Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameitaka Serikali kuandaa ajenda ya kitaifa ya kuendeleza viwanda, wakieleza kuwa kukosekana kwa mpango wa pamoja na endelevu kumesababisha kila utawala kuwa na mkakati wake binafsi, hali inayodhoofisha maendeleo ya sekta hiyo muhimu kwa utoaji wa ajira na ukuaji wa uchumi.
Pia, Wawakilishi wameitaka Serikali kuweka mipango madhubuti ya kutafuta masoko ya bidhaa za Zanzibar nje ya nchi, wakieleza kuwa kwa sasa visiwa hivyo vinaingiza bidhaa nyingi kuliko inavyouza nje, hali inayokwamisha ukuaji wa uchumi.
Wawakilishi hao wamesema hatua hiyo ni muhimu ili kuimarisha sekta ya biashara na kukuza uzalishaji wa ndani, badala ya kuendelea kutegemea bidhaa kutoka nje ambazo zinadhoofisha pato la taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo, Mei 16, 2025, wakati wa mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, katika mkutano wa 19 wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea Chukwani.
Awali, Waziri mwenye dhamana, Omar Said Shaaban aliomba baraza hilo lijadili na kuhidhinisha Sh57.55 bilioni kutekeleza vipaumbele katika sekta tatu.

Mwakilishi wa Kojani, Hassan Hamad Omar (ACT Wazalendo), akizungumza wakati wa kuchangia makadirio ya mapato na matumizi ya hotuba ya Wizara ya Viwanda na Biashara Barazani Chukwani Zanzibar
Akichangia bajeti hiyo, Mwakilishi wa Ziwani, Suleiman Makame Ali (CCM), amesema zamani kulikuwa na viwanda vingi Zanzibar, lakini kwa sasa havipo na changamoto kubwa kila mmoja anakuwa mipango yake na kushindwa kuendelezwa.
Hata hivyo, amepongeza jitihada ambazo anachukua Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kufufua viwanda hivyo lakini akasema nguvu hiyo inapaswa kuungwa mkono na ajenda ya kitaifa.
Ametolea mfano wa baadhi ya viwanda vilivyokuwapo zamani kisiwani hapo lakini kwasasa havipo tena ni pamoja na viwanda vya maziwa, viatu, sigara, soda, mifugo na masufuria.
“Umefika wakati sasa lazima tuwe na mpango au ajenda maalumu ya kuandaa viwanda, sote tunajua hapa Zanzibar tulikuwa na viwanda vingi lakini havipo tena, hii ni kwasababu kila mmoja anayekuja anakuwa na ajenda yake, hatuwezi kufika tunapotaka kufika,” amesema Suleiman.
Amesema wakati Serikali ikitaka kuwatafutia watu ajira nje ya nchi, ni bora ikajikita zaidi kwenye kujenga na kuboresha viwanda na ajira hizo zitapatikana ndani badala ya kwenda nje ya nchi.
“Tunashindwa vipi kuendeleza viwanda na hizi ajira tunazosema kwenda kutafuta nje zikapatikana humu humu ndani?” amehoji.
Mwakilishi wa Kojani, Hassan Hamad Omar (ACT Wazalendo) amesema kulikuwa na ujenzi wa viwanda Pemba, lakini kimoja cha mabati kimesimama bila kujua sababu ni kitu gani na kiwanda cha kusarifu (kuchakata) mwani licha ya kukamilika lakini kimeshindwa kuanza kufanya kazi.
“Tunazungumza viwanda kwa sababu tunajua ndio vinatoa ajira nyingi, sasa kama vinakwama hizi ajira zitatoka wapi, wananchi wana hamu ya kufahamu,” amesema.
Mwakilishi wa Mtoni, Hussein Ibrahim Makungu (CCM), amesema Serikali haiwezi kuajiri watu wote hivyo ni jukumu lake kuboresha mazingira na kuweka miundombinu mizuri katika sekta ya biashara ambayo itaajiri wengi.
Pamoja na kuongeza wigo mpana wa viwanda, Makungu ameshauri mpango huo uende sambamba na kutafuta masoko nje ya nchi ili bidhaa zinazozalishwa ziondoke haraka kwani mahitaji ni makubwa.
Makungu pia amezungumzia kuhusu gharama za kuingiza bidhaa kati ya Tanganyika na Zanzibar kwamba bado ni changamoto mbayo inaendelea kuwatesa siyo wafanyabiashara bali hata wananchi wa kawaida.
Ametaka wizara zinazohusika kushirikiana kuweka utaratibu maalumu au hata kubandika bango linaloonyesha gharama za usafirishaji mzigo bandarini ambao sio wa biashara kwani kuna kodi zinatozwa kwa wananchi lakini hazipaswi kutozwa kiasi kinachotozwa hivi sasa.
“Mtu amenunua zawadi labda ya televisheni au friji anampelekea ndugu yake au hata ana mke wake yupo Tanganyiki, lakini tozo zinakuwa kubwa haijulikani ni shilingi ngapi inatakiwa kutozwa kwa kitu gani, kwahiyo hili lianagaliwe na kama inawezekaan tuwek maabngo bandarini,” amesema Makungu.
Kwa upande wake mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad (ACT Wazalendo) amesema bado hakujawa na dhamira ya kweli hata kujenga vituo vya biashara.
Amesema katika malengo ya serikali wanatakiwa kuweka mipango ya dharura jambo ambalo halijaonekana kwa dhati.
“Sidhani kama miradi tunayoifanya kwasasa ni muhimu na ya dharura kuliko viwanda, maana viwanda vinatoa ajira na kukuza uchumi wetu, hapa bado kuna changamoto,” amesema.