Rais Samia ahoji uzalendo wasiotaka kujiandikisha

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wale wasiojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura au wasiotaka kujitokeza kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kujiuliza rohoni mwao uzalendo wao uko wapi.

Uandikisaji na uboreshaji taarifa za wapiga kura unafanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.

Rais Samia ametoa kauli hiyo kipindi ambacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeshaweka msimamo hakishiriki uchaguzi mkuu huo kama hakutakuwa na mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi.

Chadema kwa sasa inaendelea na operesheni ya No Reforms, No Election ‘Bila mabadiliko, Hakuna uchaguzi’ ya mikutano ya hadhara ambayo imeshafanyika kanda ya Nyasa, Kusini, Pwani, Victoria sasa wako Serengeti.

Licha ya Chadema kueleza msimamo huo, INEC ilitangaza Aprili 12, 2025 kwamba chama hicho kwa kushindwa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi, kimepoteza sifa za kushiriki uchaguzi mkuu 2025 na chaguzi zingine ndogo kwa miaka mitano hadi 2030.

“Chadema ambacho hakikusaini kanuni za maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2025, hakitashiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu na chaguzi zote ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano,” alisema Ramadhani Kailima, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC siku ambayo vyama vingine 18 vilisaini.

Leo Jumamosi, Mei 17, 2025, Rais Samia amezungumzia hilo la ushiriki kwenye chaguzi wakati akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua kutoka kwa mkuu huyo wa nchi ni upi wito wake kwa Watanzania kuelekea uchaguzi mkuu.

Rais Samia aliulizwa swali hilo mara tu baada ya kumaliza kuboresha taarifa zake za mpiga kura katika ofisi ya serikali ya Kijiji, Chamwino mkoani Dodoma.

“Kutojitokeza ni kukataa haki yao ya Kikatiba na kuwa mbali na haki ya Kikatiba,  unajiuliza wewe ni mzalendo wa aina gani ambaye Katiba imekupa fursa hii,” amesema.

Amewataka kwenda kujiandikisha na kupiga kura na kisha kuweka kiongozi wanayemuona atakuja kuwahudumia.

“Kwa hiyo wewe unaikataa, ukiikataa wenzio watakwenda kuweka wanayemtaka na unakosa fursa ya kushawishi mwingine kuweka yule mnayemtaka,” amesema.

Amesema mtu huyo anakuwa wa kubabaisha na kulalamika lakini suala kubwa hapo ni uzalendo.

“Jiulize mwenyewe uzalendo wako uko wapi? Ni fursa kubwa inatokea kila baada ya miaka mitano haiji kila siku ni vyema kila Mtanzania ajitokeze kutumia fursa hii,” amesema Rais Samia.

Awali, alitoa sababu za kwa nini ameamua kuboresha taarifa zake akisema mwaka 2020 alishiriki uchaguzi na kupiga kura Zanzibar kipindi hiko akiwa Makamu wa Rais na kwa sasa ni Rais na makao makuu ya nchini yapo Dodoma ndio maana ameamua kuziboresha.

Kipindi hicho mwaka 2020, Rais alikuwa John Magufuli ambaye Machi 17, 2021 alifariki dunia katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo. Baada ya hapo Machi 19, 2021, Samia aliapishwa kuwa Rais.

“Nimeona nijiunge nanyi, kama mnavyojua mimi ni mkazi wa Chamwino na nimepiga kura nyingi huko nyuma lakini kwa mwaka huu ni lazima nipige hapa Chamwino,” amesema.

“Kwa hiyo ndio maana nimekuja kurekebisha taarifa zangu si mpiga kura mpya lakini huko nyuma nilikuwa napiga Zanzibar kwa kuwa nilikuwa makamu wa Rais. Na Rais alikuwa anapiga hapa Dodoma lakini mwaka huu inabidi nipige hapa Dodoma hapa ndio makao makuu ya Serikali,” amesema Rais Samia.

Amewaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao na kuwaeleza ambao hawajafika huo ni zunguko wa pili wakiukosa hakutakuwa na nafasi nyingine.

“Huko mbele hakuna nafasi ya kurudia ili usipoteze haki yako niwaombe mjitokeze kwa wingi, msipoteze nafasi hii ili tupate kupiga kura na kurejesha Serikali inayoleta maendeleo kwa wananchi,” amesema.

Amesema kazi ya uandikishaji inavichangamoto kidogo na kutaka inapojitokeza wawe wastahimilivu na kusubiri pale inapotokea mashine imechoka kadi zimepungua ama kuisha.

Amesema kwa mipango mizuri waliowaliojiwekea kila mwenye haki ya kuandikishwa ataandikishwa.

Amewataka watu kujitokeza kwa wingi ili wawezekupata haki ya kupiga kura kutimiza haki yetu ya kikatriba

Pia amewashukuru maofisa waandikishaji ambao wamekuwa wakifanya kazi ya uandikishaji wapiga kura ambao wanajitokeza kwa kutwa nzima.

Rais Samia aliingia katika kituo hicho saa 8.20 mchana na kutoka saa 8.31 mchana, baada ya kutanguliwa na mwandikishaji mmoja mbele yake.

Ofisa Mwandikishaji wa majimbo ya Chamwino na Mvumi, Godfrey Mnyamale amesema shyghuli hiyo inalenga kuwaandikisha wapiga kura wapya wenye sifa na kuhakiki taarifa za waliojiandikisha, kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa.

“Hadi sasa zoezi linaendelea vizuri halmashauri ina vituo 50, vifaa vyote viko site, waandishi wanaendelea vizuri hakuna changamoto hadi sasa,” amesema.

Amesema wamelenga kuandikisha na kuhakiki taarifa za wapiga kura 280,000 katika Halmashauri ya Chamwino mkoa wa Dodoma.

Naye mkazi wa Chamwino, Salma Ramadhan amesema kwenye kuchukuliwa taarifa, hadi kupata kitambulisho chake ni shughuli ambayo haikuchukua dakika tano.

“Wananchi wajitokeze kwa wingi waje wajiandikishe ili tuweze kupiga kura, waweze kumchagua Rais, mbunge na diwani kwa kuwa hii ni kwa manufaa yetu, jamii ,watu wanaotuzunguka na Taifa kwa ujumla,” amesema.

Ratiba ilivyo

Aprili 14, 2025, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele alitangaza ngwe ya pili ya uboreshaji wa daftari la kudumu la mpigakura kuanzia Mei 1 na kutamatika Julai 4, 2025.

Akitaja mizunguko hiyo itakavyokuwa, Jaji Mwambegele amesema mzunguko wa kwanza utahusisha mikoa 15, kwa wakati mmoja na utafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia Mei Mosi 2025 hadi Mei 7, 2025.

“Vituo vya uandikishaji 3,808 vitatumika, mikoa itakayohusika katika mzunguko wa kwanza ni Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora na Katavi. mingine ni Kigoma, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe,” alisema.

Mzunguko wa awamu ya pili Jaji Mwambegele amesema utahusisha mikoa 16 kwa wakati mmoja na utafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia Mei 16, 2025 hadi Mei 22, 2025 ambapo vituo 3,321 vitatumika.

“Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba,” alisema.

Mzunguko wa tatu katika uboreshaji wa daftari hilo la kudumu la mpigakura, kwa mujibu wa Jaji Mwambegele utahusisha vituo 130 vilivyopo kwenye magereza yaliyopo Tanzania Bara, na vituo 10 vilivyopo kwenye vyuo vya mafunzo Tanzania Zanzibar.

“Shughuli itafanyika kwa wakati mmoja na ni siku saba, kuanzia Juni 28, 2025 hadi Julai 4, 2025,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *