
Dar es Salaam. Lori la mafuta mali ya kampuni ya Lake limepata ajali na kupinduka eneo la Mbwewe, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, huku baadhi ya wananchi wakifika eneo la tukio na kuanza kuchota mafuta yaliyokuwa yakivuja kwenye tenki la lori hilo.
Kipande cha video kilichosambaa kwenye mitandao ya kijamii kinaonyesha watu waliobeba madumu wakichota mafuta yanayovuja kutoka kwenye tenki la lori, jambo linalohatarisha usalama wao.
Akizungumza na Mwananchi leo Mei 16, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo leo, huku akieleza kwamba hakuna madhara yaliyojitokea kwa binadamu.
“Ni kweli kuna ajali imetokea saa 4 asubuhi, eneo la Mbwewe na askari wamefika haraka kwa sababu sehemu ilipotokea ajali kuna vikosi vyote vya polisi na hakuna madhara yaliyotokea kwa binadamu, zaidi ya uharibifu wa miundombinu,” amesema Kamanda Lutumo.
Hata hivyo, amesema kikosi kingine kimetoka mkoani kikiambatana na wataalamu wa ufuatiliaji wa majanga kwenda kwenye ajali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Shuhuda aliyekuwepo eneo la tukio, Masoud Maulid amezungumza na Mwananchi kwa simu akisema lori hilo limetokea Dar es Salaam kuelekea Arusha na lilipofika eneo hilo liliacha njia na kuanguka.
“Hatujui dereva alilala au vipi maana njia ilikuwa nyeupe, haina chochote, akajikuta anapoteza mwelekeo na kuangusha gari, lakini dereva amepona na tumekuwa naye hapa kwenye tukio na yeye hajui ajali imetokeaje,” amesema Maulid.
Alipozungumza na Mwananchi kuhusu elimu ya usalama barabarani, Mkuu wa Usalama Barabarani, Mrakibu Mwandamizi, Edson Julius amesema ajali zinazotokea ni kutokana na uchovu wa madereva na msongo wa mawazo.
“Elimu tunatoa mara kwa mara kwa madereva kwa kurejea baadhi ya ajali na wanachopaswa kufanya lakini haya mambo bado yanaendelea na tukifuatilia makosa yanakuwa ya madereva,” amesema Kamanda Julius.
Amesema ajali ambazo zinatokea eneo la tambarare madereva wanakuwa wamechoka hivyo kuhama njia na kusababisha ajali.
Kamanda Julius amesema bado kikosi cha usalama barabarani wataendelea kutoa elimu kwa madereva hata wanapowasimamisha wamekuwa wakiwaeleza vitu vya kufanya.
Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Pwani, Jennifa Shirima amesema kwa kushirikiana na vikosi vingine vya polisi wamehakikisha kuna usalama wa kutosha na kinachosubiriwa kwa sasa ni kufika kwa lori lingine kwa ajili ya kuhamisha mafuta.
Amesema baada ya kutokea kwa ajali hiyo, tenki zilianza kuvujisha mafuta aina ya petroli, wakati hilo likiendelea wananchi walifika kwa ajili ya kuchota mafuta lakini jeshi lilifika haraka na kuwadhibiti wananchi wote waliokuwa wakiendelea na shughuli hiyo na kuwaondoa eneo hilo.
“Kikosi chetu kilifika eneo la tukio haraka na walikuta mafuta yanamwagika jambokuwa sio mengi na tulifanikiwa kuwaondoa watu wote waliokuwepo eneo la tukio kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa na hapa kinachosubiriwa ni gari lingine kwa ajili ya kuhamisha mafuta,” amesema Kamanda Jennifa.
Ajali hiyo inafanana na ile iliyotokea Aprili 14, 2024 eneo la Misugusugu, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, huku baadhi ya wananchi wakifika kwenye tukio na kuanza kuchota mafuta yaliyokuwa yakivuja kwenye tenki la lori.
Pia, Agosti 10, 2019 katika eneo la Msamvu mjini Morogoro, watu zaidi ya 100 walipoteza maisha baada ya lori la mafuta lililopinduka kulipuka wakati wananchi wakichota mafuta.
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ilipokea majeruhi 47 waliofikishwa hospitalini hapo kwa nyakati tofauti wakitokea Morogoro ili kupatiwa matibabu na baadhi yao walipona na wengine kufariki dunia.