Baada ya Vijana kuifinya Savio UDSM, Stein kazi ipo

KIWANGO cha chini kilichoonyeshwa na Savio kilisababisha ifungwe na Vijana ‘City Bulls’ kwa pointi 70-50, katika Ligi ya kikapu Dar es Salaam inayofanyika katika Uwanja wa Donbosco, Upanga.

Savio iliyowahi kuwa bingwa wa  ligi hiyo ya BDL 2015, 2016, 2017, 2018 na 2021, ilishindwa kuonyesha makali yao kama ilivyozoeleka.

Katika mchezo huo, ilionekana haijajianda vizuri kuhimili mikikimikiki ya ligi hiyo mwaka huu.

Timu hiyo iliyoongozwa na mkongwe Cornelius Mgaza na iliyozoeleka kujipanga vizuri katika mzunguko wa pili, imeonyesha itakuwa na  wakati mgumu kufanya vizuri kutokana na mfumo unaotumika mwaka huu wa kucheza mzunguko mmoja.

Kocha wa Vijana ‘City Bulls’, Kabiola Shomari alisema wachezaji  waliowatumia kuiangamiza Savio ni waliowasajili kutoka  kikosi chao cha pili cha Jogoo.

Timu zitakazoshika nafasi nane za juu zitacheza hatua ya robo fainali na tatu za chini zitashuka daraja.

Kazi ipo kesho katika mchezo kati ya UDSM Outsiders na Stein Warriors, wa Ligi ya kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BDL), utakaopigwa Uwanja wa Donbosco, Upanga.

Mchezo huo utakuwa ni pili kwao na wa kwanza UDSM iliishinda JKT kwa pointi 60-56, huku  Stein Warriors ikiishinda KIUT kwa pointi 70-62.

UDSM iliyofanya maandalizi kwa kipindi kifupi kutokana na nyota wake sita kutimkia Stein Warriors na JKT, imeonyesha imedhamiria kufanya makubwa katika ligi ya mwaka huu. 

Wachezaji waliotimukia Stein Warriors ni Tyrone Edward, Mwalimu Heri, Evance Davies, huku wengine Baraka Sabibi na Jimmy Brown wakijiunga na JKT.

Baada ya kuondokewa  wachezaji hao, UDSM ilisajili wachezaji  wapya ambao ni Abdul Chinewengwe, Mikado Ebengo na Felix Mteba.

Stein iliyopanda daraja mwaka huu, imeonyesha imejianda vizuri  katika ligi ya mwaka huu na inafundishwa na Karabani Karabani, pia ilichomoa nyota wa JKT,  Jonas Mushi na Felix Luhaba ambao ni mafundi wa kufunga katika eneo ya mtupo mmoja wa ‘pointi tatu’.

Michezo mingine itakayochezwa uwanjani hapo ni DB Lioness dhidi ya Kigamboni Queens, Vijana Queens dhidi ya City Queens na JKT itacheza na Mgulani  JKT.

UDSM, JKT zafunika

Baada ya michezo 11 ya ligi hiyo,  UDSM Outsiders dhidi ya JKT ndiyo  unaotajwa kuvutia hadi sasa kutokana na ushindani  mkubwa ulionyeshwa katika robo zote nne. 

Nyota wa timu hizo pia walicheza na kuzitendea haki nafasi zao vizuri uwanjani, hali iliyofanya mchezo uvutie.

Omary Sadiki wa  JKT na Felix Mteba wa UDSM, wanaocheza nafasi ya namba 1 ‘Point Guard’ walionekana  ni burudani tosha katika mchezo huo. Wengine ni Baraka Sabibi wa JKT anayecheza namba 2 ‘Shooting Guard’ na Mikado Ebengo walivutia kwa jinsi wanavyotumia vizuri nafasi za kufunga.

Katika mchezo huo,  timu ya UDSM Outsiders ilishinda kwa pointi 60-56.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *