
Dar es Salaam. Urushaji wa matangazo ya redio ulianza kwenye miaka ya 1920 katika nchi ya Marekani, vituo vya redio mapema vikagundua kuwa muziki ni kivutio kikubwa cha usikilizaji wa redio. Wakati huohuo wenye kampuni za kutengeneza santuri nao wakagundua kuwa santuri zilizopigwa katika vituo vya redio mauzo yake yaliongezeka.
Kampuni ya muziki iliyoitwa Victor Records ilikuwa kampuni ya kwanza kusukuma redio zipige santuri zao. Katika miaka hiyo hiyo kukazaliwa kitu kilichoitwa Payola.
Mwaka 1943, kampuni ya Capitor records ya Marekani ikaja na mpango kazi wake;
i. Ikawa kila ikitoa santuri mpya inatengeneza santuri maalumu zenye jina la DJ wa redio na kuzisambaza maDJ maarufu wa kila redio
ii. Pia ikaanzisha utaratibu za kusambaza santuri za bure kwenye kila kituo cha redio.
iii. Na taratibu ukaanzisha utaratibu wa kuwalipa MaDj wa radio ili nyimbo zipigwe hewani. Utaratibu huu ukapewa jina la Payola. Ikiwa na maana ya Pay as you play (lipa nyimbo ipigwe).
Muda si mrefu, MaDj wakawa ndio washika funguo za biashara ya mauzo ya muziki.
Urafiki wa kampuni za muziki na Madj wa radio ulikuwa mkubwa sana, kufikia miaka ya 1950 na swala la Payola lilikuwa linatambulika wazi wazi. Ma Dj maarufu walifikia kulipwa mpaka dola 50 kwa wiki kwa kila wimbo waliousimamia.
Hali ilikuwa mbaya kwa tasnia ya muziki kwa ujumla, ikalazimika Bunge la Marekani liingilie kati, Ma Dj wawili maarufu wakajikuta wakihojiwa mbele ya kamati ya Bunge na Dj maarufu Alan Freed akakutwa na kosa la kupokea Payola, hili likamfanya apoteze kazi yake na hakuna kituo cha redio kilichotaka kumuajiri tena. Mwaka 1960 Payola ilipigwa marufuku rasmi nchini Marekani.
Hapa kwetu kituo cha kwanza cha redio kilianza mwaka 1951 kikaitwa Dar es Salaam Radio na masafa yake yalikuwa yakisikika Dar es Salaam tu, na pia kwa enzi zile za ukoloni matangazo yote yalikuwa ya Kiingereza na kulikuwa na saa moja tu ya matangazo ya Kiswahili kwa wiki. Mwaka 1954 ikazaliwa TBC (Tanganyika Broadcasting).
Zama hizo hakukuwa na kampuni ya kutengeneza santuri, wanamuziki hawakuwa wakifanya muziki kama biashara, hivyo nyimbo zao kupigwa redioni ilikuwa ni jambo la fahari tu.
Wanamuziki wachache walioweza kuvuka na kwenda Kenya au kuwa na mahusiano na kampuni za rekodi za Kenya waliweza kutoa santuri, lakini hiyo nayo ilikuwa ni biashara ya kampuni za muziki za Kenya.
Ujio wa Wakongo mwanzoni mwa miaka ya 60 ndio uliokuja kubadili mtazamo wa wanamuziki kuwa muziki ni kazi. Lakini kwa kuwa hakukuwa na lebo wala kampuni iliyokuwa ikifanya biashara ya muziki, mapato ya wanamuziki yalitokana na viingilio kwenye maonyesho yao.
Hivyo nyimbo kupigwa redioni lilikuwa jambo la muhimu ili watu kuijua bendi, ili kuhamasisha nyimbo kupigwa redioni Payola ikaingia nchini mwetu. Baadhi ya watangazaji walilipwa fedha, wengine walihakikishiwa pombe na usafiri wakizitembelea bendi na hata bendi za mikoani zilikuwa zikiwazawadia watangazaji wengine hata magunia ya mahindi na mchele katika jitihada za kutafuta nafasi nyimbo zao zipigwe radioni.
Miaka ya 1980, biashara ya kanda za kaseti ikaanza, nayo ikachukua mkondo uleule uliofanywa na makampuni ya santuri ya Kimarekani, payola ikaanza kulipwa ili kusaidia mauzo ya kaseti.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, redio binafsi zilianza na katika kipindi hichohicho biashara ya kuuza CD na kaseti za nyimbo za vikundi vya hapa nyumbani ikashamiri zaidi, redio zilitumika sana kufanya promosheni ya nyimbo, Ma DJ wakachukua nafasi yao ya kuwa washika funguo wa tasnia.
Payola ikawashamiri, zililipwa fedha, vocha za simu, kwa wanamuziki wa kike waliotaka kazi zao zisikike walijikuta nao wakilipa payola ya mwili kwa watangazaji wa kiume. Watangazaji wengine wakawa mameneja wa wasanii, redio nyingine zikawa pia na lebo za muziki.
Wakati huohuo sheria ya Hakimiliki ilikuwa bado haijafanyiwa marekibisho, basi ikawa mwenye nguvu ya fedha ndiye anafanikiwa zaidi. Ujio wa TV nao ukaendeleza taratibu hizo za payola, na utaratibu huu ulikuwa kwa vyombo vyote vya utangazaji bila kujali itikadi za kituo vya utangazaji.
Kama unavyojulikana ule msemo, ‘Rushwa ni adui wa haki’, Watanzania wamenyimwa haki ya kusikiliza maelfu ya nyimbo nzuri kutokana na payola ambayo hakika bado inaendelea kwa chinichini mpaka leo hii.