Siku ya rekodi Simba, yawekewa mzigo

Berkane. Baada ya kusubiri kwa miaka 32, Simba leo inacheza kwa mara nyingine hatua ya fainali ya Kombe la Klabu Afrika kwa kuanzia ugenini dhidi ya RS Berkane ya hapa Morocco katika mechi ya kwanza ya hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane, kuanzia saa 2:00 usiku sawa na saa 4:00 usiku kwa muda wa Tanzania.

Matokeo mazuri katika mchezo wa leo hapana shaka yataiweka Simba katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo ambao utakuwa wa kwanza kwao kwenye mashindano ya klabu Afrika baada ya kukosa taji mwaka 1993, ilipopoteza kwa mabao 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast.

Simba ilitinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu baada ya kuitoa Stellenbosch ya Afrika Kusini kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0 katika mechi mbili baina yao huku RS Berkane ikitinga hatua hiyo kwa kuitupa nje CS Constantine ya Algeria kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1.

Mambo mengi yamebadilika na muda mrefu umepita tangu Simba ilipocheza kwa mara ya mwisho hatua ya fainali ya mashindano ya klabu yanayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika Afrika (CAF) na hilo ndilo linawapa matumaini wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo kuwa safari hii wanaweza kuandika historia ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutwaa ubingwa wa mashindano ya klabu Afrika.

“Kipindi kile wakati tunacheza fainali ya Kombe la CAF, kuna mambo mengi yalitukwamisha lakini kuwa hasa ni kwamba bado soka letu lilikuwa nyuma na hatukuwa na uzoefu mkubwa wa namna mashindano haya yanavyochezwa,” anasema katibu mkuu wa zamani wa Simba, Hassan Hassanoo.

Mpango ni ushindi Morocco

Hatua ya fainali itakuwa na mechi mbili ambapo ya kwanza ni hii inayochezwa leo na nyingine ya marudiano ambayo itachezwa Jumapili, Mei 25 mwaka huu katika Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar.

Hata hivyo, hesabu za Simba ni kumalizia shughuli hukuhuku Morocco kwa kupata ushindi katika mechi ya leo ili isiwe na mzigo na presha kubwa katika mechi ya marudiano ambayo itachezwa nyumbani wiki moja baadaye.

Na hilo linadhihirishwa na maandalizi makubwa ambayo Simba imekuwa ikiyafanya  kuanzia ilipoanza safari Dar es Salaam hadi ilipofika hapa.

Simba imekuja na kundi kubwa la watu ambao idadi yao ni takribani 260 lengo likiwa ni kuhakikisha inakuwa na sapoti kubwa hapa katika dakika 90 za mechi hiyo.

Katika kuhakikisha timu inakuwa katika mazingira salama na kutotoa mwanya kwa wenyeji kuwafanyia hujuma, Simba iliamua kukaa kwa siku mbili katika jiji la Casablanca na baada ya hapo Alhamisi jioni ikasafiri hadi Oujda kwenye mji mdogo wa Saidia ambako itaondokea hapa kwenda Berkane siku ya mchezo.

Simba haikutaka kukaa Berkane kwa vile kabla ya kuja Morocco ilipata taarifa za kijasusi kuwa wenyeji wamekuwa wakitumia mbinu chafu kwa timu ngeni hasa siku ya kuamkia siku ya mchezo.

Lakini ndani ya Uwanja, kocha Fadlu Davids na benchi lake la ufundi wamewaandaa wachezaji wa Simba kuhakikisha kwanza hawaruhusu nyavu zao kutikiswa katika mchezo huo wa kwanza na kisha kufunga mabao kadri nafasi zitakapopatikana na yeye mwenyewe amesisitiza kuwa anataka shughuli imalizikie ugenini.

“Tunahitajika kupata matokeo mazuri katika mechi hii ya kwanza dhidi ya Berkane kwani ndio itatupa mwanga wa nini kitatokea katika mechi yetu ya marudiano nyumbani na sisi kama timu tumejipanga kwa hilo.

“Presha katika hatua kama hizi ni jambo lisilo epukika lakini kwa upande wetu hatuipi nafasi na badala yake akili na mawazo yetu ni katika kutimiza kile kinachohitajika kufanyika ndani ya uwanja,” amesema Davids.

Bilioni moja mezani

Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya uongozi wa Simba kimethibitisha kuwa wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi la Simba watavuna kiasi cha Sh1 bilioni ikiwa watafanikiwa kutwaa taji la mashindano hayo.

Ukiondoa kiasi hicho cha fedha, kuna bonasi ya Sh30 milioni kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kila bao ambalo Simba itafunga katika mchezo wa leo pamoja na ule wa marudiano wiki ijayo.

Kumbukumbu nzuri kwa Simba

Mchezo wa leo utasimamiwa na mwamuzi Pierre Ghislain Atcho kutoka Gabon akisaidiwa na Boris Marlaise Ditsoga (Gabon) na Eric Ayimavo Ayamr Ulrich (Benin) huku refa wa akiba mezani atakuwa Patrice Tanguy Mebiame wa Gabon.

Atcho ana kumbukumbu nzuri na Simba kwani Desemba 19, 2023 ndiye alichezesha mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad AC ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 nyumbani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *