Ulega aagiza uchunguzi mshauri mradi wa BRT

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametangaza mpango wa kuitisha uchunguzi dhidi ya mshauri elekezi wa mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya nne – LOT 4(1), unaohusisha kipande cha barabara cha Posta hadi Daraja la Kijazi (kilometa 13.5), kufuatia ucheleweshaji wa utekelezaji na uchimbaji usio na mpangilio unaoendelea katika maeneo mbalimbali.

Ulega amesema ingekuwa busara kwa mkandarasi M/S Geo Engineering kuanza ujenzi katika maeneo tayari yaliyochimbwa badala ya kuendelea na uchimbaji katika maeneo mengine, hatua ambayo imeongeza usumbufu kwa wananchi.

“Kutokana na uchimbaji usio na mpangilio unaofanywa na wakandarasi, wananchi wanateseka na kuzungukwa na tope huku wakikumbana na foleni za magari hali ambayo ingeweza kuepukika,” amesema Ulega.

Kauli hiyo ameitoa leo, Mei 16, 2025, baada ya kufanya ziara ya ukaguzi katika barabara hiyo, amesema haridhishwi na kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

“Wanachimba kila mahali lakini hawakamilishi Wanachimba halafu wanaondoka, Hatuwezi kuendelea hivi, tutabadilisha wote wanaosimamia mradi huu, huyu (mshauri elekezi) nitamchunguza na nikigundua hashughuliki ipasavyo, namwondoa,” amesema Waziri Ulega.

Waziri huyo amesema mkandarasi alipaswa kukamilisha eneo moja kabla ya kuhamia eneo lingine badala ya kugeuza kazi hiyo kuwa kero kwa wananchi.

Amesema kutokana na mkataba wa mkandarasi huyo kufikia ukomo huku kazi ikiwa nje ya makubaliano, Serikali imechukua hatua ya kudai fidia.

“Nilikuwa kwenye hatua mbili, kwanza nimeshawaagiza wakandarasi wote waliochelewesha miradi yetu walipe fidia, pili, nilikuwa na ruhusa ya kuwanyang’anya baadhi ya maeneo.

“Sasa, huyu mshauri tayari ameshaonyesha udhaifu, nataka kujua ni nani waliomruhusu mkandarasi aendelee kuchimba kila mahali,” amesema.

Ulega amesisitiza kuwa hata kama wakandarasi hao wanakimbizana na muda wa mkataba, hawakupaswa kuchimba kila sehemu kiholela, kwani uamuzi wa kuongeza muda wa mkataba ni wa Serikali pekee.

Msimamizi wa Mradi huo, Rajab Idd ameomba radhi kwa niaba ya timu yake kutokana na kuchelewa kwa mradi huo. Amesema juhudi zinaendelea kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Ameeleza kuwa sababu kuu ya uchimbaji katika maeneo mengi ni maandalizi ya ujenzi wa vituo vya mabasi, ambavyo vinachukua muda mrefu zaidi kuliko barabara.

“Tuna jumla ya vituo 18 vya mabasi tunavyopaswa kujenga, baadhi tumekamilisha na imebaki tu kuweka vyuma. Vituo vilivyobaki ni pamoja na vya Aga Khan na Daraja la Selander.

“Tulianza na vituo tukiamini Serikali itatupatia pongezi, lakini hali imekuwa tofauti. Tunaomba radhi,” amesema.

Mmoja wa madereva wanaotumia barabara hiyo Samson Peter amesema kumekuwa na changamoto ya foleni kutokana na barabara kuwa finyu.

“Shimo ambalo limechimbwa katikati ya barabara imesababisha barabara kuwa finyu nah ii imeleta changamoto ya foleni, ujenzi unapaswa kufanyika hapa kwa saa 24 ili kutofanya kero kudumu kwa muda mrefu,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *