
Arusha. Mahakama ya Rufani imetengua adhabu ya kifo waliyokuwa wamehukumiwa watu watatu waliokuwa wamekutwa na hatia katika kesi tofauti za mauaji.
Aidha, katika kesi nyingine mbili, Mahakama hiyo imebatilisha mwenendo, kufuta hukumu na kuamuru kesi hizo zisikilizwe upya na Mahakama Kuu kutokana na dosari mbalimbali za kisheria zilizojitokeza.
Hukumu hizo tano zilitolewa jana Ijumaa Mei 16, 2025 na jopo la majaji watatu –Stella Mugasha, Lucia Kairo na Mustafa Ismail, katika vikao vya Mahakama hiyo vilivyoketi Kigoma.
Katika hukumu hizo ambazo nakala zake zinapatikana katika mtandao wa Mahakama, majaji hao wamesema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, kupitia mwenendo na hukumu zilizokuwa zimetolewa, walijiridhisha kesi hizo hazikuthibitishwa pasipo kuacha shaka.
Walioachiwa katika kesi hizo ni Lucas Charles, Emmanuel Charles na Abel Andrew.
Kesi ya kwanza
Katika rufaa ya jinai namba 631/2023 Lucas na Emmanuel Charles, walihukumiwa adhabu ya kifo baada ya kukutwa na hatia ya kumuua Yamungu, katika tarehe isiyojulikana Februari 2020, tukio lililotokea katika Kijiji cha Ruchungi, Uvinza mkoani Kigoma.
Mwili wa Yamungu ulikutwa unaelea kwenye mto huku ukiwa na majeraha sehemu kadhaa za mwili wake na sehemu za siri zikiwa zimenyofolewa.
Warufani hao walikamatwa Machi 20, 2022 na kufikishwa Kituo cha Polisi Uvinza na kwa mujibu wa ushahidi walipaondika maelezo ya onyo walikiri kumuua mtu huyo lakini wakati wa utetezi walieleza kuwa waliteswa na kulazimishwa kutoa maelezo ya kukiri kosa, ambayo ndiyo yalitumika kuwatia hatiani.
Katika sababu zao za rufaa walikuwa wakiikosoa Mahakama Kuu iliyowahukumu, kuwa ilitegemea ushahidi dhaifu usiotosha kuwatia hatiani, maelezo ya onyo yalichukuliwa kinyume cha sheria kwa kuwa yalirekodiwa zaidi ya saa nne.
Majaji hao baada ya kusikiliza sababu za rufaa na kupitia mwenendo wa rufaa hiyo, walifuta kwenye kumbukumbu za Mahakama maelezo ya onyo ya warufani hao kwa kurekodiwa kinyume na sheria.
Jaji Mugasha amesema Mahakama inawaachia huru baada ya kujiridhisha upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi dhidi yao.
Kesi ya pili
Katika rufaa ya jinai namba 623/2023, majaji hao pia walimuachia huru Abel, aliyekuwa amekutwa na hatia ya kumuua Joseline Leonard wa Kijiji cha Nyakasanda wilayani Kibondo mkoani Kigoma, Juni 22, 2022.
Siku ya tukio majira ya usiku, Joseline (marehemu kwa sasa), alikuwa njiani akienda dukani kununua mboga, ndipo ilidaiwa Abel alimshambulia kwa fimbo.
Kutokana na kelele ya kuomba msaada, waliojitokeza walieleza kumkuta ameshafariki huku Abel akikimbia, akiwa ameshikia panga na fimbo ya mianzi.
Ilielezwa kuwa baada ya Abel kukamatwa aliwaongoza polisi hadi nyumbani kwake na kutoa vielelezo hivyo na kukiri kutenda kosa hilo alipokuwa akihojiwa.
Abel alikana madai ya upande wa mashtaka na kuiambia Mahakama kuwa, alipigwa na polisi na kulazimishwa kusaini taarifa hiyo ya onyo, hivyo hakukiri kosa hilo.
Katika rufaa hiyo alikuwa na sababu sita za rufaa, ikiwemo kesi kutothibitishwa bila kuacha shaka na mahakama hiyo ya rufaa baada ya kupitia hoja za pande zote na kumbukumbu za rufaa hiyo, ilibaini hakuna shahidi wa mashtaka aliyeshuhudia Abel akimuua Joseline.
Jaji Mugasha amesema Mahakama imebatilisha hukumu na kuamuru Abel aachiwe baada ya kufuta maelezo ya ungamo na kukubaliana na sababu nyingine, ikiwemo kosa kutothibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa.
Kesi kusikilizwa upya
Wakati hao watatu wakiachiwa huru, Mahakama hiyo imeamuru warufani wengine wawili waliokuwa wamekutwa na hatia za mauaji na kuhukumiwa adhabu hiyo ya kifo, zisikilizwe upya.
Katika rufaa ya jinai namba 171/2022, iliyofunguliwa na Kinyota dhidi ya Jamhuri baada ya kukutwa na hatia ya kumuua Lucia Tekana, katika Kijiji cha Muzye wilayani Kasulu mkoani Kigoma, Mahakama hiyo imebatilisha mwenendo wa kesi iliyosikiliza kuanzia Februari 15, 2022 na kumtia hatiani.
Jaji Kairo amesema Mahakama imebatilisha kuanzia upande wa mashtaka ulipofungua kesi yao na uamuzi uliotolewa, kufuta hukumu ya mrufani kutokana na dosari za kisheria ikiwemo aina ya kosa na kesi kukaa muda mrefu.
Mahakama hiyo imeamuru kuharakishwa upya usikilizwaji wa kesi hiyo ndani ya kipindi cha miezi sita kuanzia tarehe ya hukumu hiyo, mbele ya jaji mwingine kwa mujibu wa sheria.
Jaji Kairo amesema Mahakama Kuu inaagizwa kuzingatia utaratibu uliowekwa katika kushughulikia utetezi wa ukichaa inapotokea unaibuliwa na wakati huohuo, mrufani atasalia kizuizini akisubiri kusikilizwa upya.
Awali wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, ilidaiwa kuwa mrufani alikiri kuua bila kukusudia, tukio lililotokea Septemba 15, 2013.
Wakati wa Usikilizaji, wakili wake alionyesha nia ya kuwa na utetezi wa wendawazimu katika kosa hilo.
Kutokana na sababu hiyo, mahakama hiyo Aprili 22, 2014 iliamuru chini ya kifungu cha 220 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), mrufani apelekwe hospitali ya magonjwa ya akili kwa ajili ya uchunguzi ambapo ripoti ilionyesha kuwa alikuwa hana tatizo lolote wakati anatenda kosa hilo la mauaji.
Juni 5, 2017 mahakama hiyo ilimkuta mrufani na hatia ya mauaji na kumhukumu kifo kwa kunyongwa.
Baada ya kukata rufaa, Mahakama ya Rufani ilibatilisha hukumuna mwenendo wa shauri na kuamuru kesi irudiwe na jaji huyo ambaye Aprili 27,2021 alimkuta na hatia.
Kwenye rufaa yake alikuwa na sababu tatu ikiwemo kupinga utimamu wa kiakili wa mrufani wakati akitenda kosa hilo na kupinga matokeo ya uchunguzi huo , akisema baadhi ya hatua hazikufuatwa kama sheria inavyotaka, ikiwemo utetezi kutopewa nafasi ya kuongoza ushahidi kuthibitisha uwezekano wa mrufani kuwa na uwendawazimu.
Katika hukumu nyingine, jopo la majaji hao lilibatilisha hukumu ya kifo aliyokuwa amehukumiwa Alimu, aliyekuwa amekutwa na hatia ya kumuua mpwa wake, Edgar Godian (3).
Mauaji hayo yalitokea Mei mosi 2021 katika Kijiji cha Heri Juu, Kasulu mkoani Kigoma, kwa kumkata na panga alipomuita chumbani na wenzake ili akawape asali.
Ilielezwa kuwa baada ya tukio hilo, Alimu alitoka nje akaanza kukimbia akiwa na panga hilo lililokuwa na damu na aliposhtakiwa mahakamani alikana kosa hilo akijitetea kuwa na tatizo la afya ya akili, suala ambalo liliungwa mkono na mjomba wake na kaka yake (mashahidi wa utetezi).
Jaji Ismail amesema Mahakama Kuu iliyosikiliza kesi hiyo iliacha vipengele muhimu vya utaratibu wa kushughulikia kesi ya wazimu, hivyo ukiukwaji huo haukubatilisha mwenendo tu bali hata hukumu iliyotolewa.
Jaji Ismail alihitimisha kuwa wanaruhusu rufaa hiyo kwa kufuta hatia na kuweka kando hukumu na kuamuru mwenendo huo upelekwe kwa Jaji mwingine na utaratibu wa usikilizwaji wa kesi za wazimu ufuatwe.