
Arusha.Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Musoma, imewahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Thobias Mwita na Daniel Mrimi, baada ya kuwakuta na hatia ya kumuua Marwa Wambura.
Awali Februari 22, 2022 mahakama hiyo iliwahukumu washitakiwa hao adhabu hiyo ya kufa baada ya kuwakuta na hatiani kwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Baada ya kutoridhika na hukumu huyo,Thobias na Daniel walikata rufaa Mahakama ya Rufani, kutokana na dosari za kisheria zilizokuwa zimejitokeza katika hukumu hiyo.
Nakala ya hukumu hiyo iliyopo kwenye mtandao wa mahakama, inaonyesha kuwa Mahakama ya Rufani baada ya kuchunguza kwa makini hukumu ya mahakama hiyo ilibainisha suala la kisheria juu ya amri ya kutiwa hatiani kwa washtakiwa ikiwa walihukumiwa ipasavyo.
Mahakama hiyo ya juu ilieleza kuwa kuhusu uhalali wa kuhukumiwa washtakiwa,mahakama ilibaini baada ya kuzingatia ushahidi wa pande zote mbili, iliridhika kuwa Wambua alifariki kifo kisicho cha kawaida na ilikwenda mbali zaidi kuangalia kama upande wa mashtaka ulithibitisha shtaka dhidi ya warufani.
Ilieleza kuwa katika ukurasa wa 89 wa kumbukumbu za rufaa inaonyesha mahakama iliyotoa hukumu Jaji alitoa hukumu dhidi ya mshtakiwa mmoja aliyetajwa kwa jina la Chacha Kawa (Mwita) jina ambalo halijaonekana sehemu nyingine kwenye kumbukumbu za rufaa na Jaji huyo kuwasomea wote wawili adhabu ya kifo bila kuwataja majina yao.
Mahakama ya Rufani ilieleza kuwa Mahakama hiyo ilimhukumu kila mshtakiwa bila kuwataja majina na kuamuru kwa kutumia mamlaka yao ya marekebisho chini ya kifungu cha 4 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, kubatilisha na kutengua hukumu ya Mahakama Kuu dhidi ya warufani hao.
Mahakama hiyo ilirejesha jalada la kesi hiyo Mahakama hiyo na kumuelekeza Jaji kuandika upya hukumu hiyo na kuondoa dosari hizo za kisheria zilizokuwa zimejitokeza awali kwa kuwahukumu washtakiwa bila kuwataja majina yao.
Mahakama hiyo ya juu iliamuru wakati huo warufani hao watasalia kizuizini kusubiri upya hukumu dhidi yao.
Hukumu mpya
Jaji Frank Mahimbali aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alitoa hukumu hiyo kwa mara ya pili Mei 13, 2025.
Jaji huyo alieleza kuwa hukumu hiii ameitoa kwa kufuata maagizo hayo ya Mahakama ya Rufani yaliyotolewa Machi 14, 2025.
Amesema kama kulivyoonyeshwa na Mahakama ya Rufani, kulikuwa na bahati mbaya ya kuchanganya majina katika hukumu hiyo kati ya washtakiwa waliotajwa kwenye maelezo ambapo badala ya kuwa na majina ya Thobias na Daniel kulikuwa na jina la Chacha Kawa (Mwita).
“ Kwanza, naomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kwa warufani na Mahakama yenyewe ya Rufani na pili, nashukuru Mahakama ya Rufani kwa kuchanganua kwa makini hukumu hiyo na makosa yaliyojitokeza ,”ameeleza Jaji.
Alieleza kuwa makosa hayo hayakufanywa kwa makusudi na kurekebisha dosari hiyo katika hukumu hiyo mpya.
Msingi wa kesi
Katika kesi ya msingi Thobias na Daniel walishtakiwa mahakamani hapo kwa kosa la mauaji walilodaiwa kutenda Januari 8, 2021 katika kijiji cha Sokoni wilayani Tarime mkoani Mara.
Katika kuthibitisha kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watatu ambao ni Massana Wambura (PW1), Baraka Wambura (PW2) na G.5081 Cyril pamoja na kuwasilisha vielelezo vitatu.
PW1 ambaye ni ndugu wa marehemu aliieleza mahakama siku ya tukio,walikuwa pamoja na marehemu wakinywa bia kwenye baa iliyoitwa Kehongo na wakiwa njiani walikutana na Daniel na Thomas katika baa hiyo,kisha kukutana nao tena njiani.
Amesema wakiwa njiani ghafla Daniel alimkaba ndugu yake (marehemu) shingoni na Thobias akamchoma kisu alichokuwa amekishika.
Alieleza mahakama kuwa katika harakati za kumuokoa ndugu yake, Daniel alimchoma yeye kisu cha kichwani na kwneye shingo, akaanguka chini,kisha wakamuibia fedha za Kenya Sh4,800 na kumuacha hapo ambapo aliokuwa msaada hadi akapoteza fahamu.
Aliieleza mahakama kuwa alipata fahamu akiwa kwenye gari la Polisi akielekea Hospitali ya wilaya ya Tarime ambapo alilazwa na kutibiwa ila ndugu yake alishafariki.
Mahakamani hapo PW1 alieleza kusimulia polisi namna tukio hilo lilivyotokea na namna aliwatambua watuhumiwa hao ambao ni majirani zao na kuwa siku ya tukio walikutana kwenye baa hiyo ambapo Daniel aliomba kununuliwa soda.
PW2 ambaye pia ni ndugu wa marehemu alieleza siku ya tukio akiwa na ndugu wengine walienda hospitali kumuona PW1 huku Massana akiwa ameshafariki na alielezwa na PW1 kuhusu wavamizi ambao aliwataka ni Thobias na Daniel ambaye yeye pia anawafahamu.
PW3 alieleza mahakama kuwa alimhoji PW1 na kuandika maelezo yake namna yeye na kaka yake walivyovamiwa na kujeruhiwa na watuhumiwa hao na akiwa kama mpelelezi wa kesi hiyo alishuhudia namna alivyopanga uchunguzi wa mwili wa marehemu.
Alieleza kuwafahamu mashahidi wengine ambao maelezo yao yalirekodiwa ajkiwemo Happiness Isaya ambaye alikuwa mhudumu wa baa hiyo ila alishindwa kwenda kutoa ushahidi katika kesi hiyo kutokana na na kuhama eneo hilo.
Katika utetezi wao washtakiwa wote walikana kosa dhidi yao ambapo wakati wa kujitetea, Thobias alikiri kukamatwa nyumbani kwake lakini hakujua kuhusu tukio hilo na kwamba hakuhusika na chochote.
Daniel naye alijitetea kuwa alikamatwa na wanaodaiwa kuwa ndugu wa marehemu wakimtuhumu kumuua ndugu yao,tuhuma ambazo alizikanusha.
Uamuzi Jaji
Jaji katika hukumu yake ameeleza kuwa hakuna ubishi kuwa marehemu alikufa kifo kisischo cha kawaida na uchunguzi wa mwili huo ulibainisha kukutwa kwa jeraha upande wa kushoto wa kifua na chanzo cha kifo kilikuwa ni kutoka damu nyingi.
Jaji amesema suala la kuzingatiwa ni iwapo ushahidi wa upande wa mashtaka umethibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka yoyote na kuwa ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo.
Jaji amesema kwa kuzingatia mashahidi wa mashtaka,shahidi pekee ni PW1 katika kesi hiyo ambaye aliieleza mahakama namna washtakiwa hao walivyomshambulia marehemu kisha kumshambulia yeye.
Amesema licha ya tukio hilo kutokea usiku,taa zilizomulika eneo hilo zilimuwezesha kuwatambua watuhumiwa hao.
Jaji amesema ameridhika bila shaka yoyote kwamba PW1 aliwatambua wahalifu eneo la tukio na iliweza kuthibitishwa na PW3 kupitia kielelezo (maelezo ya mhudumu wa baa) na kuhitimisha kuwa watuhumiwa walitambuliwa vizuri eneo la tukio.
“Katika uchambuzi wangu wa mwisho wa ushahidi wote wa mwendesha mashitaka kama nani wanahusika na mauaji hayo, kwa mujibu wa ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu, naona washtakiwa wote wawili wanahusika. Ingawa washtakiwa walitetea utetezi wa alibi, lakini ushahidi wa PW1 una nguvu zaidi,”
Jaji Mahimbali alihitimisha kwa kueleza kuwa ushahidi wa mashtaka umethibitisa kosa hilo na Mahakama hiyo inawatia hatiani watuhumiwa wote wawili na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.