Heche atumia Simba, Yanga kunadi ‘No reforms, no election’ Shinyanga

Solwa. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche ametumia mchezo wa soka kwa kuzitaja timu za Simba na Yanga  kunadi kampeni ya chama hicho ya ‘No reforms, No election’ inayolenga kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi.

Akihutubia mkutano wa hadhara kwa nyakati tofauti katika maeneo ya  Solwa na Mwakitolyo wilayani Shinyanga leo, Mei 16, 2025, Heche amesema soka ni mchezo wa kiungwana wenye sheria na kanuni zinazolinda haki na kutenda haki sawa kwa timu zote, bila kujali ukubwa wala udogo wa washindani.

“Mechi kati ya Simba na Yanga haiwezi kuamuliwa na mwamuzi au mshika kibendera ambaye ni kiongozi wa Simba au Yanga kwa sababu hatatenda haki,” amesema Heche

Huku akishangiliwa, Heche amesema; “Haji Manara hawezi kuwa mwamuzi kwenye mechi kati ya Simba na Yanga… ikiwa hivyo mchezaji wa Yanga atachezewa rafu katikati ya uwanja lakini Manara ataamuru pigo la penati. Vivyo hivyo Ahmed Ally akiwa mshika bendera atamezea offside zote….tena atawaambia wachezaji wasirudi eneo lao wabaki huko huko mbele kwenye goli la Yanga, ili wapigiwe pasi ndefu na wakifunga atalikubali goli kwa kuitisha mpira katikati,” amesema.

Amesema kama ambavyo viongozi wa Yanga na Simba hawawezi kutenda haki wakiwa waamuzi kwenye mechi zinazohusisha timu zao, ndivyo ambavyo viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) walioko kwenye Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) hawawezi kuvitendea haki vyama vya upinzani.

“Ndio maana sisi Chadema tumesema hatushiriki uchaguzi ambao miongoni mwa wanaousimamia ni aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CCM, Omar Ramadhani Mapuri,” amesema Heche.

Amesema Serikali inayoundwa na CCM inaogapa mabadiliko ya sheria kwa sababu itaondoa mianya inayotumika kukipendelea chama tawala.

“Kila wakati viongozi wa CCM na Serikali wanadai Rais Samia Suluhu Hassan anaupiga mwingi, sasa wanaogopa nini? Warekebishe sheria na mfumo kuwezesha uchaguzi huru na haki kwa wagombea na vyama vyote,” amesema.

Amesisitiza msimamo wa chama chake wa kutoshiriki uchaguzi wowote katika mfumo na sheria zilizopo kwa sababu uzoefu wa chaguzi za mwaka 2019, 2020 na 2024 unadhihirisha kuwa wagombea kupitia vyama vya upinzani hawatatendewa haki.

Amedai haiba ya CCM mbele ya umma imeshuka, ndio maana inahofia mabadiliko ikijua Watanzania watainyima kura na kuiondoa madarakani iwapo uchaguzi utakuwa huru na haki.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema (Bazecha), Suzan Lyimo amewaomba wazee wote nchini kuunga mkono kampeni ya mabadiliko yatakayohakikisha viongozi wa kisiasa wanapatikana kwa haki, kupitia kura za wananchi na hivyo kuwajibika kwa umma.

Amesema Serikali inayopatikana kwa nguvu ya kura itawajibika kwa wananchi kwa sababu viongozi watahofia kuwajibishwa wasipotimiza wajibu.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila amewataka vijana nchini kuwa chachu ya mabadiliko, akisema kote duniani, mabadiliko ya kweli huletwa na vijana na masikini wanaopigania maisha bora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *