamani natekwa majirani nisaidieni,” amesema.
Gumbo amesema: “Mimi nikiwa ndani nilisikia kelele hizo, nikatoka nikakuta wanamtupia mwanangu kwenye gari kisha wakaondoa gari kwa kasi.”
Amesema alilikimbilia gari hilo bila mafanikio akanyanyua jiwe kulipiga kwa nyuma akapasua kioo, lakini haikusaidia kumnusuru mwanaye.
Gumbo amesema alikwenda Kituo cha Polisi Muriet kutoa taarifa akatakiwa kurudi hapo leo Mei 17, 2025 baada ya saa 24 kupita.
“Polisi walisema nirudi baada ya saa 24 kama hajaonekana nikatoe taarifa upya waanze kazi ya kumtafuta mwanangu, hivyo naomba Serikali inisaidie nimpate mwanangu,” amesema.
Lucy Lucas, muumini wa kanisa hilo amesema akiwa nje anafua aliona gari jeupe likisogelea gari la mchungaji, kisha wakashuka watu wawili wenye miili mikubwa wakazungumza naye taratibu kabla ya kutokea purukushani za hapa na pale.
“Sisi tulivyoona wanakuja, nilijua wana shida na balozi ndio wanamuulizia, lakini ghafla tukaona wanamburuza mchungaji wetu, huku akipiga kelele ndipo tukapiga yowe kuomba msaada lakini lilikuwa tukio la haraka kwani walifanikiwa kuondoka naye.
“Watu wa barabarani wanasema gari lilikuwa mwendo kasi hadi likasababisha ajali iliyomuua dereva bodaboda pale Mbauda. Madereva wengine walinyanyuka kulikimbiza lakini lilipofika Kisongo walinyooshewa bunduki wakaogopa wakarudi,” amedai shuhuda huyo.
Amesema tukio hilo ni la kwanza kutokea katika mtaa huo, akimwelezea mchungaji wao kuwa hana chuki na mtu zaidi ya kutoa maono ya ndoto zake.