Libya: Mapigano makali yazuka kati ya makundi hasimu yenye silaha katika mji mkuu Libya

Mapigano makali kati ya makundi hasimu yenye silaha yamezuka tena katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, na kuendelea Jumatano katika maeneo kadhaa yenye watu wengi, baada ya mapigano katika siku za hivi karibuni na kusababisha vifo vya watu wasiopungua sita, kulingana na vyanzo vya usalama.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

“Mapigano yameanza tena huko Tripoli, wakati huu kwa kiwango kikubwa, yakienea katika maeneo kadhaa, kati ya Kikosi cha Radaa na Brigade 444,” afisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ameliambia shirika la habari la AFP, akimaanisha mapigano yanayohusisha silaha nzito.

Kikosi cha Radaa hakiko chini ya mamlaka ya Waziri Mkuu wa serikali ya Tripoli, Abdelhamid Dbeibah, wakati Brigade 444, iliyo chini ya Wizara ya Ulinzi, inamuunga mkono.

Siku ya Jumanne, Bw. Dbeibah alitangaza kuvunjwa kwa kikosi cha Radaa, pamoja na kuvunjwa kwa vyombo vya usalama vilivyokuwa vimedhibitiwa hapo awali na kundi jingine lenye nguvu lenye silaha, SSA (Mamlaka ya Usaidizi wa Utulivu), ambalo kiongozi wake, Abdelghani “Gheniwa” el-Kikli, aliuawa siku ya Jumatatu jioni.

Hakuna ripoti za wahasiriwa au majeruhi zimetolewa katika mapigano hayo mapya.

Milipuko mikubwa ilisikika katika jiji lote, haswa magharibi na kusini mwa Tripoli, ambapo makundi “yanaunga mkono Kikosi cha Radaa yalikuja kusaidia kikosi hiki dhidi ya vikosi vya Brigade 444,” kulingana na chanzo cha usalama.

Kwa mujibu wa chanzo kingine kilichoarifiwa kuhusu hali hiyo, kundi lenye silaha kutoka Zawiya, kilomita 45 magharibi mwa Tripoli, liliingia katika kitongoji kimoja magharibi mwa Tripoli “kukusaidi  kikosi cha Radaa.”

Watumiaji wa mtandao wameshiriki picha za magari yanayoteketea kwa moto na majengo yaliyokumbwa na mashambulizi.

Kulingana na ripoti rasmi, watu wasiopungua sita waliuawa wakati wa mapigano makali kati ya makundi hasimu yenye silaha usiku wa Jumatatu kamkia Jumanne. Mapigano hayo yalifuatia tangazo la Jumatatu jioni la kifo cha “Gheniwa”, mkuu wa kundi lenye silaha lenye nguvu zaidi huko Tripoli, aliuawa katika hali isiyoeleweka wakati alikuja kwa upatanishi katika kambi ya kikosi cha Brigade 444.

Kukiwa na mgawanyiko tangu kuanguka na kifo cha dikteta Muammar Gaddafi mwaka 2011, Libya inatawaliwa na serikali mbili hasimu: ile ya Bw. Dbeibah, inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, na nyingine mashariki, inayodhibitiwa na kiongozi wa kivita Marshal Khalifa Haftar.

Licha ya jamaa kurejea kwa hali ya utulivu katika miaka ya hivi majuzi, mapambano ya ushawishi mara kwa mara yanaripotiwa kati ya maelfu ya makundi yenye silaha haswa huko Tripoli na magharibi mwa nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *