Dar es Salaam. Mamia ya waumini wa kituo cha sala na maombezi cha Mama Bikira Maria (Marian Faith Healing), kilichokuwa kikiongozwa na Padri Felician Nkwera (89), walijitokeza leo katika misa na kuuaga mwili wa kiongozi huyo, shughuli iliyotawaliwa na vigelegele vikiambatana na vilio.
Padri Nkwera ambaye muasisi wa kituo hicho alifariki dunia Mei 8, 2025 katika hospitali ya TMJ alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuzidiwa ghafla.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa huduma za maombezi wa kituo hicho, Deogratias Karulama, maziko yatafanyika kesho Mei 17, 2025 kituoni hapo, Ubungo Riverside, Dar es Salaam yakitanguliwa na misa.
Karulama alisema jana kuwa, viongozi wa kiserikali na wa kiroho kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria maziko, shughuli inayotarajiwa kuanza saa tatu asubuhi.
Mwili ulivyoagwa
Mwili wa Padri Nkwera ulifikishwa kituoni hapo jana saa 5:30 asubuhi ukitokea Hospitali ya Lugalo ulikokuwa umehifadhiwa.
Awali, saa nne asubuhi umati wa waumini ulijitokeza eneo la Daraja la Kijazi, Ubungo, Dar es Salaam kuupokea na kuusindikiza hadi kituoni. Msafara kuelekea kituoni uliongozwa na pikipiki ya Jeshi la Polisi, mwili ukiwa kwenye gari maalumu jeusi lililopambwa kwa maua.
Waumini waliovaa fulana nyeupe zikiwa na picha ya Padri Nkwera na wanawake wakiwa na kanga maalumu, walitembea kwa miguu kwenye msafara huo.

Baada ya mwili kuwasili kituoni viongozi wa kiroho wa kituo hicho walishusha jeneza na kuwakabidhi vijana wanane walioliingiza jeneza kituoni.
Wakati jeneza lenye mwili likiingizwa kituoni, waumini wanawake walitandika nguo zikiwamo kanga na mitandio chini ikiwa ni ishara ya heshima kwa kiongozi wao.
Vijana waliokuwa wamevaa fulana nyeupe, suruali nyeusi na glovu nyeupe walitembea kwa mwendo wa polepole kisha wakaweka jeneza kwenye chumba maalumu, ambako viongozi wa kituo hicho na wanafamilia walitoa heshima za mwisho.

Shughuli hiyo iliongozwa na Mtenda Kazi, Sista Eledina Ntandu. Baadaye waumini wengine walipata fursa ya kuaga mwili wa mpendwa wao.
Akitoa salamu, Sista Ntandu alisema huduma za maombezi katika kituo hicho zitaendelea kama kawaida baada ya kumalizika kwa shughuli ya maziko.
“Baba (Padri Nkwera) amekwenda lakini kazi ya Mungu bado itabaki kuishi, niwahakikishie kwamba huduma katika kituo hiki zitaendelea na zitakuwa zikiongozwa na Mtenda Kazi, Sista Eleidina,” alisema.
Uvuaji viatu
Ikiwa ni utaratibu wa kawaida kwa waumini wanaofika kituoni hapo kuvua viatu na kuviacha nje kabla ya kuingia kituoni, suala hilo liliwapa shida wageni waliofika kuomboleza, licha ya mvua kunyesha.
Baadhi yao walionekana wakitafuta mifuko ili kuhifadhi viatu vyao kwa kuhofia visiibwe au kunyeshewa lakini wengine waliviacha.
Kwa walioingia na kutoka ndani ya kituo baadhi walitembea peku pasipo kujali tope lililokuwapo barabarani.
“Nimeshavua viatu, nishatembea sana kwenye tope, hivyo siwezi kuvaa tena mpaka nitakapotoka eneo hili ndiyo maana nimeamua kutembea peku,” amesema mmoja wa waombolezaji.
Suala hilo liliwahi kufafanuliwa na Padri Nkwera enzi za uhai wake kuwa pale wanavua viatu kwa kuwa ni mahali patakatifu, sawa maandiko ya biblia, pale Mungu alipomweleza Musa, “Vua viatu vyako, kwa sababu uliposimama ni patakatifu.”
Barabara yatengenezwa
Barabara ya kuelekea kilipo kituo hicho cha maombezi katika Mtaa wa Bakwata, imesawazishwa kwa kutumia greda.
Mfanyabiashara kando mwa barabara hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Richard, amesema marekebisho ya barabara hiyo imekuwa neema kwao kwa ni kipindi cha mvua ilikuwa ikijaa tope.
“Ukisikia kufa kufaana ndiyo huku, siku zote barabara ilikuwa mbovu lakini baada ya msiba juzi tumeona katapila likipita kukwangua barabara,” alisema.
Kuhusu kifo
Padri Nkwera alifariki dunia saa mbili usiku wa Mei 8 katika Hospitali ya TMJ alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya presha kushuka.
Mwenyekiti wa Huduma ya Maombezi kituoni hapo, Karulama akizungumza na Mwananchi Mei 9 alisema Padri Nkwera alianza kujihisi vibaya Mei 8, asubuhi akiwa kituoni hapo ambako pia ni nyumbani kwake.

Padri Nkwera aliwahi kuhudumu Kanisa Katoliki kabla ya kutengwa na uongozi wa kanisa hilo.
Mbali ya kuwa kiongozi wa kiroho, Padri Nkwera alikuwa mtaalamu wa lugha ya Kiswahili na ametunga vitabu zaidi ya saba vya kufundishia lugha hiyo, kikiwemo kilichokuwa maarafu cha Sarufi na Fasihi kwa Sekondari na Vyuo.