
Arusha. Mchungaji wa Kanisa la Huduma ya Kristo lililopo Mtaa wa FFU, Kata ya Muriet mkoani Arusha, Steven Jacob (35) ametekwa na watu wasiojulikana alipokuwa akitoka nyumbani kwake asubuhi ya Mei 16, 2025, walioshuhudia wasimulia.
Baba mzazi wa Steven, ambaye ni balozi wa nyumba 10 wa CCM pamoja na walioshuhudia tukio hilo, wamesema waliomteka walikuwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser lisilokuwa na namba za usajili.
Inadaiwa mchungaji huyo alikokotwa kwa nguvu, huku akipiga kelele kwamba anatekwa kisha akatupwa kwenye gari lililoondoka eneo hilo kwa kasi.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, gari hilo pia lilimgonga mwendesha bodaboda ambaye hajafahamika na kusababisha kifo chake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia tukio hilo simu yake iliita bil kupokewa na hata ujumbe mfupi wa maneno (sms) aliotumiwa haukujibiwa.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amesema tukio hilo linafanyiwa upelelezi wa kina kujua undani wake na chanzo chake.
“Tumeshaanza uchunguzi wa tukio la kijana kuchukuliwa na hao watu na tayari tuko hatua nzuri, tutawajulisha kitakachoendelea,” amesema Mkude.
Mwenyekiti wa Mtaa wa FFU, Veronica Guta akizungumzia tukio hilo amesema jana Mei 16, saa mbili asubuhi alipigiwa simu na majirani wakidai mtoto wa balozi ametekwa.
“Nilikuja hadi eneo la tukio nikapata taarifa hizo, juhudi za kumtafuta zinaendelea,” amesema.
Kauli ya mzazi
Jacob Gumbo, baba mzazi wa Steven amesema akiwa nyumbani, mwanaye alimpigia simu akamweleza kuna wataalamu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani wanakwenda kukagua kanisa ili kuwapatia cheti cha usajili.
“Hiki cheti tuliomba siku nyingi lakini hatukupewa, nashangaa leo ghafla mwanangu anasema kuna watu wanakuja kukagua kanisa ili watupe cheti, nilimuuliza unawajua akasema ndiyo wamejitambulisha hivyo, nikakubali,” amesema na kuongeza:
“Baada ya muda kweli wakaja watu wawili mwanamke aliyejitambulisha Jackline Lyimo na mwanamume aliyesema anaitwa Ramadhani, wakawa wanakagua kanisa na kupiga picha za video na za mnato, kisha wakaondoka kwa miguu.”
Amesema baada ya watu hao kuondoka yeye aliingia ndani na baada ya saa mbili mwanaye alipanda gari akitaka kuondoka, lakini kabla ya kufika mbali na uwanda wa nyumbani, akazuiwa kwa mbele na gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye rangi nyeupe.
“Majirani wanasema walishuka watu wawili wakawa wanaongea naye taratibu kabla ya kumtoa kwenye gari na kuanza kumburuza, ndipo akaanza kupiga kelele: ‘Natekwaa… natekwaa… jamani natekwa majirani nisaidieni,” amesema.
Gumbo amesema: “Mimi nikiwa ndani nilisikia kelele hizo, nikatoka nikakuta wanamtupia mwanangu kwenye gari kisha wakaondoa gari kwa kasi.”
Amesema alilikimbilia gari hilo bila mafanikio akanyanyua jiwe kulipiga kwa nyuma akapasua kioo, lakini haikusaidia kumnusuru mwanaye.
Gumbo amesema alikwenda Kituo cha Polisi Muriet kutoa taarifa akatakiwa kurudi hapo leo Mei 17, 2025 baada ya saa 24 kupita.
“Polisi walisema nirudi baada ya saa 24 kama hajaonekana nikatoe taarifa upya waanze kazi ya kumtafuta mwanangu, hivyo naomba Serikali inisaidie nimpate mwanangu,” amesema.
Lucy Lucas, muumini wa kanisa hilo amesema akiwa nje anafua aliona gari jeupe likisogelea gari la mchungaji, kisha wakashuka watu wawili wenye miili mikubwa wakazungumza naye taratibu kabla ya kutokea purukushani za hapa na pale.
“Sisi tulivyoona wanakuja, nilijua wana shida na balozi ndio wanamuulizia, lakini ghafla tukaona wanamburuza mchungaji wetu, huku akipiga kelele ndipo tukapiga yowe kuomba msaada lakini lilikuwa tukio la haraka kwani walifanikiwa kuondoka naye.
“Watu wa barabarani wanasema gari lilikuwa mwendo kasi hadi likasababisha ajali iliyomuua dereva bodaboda pale Mbauda. Madereva wengine walinyanyuka kulikimbiza lakini lilipofika Kisongo walinyooshewa bunduki wakaogopa wakarudi,” amedai shuhuda huyo.
Amesema tukio hilo ni la kwanza kutokea katika mtaa huo, akimwelezea mchungaji wao kuwa hana chuki na mtu zaidi ya kutoa maono ya ndoto zake.