Msaga Sumu apata ajali, alazwa MOI kwa matibabu

Dar es Salaam. Msanii wa muziki wa Singeli, Msaga Sumu, amenusurika kifo katika ajali ya gari iliyotokea jana Mei 16, 2025, akiwa njiani kurejea Dar es Salaam akitokea Wilayani Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma alikokuwa amekwenda kutumbuiza kwenye mkesha wa Mwenge wa Uhuru.

Taarifa za awali kuhusu ajali hiyo zilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Ngollo Malenya, ambaye amesema ajali ilitokea katika Kijiji cha Azimio, Kata ya Mtina, Wilaya ya Tunduru, baada ya gari walilokuwa wakisafiria Msaga Sumu na meneja wake kugongana na kitu wakati wakimkwepa bodaboda aliyekatiza ghafla barabarani.

“Msaga Sumu alikuja Wilaya ya Namtumbo Mei 15, 2025 kutumbuiza usiku wa mwenge. Mei 16 asubuhi alianza safari ya kurudi Dar es Salaam kupitia Tunduru, ndipo ajali ilipotokea,” amesema Malenya.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Msaga Sumu alijeruhiwa kwenye paji la uso na kupata maumivu kwenye mbavu, hali iliyosababisha asafirishwe kwa gari la wagonjwa hadi Hospitali ya Taifa ya MOI kwa uchunguzi na matibabu zaidi.

Meneja wa Msaga Sumu, Khalid Khalid, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa alikuwa ndani ya gari moja na msanii huyo wakati tukio lilipotokea.

“Ni kweli tumepata ajali. Bodaboda alikatiza mbele yetu, dereva alipomkwepa gari likaparamia kitu na kupinduka mara tatu. Nimeumia mkononi na mbavuni kidogo, lakini Msaga ameumia zaidi usoni, ingawa kwa sasa anaendelea vizuri,” amesema Khalid katika mahojiano na Mwananchi.

Amesema hali ya Msaga Sumu imeimarika ukilinganisha na siku ya kwanza walipomtoa Tunduru kumleta Dar es Salaam.

“Tupo MOI, madaktari wanaendelea kumfanyia uchunguzi wa kina, lakini anaongea na anaonekana kuwa na nafuu ukilinganisha na jana,” ameongeza meneja huyo.

Msanii huyo anatarajiwa kuendelea na matibabu hadi atakapopata nafuu kamili, huku mashabiki wake wakimtakia uponaji wa haraka kupitia mitandao ya kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *