Sababu Lamine Yamal kutumia majina mawili

Barcelona Hispania. Baada ya muda mfupi tu katika soka la kulipwa, Lamine Yamal amekuwa sehemu ya wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Barcelona.

Anakumbukwa akiwa kinda kabisa alipoiwezesha Hispania kutwaa taji la nne la Ubingwa wa Ulaya kwa kuvunja rekodi dhidi ya England, akifunga bao moja na kusaidia mabao manne.

Kiwango chake kimeendelea kuwa bora zaidi kila msimu huu, ikiwa jana aliisaidia Barcelona kutwaa ubingwa wa La Liga, ambapo kijana huyo mwenye umri wa miaka 17, tayari msimu huu amefunga mabao manane, asisti 13 kwenye La Liga akiwa na jezi ya Barcelona baada ya mechi 33, lakini ndiye kinara kwenye eneo hili kwenye La Liga.

 Kwa sasa, anaonekana kuwa na mustakabali mkubwa na anachukuliwa kama mchezaji bora kijana duniani, hakuna shaka kuwa kama angetwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, basi yangezumzwa mambo mengine.

Lakini licha ya mashabiki wa soka kote duniani kumfahamu vyema kwa jina lake, si kila mtu anafahamu asili ya jina lake na sababu ya kwa nini anachagua kuvaa majina yote mawili “Lamine” na “Yamal” mgongoni mwa jezi zake za Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania, kumbuka hata magwiji wakubwa kama Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, David Beckham, na wengine wengi walitumia jina moja tu kwenye jezi zao.

Yamal ana historia ya kipekee inayohusu jina lake. Jina lake kamili ni Lamine Yamal Nasraoui Ebana, ambapo Ebana ni jina la mama yake na Nasraoui ni jina la baba yake. “Lamine Yamal” ni jina la muungano (yaani jina moja linalotenganishwa). Ingawa wengi hudhani “Yamal” ni jina lake la ukoo, si hivyo.

Kama ilivyo kwa jina la “Luis Enrique”, ambalo pia ni la muungano, hivyo ndivyo inavyopaswa kutamkwa “Lamine Yamal”.

Kwa mujibu wa jarida la Tribuna, wazazi wa Yamal walimpa majina “Lamine” na “Yamal” kwa heshima ya watu wawili waliowasaidia kifedha muda mfupi baada ya kuzaliwa kwake.

Katika kipindi hicho kigumu, watu wawili waliitwa Lamine na Yamal mmoja aliwasaidia kulipia kodi ya nyumba na mwingine aliwasaidia mahitaji mbalimbali ya nyumbani.

Baba yake Yamal ambaye jina lake ni Nasraoui alikuwa mzazi wa kipato cha chini ikiwa kazi yake ambayo inamuingizia kipato ni kupaka rangi kwenye nyumba za watu, wakati akiwa anazaliwa kinda huyo hali yake ya kiuchumi ilikuwa mbaya zaidi na hivyo kuhitaji msaada, huku mama yake akiacha kazi kwenye eneo lililokuwa linauza vinywaji, sehemu ambayo alikuwa amefanya kazi kwa muda mrefu kwa ajili ya kutafuta ridhiki.

Hivyo, baada ya kupata msaada huo wa kwanza kufika kwa mzee Nasraoui alikuwa mtu anaitwa Yamal ambaye alilipa kodi ya nyumba, huyu mzee alimuahidi mtu huyu kuwa mtoto atakayezaliwa atampa heshima kwa kumuita Yamal.

Lakini baada ya muda akaja mtu mwingine, akawasaidia kuhusu mahitaji kadhaa ya nyumbani, kikiwemo chakula, maji na vitu vingine, mzee huyu akatoa ahadi kama ile ya mwanzo, kuwa mtoto akizaliwa atampa jina la mtoa msaada.

Hivyo baada ya kuzaliwa, mzee Mounir akaona isiwe taabu, akamuita mwanaye Lamine Yamal, likisimama kama jina moja. hivyo kwenye hayo majina hakuna jina hata moja la mzazi kwa kuwa baba yake Yamal anaitwa sana na baba yake,  akaapa kwamba wakipata mtoto, watampa majina hayo kama ishara ya shukrani.

Yamal alizaliwa tarehe 13 Julai 2007, na wazazi wake wakampa jina la Lamine Yamal Nasraoui Ebana, hilo Ebana ni jina la mama yake ambaye ni mzaliwa wa Equatorial Guinea,  huku Nasraoui likiwa jina la baba yake ambaye ni mzaliwa wa Larache nchini Morocco.

Hata hivyo, pamoja na kupita kwenye shida nyingi, wazazi hawa waliachana mara tu baada ya Yamal kufikisha miaka mitatu, lakini wakaendelea kumlea mtoto pamoja, lakini malezi yake ya soka yamepitia kwa mama yake zaidi.

Jina lake pia lina maana maalumu, likiwa linamaanisha “uaminifu” na “uzuri” kwa Kiarabu misingi ambayo kijana huyu ameifuata katika safari yake ya mafanikio. Katika kituo cha kukuza vipaji cha Barcelona, La Masia, alikuwa anaelezewa kama kijana mnyenyekevu, mpole na makini ambaye haonyeshi kama yeye ni umaarufu.

Lakini mara tu anapokuwa uwanjani, unyenyekevu huo hubadilika kuwa nguvu na uwezo wa kipekee wa kisoka, ana ndugu zake wawili Keyne aliyezaliwa mwaka 2022 na dada yake anaitwa Baraa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *