Ukraine na Urusi kwa mara ya kwanza zinatarajiwa kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana baada ya zaidi ya miaka 3 tangu mataifa hayo yaingie vitani, huku rais Vladmir Putin akiwa hayuko kwenye orodha ya ujumbe utakaosafiri kwenda Uturuki.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Awali rais wa Ukraine, Volodymry Zelensky alimtaka rais Putin kukutana nae ana kwa ana mjini Instanbul, kuonesha kweli ana nia ya kupata suluhu ya mzozo unaoendelea, hata hivyo Urusi imeamua kutaja timu ya ujumbe wa kawaida kushiriki mazungumzo hayo.
Wachambuzi wa mambo wanasema kutokuwepo kwa rais Putin ni pigo jingine katika juhudi za kusaka suluhu ya vita kati ya nchi yake na Ukraine.

Wiki iliyopita rais Putin alipendekeza Mei 15 yafanyike mazungumzo ya amani ya moja kwa moja kati yake na Ukraine, kauli iliyoonekana kama ishara chanya, ingawa viongozi kadhaa wa Ulaya walihoji utashi wa Moscow.
Vyanzo vya kidiplomasia vilivyo karibu na mchakato ulioanzishwa na Marekani, vinasema kutokuwepo kwa maofisa wa juu toka Moscow na Washington, ni ishara ya wazi kuwa hakuna hatua itakayopigwa kuelekea usitishwaji wa kudumu wa mapigano.