Meatu. Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimefanikiwa kuwasilisha taarifa ya hali ya kisiasa nchini katika mkutano wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IDU) unaofanyika mjini Brussels, Ubelgiji, licha ya Jeshi la Polisi kumkamata na kumzuia Naibu Katibu Mkuu wao, Amani Golugwa kuhudhuria mkutano huo.
Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Mwanhuzi wilayani Meatu leo Mei 15, 2025, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche amesema taarifa hiyo imewasilishwa kwenye mkutano wa IDU kupitia kwa Alicia Lissu ambaye ni mke wa Mwenyekiti wa Chadema, Tindu Lissu.
“Walimkamata Naibu Katibu Mkuu wetu Amani Golugwa kwa lengo la kumzuia kuhudhiria mkutano wa IDU; walijua angeeleza dunia jinsi Serikali inavyokiuka haki za kiraia na demokrasia. Sasa tumefanikiwa kuwasilisha taarifa hiyo kupitia kwa mke wa Mwenyekiti ambaye yuko kule Ubelgiji,” amesema Heche.

Alicia Lissu mke wa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu. Picha na Mtandao
Huku akishangiliwa na umati uliohudhuria mkutano huo, Heche amesema; “Chadema tutaendeleza mapambano ya kudai haki na demokrasia kwa kuibana Serikali ndani na nje ya nchi hadi kieleweke,” amesema.
Utayari wa kushiriki uchaguzi
Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao, Makamu Mwenyekiti huyo amesema chama hicho kiko tayari wakati wowote kushiriki uchaguzi, lakini kwa sharti la kufanyika kwa mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi.
“Chadema hatuogopi uchaguzi na tuko tayari kuingia kwenye uchaguzi wakati wowote kwa sababu tunaungwa mkono na umma wananchi, lakini hatuko tayari kushiriki uchaguzi kwa sheria na mfumo uliopo usiotoa haki kwa wagombea wetu,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mwalilo Mnadani wilayani Meatu.
Amesema Serikali ya CCM inaogopa mabadiliko kwa sababu itaondoa mianya inayotumika kuwaengua wagombea kupitia vyama vya upinzani.
“Kila siku wanasema Serikali inaupiga mwingi, sasa kwa nini wanaogopa mabadiliko yatakayoweka sawa uwanja wa siasa kwa vyama vyote?” amehoji Heche.
Huku akishangilia na waliokuwa wakimsikiliza, Heche amesema; “Kama CCM na Serikali inajiamini, basi warekebishe sheria na mfumo tuwe na uchaguzi huru; wagombea wapigiwe kura tuone nani atashinda. Haki ya Mungu Chadema tutashinda asubuhi na mapema,” amesema.
Amewaomba vijana kote nchini kuunga mkono harakati za kudai mabadiliko akisema kundi hilo, hasa vijana maskini wasiokuwa na uhakika wa maisha ya kesho ndilo chachu na mabadiliko kote duniani.
“Watu wenye uwezo kiuchumi na viongozi hawahitaji mabadiliko kwa sababu ni wanufaika ya hali iliyopo; hawa wanaogopa mabadiliko kwa kuhofia maslahi yao,” amesema
Mahinyila awavaa Polisi
Akihutubia mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Deohratius Mahinyila amelitaka Jeshi la Polisi kuacha kukisaidia CCM kwa kuingilia shughuli za kisiasa za vyama vya upinzani, hasa Chadema.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mwalilo Mnadani wilayani Meatu.
“Jana tulifanya mkutano mkubwa mjini Musoma na baada ya Makamu Mwenyekiti kumaliza kuhutubia, wananchi wakaamua kumsindikiza kwa amani, lakini cha ajabu polisi wakawatawanya kwa kuwafyatulia mabomu ya machozi. Vitendo vya namna hii siyo tu vinakiuka haki, bali pia vinachochea chuki kati ya Jeshi la Polisi na wananchi,” amesema Mahinyila.
Kiongozi huyo wa vijana amewashauri viongozi katika ofisi za umma kutambua kwamba iko siku wataondoka kwenye nafasi hizo kwa sababu vyeo na nafasi zao ni za muda.
“Wapo watu walikuwa na nafasi za juu lakini sasa hawapo katika nafasi hizo. Viongozi katika ofisi za umma wafahamu vyeo vyao ni koti la kuazima. Iko siku wataondoka,” amesema Mahinyila.