
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wamiliki wa vyombo vya moto vinavyotumia umeme kama pikipiki na maguta kusajili na kubandika vibao vya namba (plate number) kuanzia leo Mei 16 hadi Juni 30, 2025.
Kwa mujibu wa tangazo lao lililochapishwa katika gazeti la Mwananchi, TRA imebaini kuongezeka kwa matumizi ya vyombo hivyo vya usafiri hasa mijini na mara nyingi havina usajili wala utambulisho rasmi, jambo linalochangia ongezeko la uhalifu na ajali zisizo na ufuatiliaji wa kisheria.
“TRA inapenda kuutaarifu umma kuwa, kuanzia Mei 16 hadi Juni 30, 2025, watumiaji wote wa vyombo hivyo vikiwemo pikipiki, maguta na vinginevyo wanatakiwa kusajili na kubandika vibao hivyo ndani ya muda uliotolewa.
“Takwa hili ni kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani (The Road Traffic Act, 1973) Kifungu Namba 8 (1) kinachomtaka kila mtumiaji wa chombo cha moto barabarani kutimiza wajibu huo. Baada ya tarehe hiyo, hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wale wote ambao hawatatekeleza jukumu hilo,” inaeleza taarifa hiyo ya TRA.
TRA imeukumbusha umma kuwa imefanya maboresho ya mfumo wa usajili wa vyombo vya moto kwa lengo la kurahisisha usajili wa vyombo vyote vinavyopaswa kusajiliwa kisheria. Mfumo huo unapatikana kupitia tovuti ya TRA (www.tra.go.tz) au Ofisi za TRA zilizopo nchi nzima.
Wakizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam, baadhi ya madereva wameonyesha hisia mseto kuhusu tangazo hilo la TRA ambapo baadhi yao wakieleza kutokuwa na taarifa kuhusu tangazo hilo huku wengine wakijua.
Ally Mahamudu, mkazi wa mbezi, amesema hajui kama kuna tangazo linawataka kufunga namba za usajili kwenye pikipiki ndogo za kuchaji na hata kama wameamua hivyo, sio mbaya kwani hakuna namna kama serikali imesema.
“Hatupingi kusajili, lakini Serikali iweke mazingira rafiki. Pikipiki hizi nyingi tunazitumia kwa kujikimu tu, hata faida yenyewe ni ndogo, kwani hizi pikipiki sio za biashara,” amesema Mahamudu.
Kwa upande wake, Sada Musa ambaye ni dereva wa guta anafanya shughuri zake maeneo ya Mbezi sokoni amesema madereva wa guta maeneo ya mbezi hawana taarifa ya kuwataka kufanya hivyo kwani uongozi wao wa soko umelala.
“Hadi leo sijui tunaanzia wapi kusajili maana uongozi wetu wa soko haujatupa taarifa yoyote hadi sasa. Hata TRA hawajatufikia moja kwa moja kutoa elimu. Wakituonyesha njia, sisi tuko tayari,” amesema Sada, mwanamke anayeendesha guta Mbezi Sokoni.
Akiunga mkono uamuzi huo wa TRA, Joel Mwampamba, dereva wa bodada Temeke amesema: “Tumechoka kuona pikipiki zisizotambulika zikihusika na uhalifu halafu dereva anatokomea bila kujulikana. Namba za usajili zitasaidia sana kwenye hilo.”