Simba yapewa nondo za kukwepa mtego wa Berkane

SIMBA tayari ipo Morocco ikijichimbia jijini Casablanca ili kujiandaa na mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Manispaa mjini Berkane, huku kikosi hicho kikipewa nondo muhimu za kuukwepa mtego  wa wenyeji wao RS Berkane.

Simba itavaana na RS Berkane katika mechi hiyo ya mkondo wa kwanza kabla ya kurudiana wiki moja baadaye kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, huku kombe likiwa uwanjani na Wekundu hao wakitaka kuandika historia iliyoishinda Yanga misimu miwili iliyopita.

Yanga ilikwama kubeba taji la michuano hiyo baada ya kufika fainali msimu wa 2022-2023 kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla dhidi ya USM Alger ya Algeria yakiwa ni sare ya 2-2, ikipoteza nyumbani kwa mabao 2-1 kisha kushinda ugenini kwa bao 1-0 na Waalgeria kubeba taji.

Ikiwa imetoka kuing’oa Stellenborch ya Afrika Kusini katika mechi ya nusu fainali, huku ikiwa na rekodi ya kucheza fainali ya Kombe la CAF 1993 na kupoteza nyumbani mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast, Simba ina kazi ugenini na nyota wa zamani wa kimataifa, Ally Mayay ameipa mbinu huko.

Kiungo huyo wa zamani wa CDA, Yanga na Taifa Stars, amesema Simba ina nafasi kubwa ya kupata matokeo mazuri ugenini, iwapo tu itaboresha safu ya ulinzi ili kujihakikishia haiwapi nafasi Berkane kisha kuja kumalizia kazi nyumbani Mei 25.

Mayay alisema mara nyingi timu za Afrika Kaskazini, maarufu kamam Waarabu wanazifunga timu za Tanzania katika mipira ya kutenga kama faulo, kona na penalti kutokana na makosa yanayofanywa na mabeki, jambo aliloshauri kwa Simba kuweka umakini kuhakikisha mwaka huu wanaandika rekodi itakayoipa nchi heshima.

“Kocha Fadlu Davids kafanikiwa kutengeneza timu inayotembeza mpira uwanjani, hilo litasaidia  kutengeneza nafasi za kufunga, mfano kama wanavyocheza kina  Leonel Ateba, Jean Charles Ahoua, Elie Mpanzu na wengine unaona wachezaji wana fiziki na fitinesi, jambo ambalo litawasaidia zaidi,” alisema Mayay aliyewahi kuwa kaimu mkurugenzi wa michezo.

Mastaa hao aliowataja Mayay ambao ni  Ahoua katika Ligi Kuu ana mabao 15, asisti saba na Ateba (mabao 12) na Mpanzu mabao matatu na asisti tano.

Mayay alimzungumzia kipa Moussa Camara aliye na ‘clean sheet’ 16 kuhakikisha anapotaka kutoka langoni awe na uhakika wa kwenda kuugusa mpira vinginevyo awe anafanya uamuzi wa kusalia eneo lake.

“Ni kipa mzuri ila awe anahakikisha anaendana na matukio ya mpira kuuwahi. Fainali hiyo ni muhimu kwa Simba na kwa heshima ya nchi, hivyo kila mchezaji lazima awe makini katika eneo lake,” aliongeza Mayay ambaye majeraha na shule ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kumtoa uwanjani mapema.

Mayay akiyasema hayo, rekodi zinaonyesha Berkane imekuwa hatari zaidi ikicheza nyumbani, kwani haijapoteza mchezo  msimu huu katika michuano ya CAF ikifunga mabao 18 bila kuruhusu bao.

Hii ni mara ya tatu Simba kukutana na Berkane kwani 2021-2022 zilivaana hatua ya makundi na kila moja kushinda nyumbani, Simba ikianza na 1-0 na kulala 2-0 ugenini.

Rekodi zinaonyesha katika mechi sita za nyumbani kwa msimu huu kuanzia raundi ya pili, Berkane imshinda zote na kufunga mabao hayo, ikianza kuifunga Dadje ya Benini 5-0, kisha makundi ikatoa vichapo kwa CD Luanda ya Angola kwa 2-0, itaizabua Stade Malien ya Mali bao 1-0 na kuinyoa Stellenbosch 5-0.

Hatua ya robo fainali iliifunga Asec Mimosas ya Ivory Coast kwa bao 1-0 na nusu fainali ikaifunga CS Constantine ya Algeria kwa mabao 4-0.

Wakati kwa mechi za ugenini, mabingwa mara mbili wa michuano hiyo, ilicheza pia sita na kushinda nne, ikipoteza moja na kutoka sare moja, ikifunga mabao matano na kufungwa mawili tu, kuonyesha sio timu nyepesi na kocha Fadlu Davids wa Simba na mastaa wa timu hiyo wanapaswa kujipanga.

Kwa mechi ya raundi ya pili, Berkane ilianza ugenini kwa kuifunga Dadje mabao 2-0, kisha makundi iliilaza Stellenbosch 3-1, ikailaza Stade Malien kwa bao 1-0, huku ikilazimishwa suluhu na CD Luanda, wakati hatua ya robo fainali iliishinda Asec pia bao 1-0 na nusu ndipo ikalala 1-0 kwa Constantine.

Hata hivyo, Simba kwa msimu huu imekuwa na rekodi nzuri kidogo kwa mechi sita za ugenini za CAF imeshinda moja dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia hatua ya makundi, imetoka sare tatu, ikiwamo moja ya raundi ya pili dhidi ya Al Ahli Tripoti ya Libya, kisha Bravos ya Angola hatua ya makundi na ile ya nusu fainali dhidi ya Stellenbosch, ikipoteza mbili zote za Afrika Kaskazini, makundi dhidi ya CS Contantine ya Algeria na Al Masry ya Misri katika robo fainali.

Hii ni mara ya tatu kwa Simba kukutana na Berkane kwani msimu wa 2021-2022 zilivaana hatua ya makundi na kila moja kushinda nyumbani, Simba ikianza na 1-0 na kwenda kulala 2-0 ugenini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *