Ndani ya Boksi: Tunazalisha kina ‘pateni’ bila misingi

Dar es Salaam. Tumetoka kwenye familia ambazo, nyumba ina korido ndefu kama treni. Kila mtu kapanga ndoo mlangoni kwake. Kulia vyumba tisa, kushoto vyumba nane, na mwenye nyumba anaishi vyumba vya uani.

Mlango wa mbele haufungwi hata siku moja. Kuna watu kazi zao ni kutoka usiku na kurudi usiku. Foleni ya chooni ni ndefu kuliko foleni ya kuingia Uwanja wa Taifa kwenye dabi ya Kariakoo.
Mama Halima ana timu yake, Mama Said na mashoga zake. Nyumba yote wapangaji tupu. Kelele kama sokoni. Vichambo, kila mtu kafungulia muziki anaopenda tena kwa sauti ya juu.

Mpangaji mpya kama alikotoka alikuwa jeuri. Hapa atafuata utaratibu wa makontawa. Lete umbea upewe udaku. Lete kelele upewe mayowe. Lete kichambo upewe shombo.

Jioni kila mtu katoa jiko mlangoni kuonesha ufundi, pika vibaya uwe stori. Kwenye vabaraza vyao nyanyuka wakuseme. Kila uliloongea na mpenzi wako usiku ukiwa ndani. Waja wanalo asubuhi.

Huku kwetu kila siku watu wanaamka vibaya, usijichanganye. Utamiminiwa mitusi na mineno kerefu. Vinywa vyao vinatema shombo kuliko wahuni wa ferry na shimoni Karikaoo.

Kuna ugomvi huo ukiingilia tu, wewe ndo utalala polisi. Huku kwetu ukiwa mstaarabu na mcha Mungu, utaishia kuacha kodi ya miezi mitatu popote pale ulipopanga. Hii ndiyo mitaa yetu tulio wengi.

Hii ndiyo mitaa inayotuzalishia vijana hodari kwenye muziki. Kwenye riadha, ndondi, wachungaji na mashekhie. Hii ndiyo mitaa inayoibua kila aina ya kipaji unachojua. Tulio wengi tunatoka huku kabla ya kuhamia Masaki na Obey.

Hii ndiyo mitaa aliyokulia Marioo. Lulu Diva. Ndiyo mitaa iliyomkuza Zuchu na Jay Melody, Leonardo na wenzao. Utotoni walifanya kila kitu ukubwani ndiyo wakabaki na kimoja tu. 
Wasanii wetu ni kama shule zetu. Primari mpaka fomu foo, utasoma kila kitu. Fomu siksi na kuendelea ndiyo unachagua masomo. Wasanii pia utotoni wafanya kila kitu, ukubwani ndiyo wakachagua kimoja tu. 

Ndiyo maana wengi hawana muongozo wala misingi ya sanaa. ‘Wanajikutaga’ wakikimbiza mjini bila elimu. Sasa ni wajibu wa jamii kwa ujumla wetu. Kulea, kutunza na kuendeleza vipaji vya wasanii wetu. 

Tuna vijana wenye vipaji lakini ni vipaji yatima. Tunaye Paten, hatuna wakili msomi wa Pateni. Tunaye Ibraah bila mwanasheria kwa dili zake. Kimsingi tunafanya vitu kienyeji sana. Na wao wanaifanya kazi kienyeji mno.

Tuwaambie watoto wetu waliopo shule. Kwamba akimuona Drake, ajue nyuma ya Drake kuna rundo la watu wasomi. Wanaoishi kwa sababu yake. Drake kazi yake kuimba tu. Dili zake zingine zinasimamiwa na watu. Tena wasomi.

Kwenye hizi sanaa tunahitaji mawakili wasomi, madaktari wasomi, meneja wasomi na mapromota wasomi. Hii biashara ni zaidi ya jasho la Diamond jukwaani. Nyuma ya Mondi anapaswa kuwa na watu sahihi.

Kijana uliye chuoni sanaa inakuhitaji. Hata yule injinia ama mchora ramani. Anahitajika kwenye ‘apatmentsi’ za Jux na mashamba ya Profesa Jay. Muziki siyo lazima wote tuimbe, alituambia hili Afande Sele. 

Unaweza kuwa mpenzi mkubwa wa muziki. Unaweza kuhusudu sanaa ya uigizaji kama Gabo. Lakini huwezi kuwa na uwezo kama wa Gabo. Hiyo haina maana uachane na sanaa hiyo, soma sana uje kuwa dokta wake.

Soma sana uje kuwa meneja wa Ben Pol. Komaa skonga uje kuwa mmoja wa meneja wa Zuchu au Meja Kunta. Usomi wako unaweza kukusogeza karibu na sanaa kuliko kulazimisha kufanya sanaa. Sanaa inahitaji wenye elimu.

Wasomi wenye mapenzi na sanaa ni vyema kuzama kwenye sanaa. Kuja kuweka misingi mizuri ili tuweze ‘kuishepu’ sanaa yetu. Kwa kusimamia vizuri kazi za sanaa. Kusimamia vizuri ni kuingiza elimu kubwa mliyopata.

Kila siku wanaibuka wasanii wapya. Siwaoni mameneja na mapromota wapya. Wadau wa muziki ni wale wale toka enzi za Mr Paul na Terrence hadi wakati wa Jux na Ben Pol. Hatumuoni Big Joe mpya wala Dj Jd wa kizazi hiki.

Kimsingi ni kwamba. Watu kama kina Diamond tuwape heshima yao. Wapo hapo kwa kutegemea walichojifunza wakiwa Yemen ya Tandale. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *