
Nchini Chad, dazeni kadhaa za watu wamefariki katika “makabiliano makali” katika kijiji cha Mandakao, katika jimbo la Logone Occidental, karibu na mpaka wa Cameroon. Kulingana na vyanzo rasmi, idadi ya waliofariki imefikia 41 na majeruhi kadhaa.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwanahabari wetu huko Ndjamena, Nadia Ben Mahfoudh
Kijiji cha Mandakao kilishambuliwa siku ya Jumatano, Mei 14. Kulingana na chanzo cha mahakama, kambi mbili za watu wa kuhamahama na takriban vibanda 80 vilichomwa moto. “Wakazi waliuawa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto,” kulingana na chanzo kimoja. Watu kadhaa waliojeruhiwa walisafirishwa hadi hospitali ya wilaya ya Beinamar, takriban kilomita 80 kutoka Moundou. Baadhi yao walifariki kutokana na majeraha yao.
“Mauaji mabaya kabisa”
Watu kadhaa waliopo Mandakao wanaeleza kuwa mzozo baina ya jamii ndio chanzo cha makabiliano haya. “Mgogoro wa aina hii upo,” kimesema chanzo cha mahakama, “lakini hali ni mbaya zaidi kuliko kawaida.” Kabla ya kuongeza kwamba “mauaji hayo yalikuwa mabaya sana. Mauaji hayo yamesababisha maombolezo katika kijiji kizima.”
Utulivu warejea
Sababu haswa bado hazijafahamika, uchunguzi umefunguliwa ili kutoa mwanga juu ya suala hilo. Vikosi vya ulinzi na usalama vya Chad, vilivyotumwa haraka kwenye eneo la tukio, tayari vimewakamata watu 82 kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea. Siku ya Alhamisi, Waziri wa Usalama na Waziri wa Tawala za Mikoa walizuru kijiji hicho na hali ya utulivu imerejea.