
Berkane. Mashabiki wa Simba nyumbani Tanzania huwaambii kitu kwa winga wao, Ellie Mpanzu Kibisawala kutokana na namna alivyoteka hisia zao tangu alipojiunga na timu hiyo katika dirisha dogo la usajili mwezi Januari.
Hata hivyo, mambo ni tofauti baada ya timu hiyo kuja Morocco kwani mashabiki wengi wa soka hapa licha ya kuifahamu Simba, mchezaji anayejulikana sana hapa wa kikosi cha wawakilishi hao wa Tanzania ni Fabrice Ngoma.
Umaarufu wa Ngoma umechangiwa kwa kiasi kikubwa na nyota huyo kuwahi kuichezea kwa mafanikio makubwa timu ya Raja Casablanca ya hapa kuanzia mwaka mwaka 2019, alipojiunga nayo akitokea AS Vita Club ya DR Congo hadi 2022, alipoachana nayo na kujiunga na Al-Fahaheel SC ya Kuwait.
Akiwa na Raja Casablanca, kiungo huyo alitoa mchango mkubwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2020/2021, na pia taji la CAF Super Cup mwaka 2020.
Katika maeneo mengi yenye mkusanyiko mkubwa wa watu ambayo kikosi cha Simba kilikuwa kinapita, Ngoma amekuwa akiombwa kupiga picha na mashabiki ambao wengi wanaonekana kuwa wa Raja Casablanca.
Baadhi ya mashabiki hao mbali na kupiga picha, wamekuwa wakizungumza zaidi na kiungo huyo ingawa pia wapo ambao wanaonekana kumfahamu vilivyo kocha wao Fadlu Davids.
Ngoma amekuwa mchezaji aliyechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Simba hadi ikaweza kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu ambapo katika mashindano hayo amecheza idadi ya mechi 11.