Dar es Salaam. Kuanzia msimu wa masomo wa mwaka 2025/26, waombaji wa mikopo katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) watalazimika kuwa na namba (NIN) au kitambulisho cha Taifa.
Kuwa na NIN au kadi ya Nida limewekwa kuwa takwa la lazima kwa kila mwombaji wa mkopo kupitia HESLB, kwa lengo la kurahisisha utambuzi wa mwombaji na usimamizi wa mikopo inayotolewa kwa wanufaika.
Utekelezaji wa takwa hilo unaanza na wanafunzi wa kidato cha sita ambao wamemaliza mitihani yao ya Taifa, ambao miezi michache ijayo baada ya matokeo kutoka, wanatarajia kujiunga na vyuo vya elimu ya juu na ya vya kati.
Kwa mujibu wa mamlaka, mwombaji ambaye hatakuwa na NIN hataweza kuomba mkopo, hivyo kushindwa kupata huduma nyingine zozote ikiwamo kufungua akaunti za benki.
Hayo yamebainishwa leo Mei 16, 2025 wakati wa mkutano wa pamoja kati ya HESLB na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), walipozungumza na waandishi wa habari kuhusu matumizi ya NIN kwa waombaji wa mikopo 2025/2026.
Kwa miaka yote takwa hilo lilikuwa si kigezo cha lazima kwa wanafunzi wanaoomba mkopo HESLB, bali wamekuwa wakitumia vyeti vya kuzaliwa kama kigezo cha utambulisho wakati wa maombi hayo.

Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia wakati mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Ingawa kitambulisho cha Nida kimekuwa miongoni mwa vigezo, lakini kwa kukikosa, muombaji hakuzuiwa kutuma maombi ya mkopo na hata kuupata.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia amesema wamefikia hatua hiyo kwa lengo la kuonyesha umuhimu wa matumizi ya NIN kwa kila mwombaji wa mkopo kwa mwaka wa masomo 2025/2026.
Amesema dirisha la maombi ya mkopo litafunguliwa Juni 2025, ili kutoa fursa kwa wanafunzi wahitaji kujaza na kuwasilisha maombi yao.
Akizungumzia umuhimu wa NIN katika mchakato wa uombaji na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi, Dk Kiwia amesema ni utambulisho wa uhakika na utasaidia kuthibitisha uhalali wa taaarifa za mwombaji.
“NIN itaiwezesha HESLB kuwa na taarifa sahihi na za kipekee za kila mwanafunzi. Kwa kutumia NIN kutatuwezesha kuboresha uwezo wetu wa kufuatilia wanufaika waliokopeshwa, baada ya kuhitimu,” amesema.
Amesema NIN inahakikisha usalama wa taarifa (data) za mwombaji na kuondoa uwezekano wa matumizi ya majina au taarifa bandia.
“Tumeunganisha mifumo yetu ili kuwezesha kuhakiki taarifa za waombaji mikopo kupitia NIN. Tayari wataalamu wa Tehama kutoka pande zote mbili wanashirikiana kuhakikisha mifumo yetu iliyounganishwa inafanya kazi kwa ufanisi,” amesema.
Amesema kuanzia maombi ya mikopo ya mwaka 2025/2026, NIN itakuwa hitaji la lazima kwa kila mwombaji wa mkopo, hivyo amewataka waombaji wote kuhakikisha wanapata NIN mapema, kabla dirisha la maombi kufunguliwa au ndani ya muda wa maombi ya mikopo kabla ya dirisha kufungwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Nida, James Kaji amesema dhamira ya Serikali kwa ujumla ni kuona kila mwanafunzi aliyemaliza elimu ya sekondari mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea na raia wa Tanzania anasajiliwa na kupata namba (NIN) na kitambulisho cha Taifa.
“Kwa kufanya hivi tutawawezesha wanafunzi kujiunga na masomo ya ngazi za juu na kati na kuomba mkopo wa masomo yao, lakini pia kupata huduma nyinginezo za kijamii na kiuchumi,” amesema.
Amesema kwa kuzingatia hilo, Nida imekuwa na utaratibu wa kutembelea vyuoni kutoa elimu kuhusu usajili na utambuzi wa watu nchini, umuhimu wa namba na kitambulisho cha Taifa kwa wanafunzi na kufanya usajili wa moja kwa moja.
“Tunafurahi wenzetu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu wameona na kutambua jitihada zetu, pamoja na mambo mengine watatuunga mkono katika kutoa hamasa hii kwa vijana wetu.
“Tunapofanya majukumu yetu yaliyo upande wetu, niwaombe wanafunzi kwa upande wao, nao watekeleze wajibu wao kwa kuchukua hatua ya kujisajili mapema,” amesema.