Aliyekuwa naibu wa rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, ambaye kwa sasa ni mkosoaji mkubwa wa aliyekuwa bosi wake rais William Ruto, baadae hivi leo anatarajiwa kuzindua chama kipya ambacho anasema kitatumika kumng’oa Ruto madarakani katika uchaguzi ujao.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Kulingana na vyanzo vya karibu na Rigathi, chama atakachokizindua kitafahamika kama Democracy Citizens Party (DCP), ambacho hata hivyo kilisajiliwa mwezi Februari mwaka huu.
Licha ya kwamba jina la chama hicho halijawekwa wazi kwa umma, waliokaribu na shughuli zake wanasema kauli mbiu ni Kazi na Haki.
Jumanne ya wiki hii, Gachagua na washirika wake waliripotiwa kukutana faragha kupanga na kuamua uongozi wa chama hicho na namna ya kuzuia uuingiliaji wa serikali.
Miongoni mwa wanasiasa tajika wanaohusishwa na chama cha Rigathi ni pamoja na Kalonzo Musyoka, aliyewahi pia kuwa makamu wa rais, Martha Karua, Eugene Wamalwa na Fred Matiang’i, waliohudumu katika serikali ya Uhuru Kenyatta.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema huenda serikali ikatumia rasilimali zake kuwavuta washirika wa Rigathi serikali pamoja na kuhujumu harakati zake.