Kitendawili, vita ya majimbo mapya

Dar/mikoani. Ingawa mgawanyo wa majimbo uliofanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) unahusishwa na mbinu ya kupunguza joto la ushindani katika baadhi ya majimbo, kitendawili kimebaki ni wapi kati ya mapya au yale ya zamani wabunge wanaoendelea wataenda kugombea.

Wakati kitendawili hicho kikiendelea, joto la kisiasa linaendelea kupamba moto hata katika majimbo mapya, kutokana na makada wa chama tawala cha CCM na upinzani kuonyesha kiu ya kuwawakilisha wananchi majimboni humo.

Hayo yanakuja ikiwa ni siku mbili zimepita tangu INEC itangaze mgawanyo wa majimbo uliosababisha kuzaliwa kwa majimbo mapya manane na kufanya Tanzania Bara na Zanzibar kuwa na jumla ya majimbo 272.

Majimbo hayo mapya kwa mujibu wa Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele, ni Mtumba (Dodoma), Uyole (Mbeya) na Bariadi Vijijini (Simiyu), Katoro na Chato Kusini (Geita), Itwangi (Shinyanga), Kivule na Chamazi (Dar es Salaam).

Mbeya Mjini

Jimbo la Mbeya Mjini limegawanywa na kuzaa jimbo jipya la Uyole, na huenda kukazaliwa mchuano mzito kati ya CCM na vyama vya upinzani katika nafasi za ubunge.

Ingawa baadhi ya wananchi wa Mbeya wanaona kugawanywa kwa jimbo hilo kumelenga kuleta ahueni ya ushindani wa kisiasa uliokuwepo kati ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson dhidi ya aliyekuwa akinyemelea nafasi hiyo, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, katika moja ya kauli zake, Sugu amewahi kukaririwa akisema yuko tayari kushindana na Dk Tulia kokote atakakogombea.

Duru za siasa zinaonyesha upepo wa Spika huyo upo zaidi katika jimbo jipya la Uyole, na pengine ndiko atakakokwenda kugombea badala ya Mbeya Mjini.

Iwapo ataamua hivyo, kiongozi huyo wa muhimili wa Bunge, mbali na Sugu, huenda pia akakabiliana na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, anayedaiwa kulinyemelea jimbo hilo pia.

Katika Jimbo la Mbeya Mjini nako hakutatosha, kwa kuwa kuna makada kadhaa wa CCM wanaotajwa kuchuana, akiwemo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho (MNEC), Ndele Mwaselela na Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Patrick Mwalunenge, na wote wana nguvu na ushawishi sawa ndani ya chama hicho.

Dar es Salaam

Kwa upande wa Jimbo la Ukonga, mbunge wa sasa na Waziri wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano ya Habari, Jerry Silaa, inaelezwa huenda akasalia katika jimbo hilo na si kwenda Kivule.

Inadaiwa huenda Silaa atabaki Ukonga kwa sababu ndiko ana uhakika wa nguvu kubwa na ndipo yalipo makazi yake, akiamini anaweza kutoboa.

Kwa upande wa Mbagala, mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Abdallah Chaurembo, amesema, “Inawezekana ikawa turufu na inawezekana ikawa maumivu. Kikubwa ni namna gani uliishi na watu. Kama umeishi na watu vizuri, jimbo likigawanywa unashindwa kujua uende wapi kwa sababu pande zote zitakuhitaji.”

Amesema hiyo ndiyo hali inayomkabili yeye kwa sasa baada ya taarifa za kugawanywa kwa jimbo hilo, akisema kila upande anakubalika, hajui aende wapi kati ya Chamazi au Mbagala.

“Kwangu imekuwa kama kuna taharuki jimboni, ukizingatia maeneo yote nina makazi, hawa wa huku wanataka nibaki huku na wa kule wanataka niende. Sasa mtihani ni kuamua,” amesema.

Kwa sababu aliutumia muda wake wa uongozi kutumikia wananchi wote, amesema haimpi wasiwasi wa kura, badala yake amebaki na mkwamo wa kuamua ni wapi aende kwa kuwa kote ana watu.

“Bahati nzuri, hata zilipokuja tetesi za mgawanyo, sikubagua. Niliendelea kufanya kazi kwa sehemu zote,” amesema Chaurembo.

Wakati INEC ikigawa majimbo, moto wa kisiasa umeendelea kushamiri kwa fununu za watu wanaotaka kugombea kuongezeka, ukisubiriwa muda wa mchuano kuanza.

Katika Jimbo la Busanda, ambalo mbunge wake wa sasa ni Tumaini Magesa, wengine wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Kulwa Biteko na MNEC, Evarist Gervas.

Baada ya kugawanywa kwa majimbo hayo, inaelezwa Biteko, ambaye ni kaka wa Mbunge wa Bukombe na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati aliyewahi kugombea katika Uchaguzi Mkuu 2020, atagombea tena katika Jimbo la Katoro.

Kwa upande wa Jimbo la Busanda, wagombea wanaotajwa kushika kasi ni Titus Kabuo, Evarist Gervas na mbunge wa sasa, Tumaini Magesa.

Jimbo la Chato Kaskazini wanaotajwa ni Cornel Maghembe, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Deusdedith Katwale (Mkuu wa Wilaya ya Tabora) na Godfrey Miti.

Kwa upande wa Jimbo la Chato Kusini, mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Dk Medard Kalemani, anatarajia kuchuana na Christian Manunga, ambaye ni mwenyekiti wa halmashauri hiyo anayeelezwa kujipanga kwenye uchaguzi huo.

Kabla halijagawanywa, Jimbo la Bariadi lilikuwa na mvutano kati ya mbunge wa sasa na Naibu Waziri wa Maji, Mathew Kundo, na Masanja Kadogosa, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), ambaye inaelezwa anatarajia kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Kwa sasa, Kundo anayetokea eneo la Nkololo anatajwa kugombea Bariadi Vijijini, na Kadogosa, anayetokea eneo la Mwakibunga, huenda akagombea Bariadi Mjini.

Miongoni mwa watu waliokuwa wanatajwa kugombea Jimbo la Solwa ni aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Azza Hamad na Sebastin Kija.

Hata hivyo, baada ya Jimbo la Solwa kugawanywa na kupatikana lingine la Itwangi, majina hayo yanatajwa kugawana kila mmoja jimbo lake, huku upande wa vyama vya upinzani kukiwa kimya.

Kwa upande wa Itwangi, Azza Hamad jina lake limekuwa likitajwa zaidi kuwa atagombea eneo hilo, kwa kuwa analotoka la Tinde liko upande wa jimbo hilo.

Jimbo la Solwa kwa sasa ni shwari, licha ya kuwepo harakati mbalimbali zinazoendelea ambazo hazijawekwa wazi, wakisubiri kipenga cha uchaguzi ili kuruhusu wenye nia kuingia kwenye mchuano.

Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, amewaweka kwenye fumbo makada wa chama wenye nia ya kugombea ubunge kutokana na ukimya wake kuhusu jimbo gani atagombea.

Hata hivyo, kitendawili hicho kitapata uteguzi kesho Mei 15, 2025, atakapoeleza uamuzi wake baada ya kuitisha Halmashauri ya Wilaya Maalumu kwa ajili ya kutoa mwelekeo.

Jimbo analoongoza sasa limegawanywa na kuzaa jimbo jipya la Mtumba, na huko ndiko ambako Mavunde anatajwa kwenda kugombea.

Baadhi wanasema, jimbo atakalochagua Mavunde huenda akakosa mpinzani, na wengi watatamani kwenda katika jimbo ambalo watakuwa wagombea wapya.

Akizungumza na wajumbe wa halmashauri ya wilaya na wajumbe wa mabaraza jana Mei 13, 2025, katika Uwanja wa Jamhuri, Jijini Dodoma, Mavunde aliahidi kuitisha kikao maalumu cha kutoa mapendekezo yake juu ya uchaguzi wa jimbo atakalokwenda kugombea.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa Wilaya imesema kesho, Mei 15, 2025, saa tano asubuhi, katika Ukumbi wa Jiji kutakuwa na kikao ambacho kitabeba ajenda moja.

Hata hivyo, hakuna taarifa rasmi za kuonyesha jimbo alilochagua kugombea, ingawa tetesi zinaonyesha atabaki Jimbo la Dodoma, na hivyo idadi kubwa ya watangaza nia sasa watajazana Mtumba.

Walichokisema wananchi

Kugawanywa kwa majimbo hayo kumepokelewa kwa hisia tofauti, huku baadhi wakiona ni kuongeza mzigo kwa wananchi na wengine wakiona ni vema ili maeneo makubwa wakazi wake wapate huduma ya uwakilishi wa karibu.

Mkazi wa Geita, Kabese John, amesema kugawanywa kwa majimbo hayo ni kuongeza mzigo kwa wananchi na lengo ni kuwanufaisha wanasiasa na si kuleta maendeleo kwa wananchi.

Sabina Athony, mkazi wa Tinde, amesema kwa sasa wanaamini baadhi ya watu waliokuwa na nia ya kugombea ubunge wamepata fursa iwapo watapita kwenye mchakato wa kura za maoni.

Philbert Robert, mkazi wa Katoro, amesema Jimbo la Busanda lilikuwa kubwa lenye kata 22, na ilikuwa ngumu kwa mbunge husika kutekeleza majukumu yake kwa wakati katika kata zote.

“Kugawanywa kwa majimbo haya ni imani yetu tutapata viongozi wazuri walioko karibu na wananchi, na maendeleo pia yatasogea karibu tofauti na ilivyokuwa awali,” amesema.

Ramadhani Sengerema, amesema kugawanywa kwa majimbo hayo kunasaidia kusogeza huduma karibu, kwa kuwa kijiografia jimbo lenye kata 22 ilikuwa ngumu kwa mbunge kutekeleza majukumu yake.

Janeth Maganga, mkazi wa mtaa wa Somanda mjini Bariadi, amesema kuanzishwa kwa jimbo hilo kutarahisisha mawasiliano baina ya wananchi na viongozi.

Mkazi wa Mbagala, Khadija Baraka, amesema kero kubwa katika jimbo hilo ni ubovu wa miundombinu, upatikanaji wa maji safi na salama, pamoja na uhaba wa vituo vya afya.

“Hadi sasa bado maiti zinahifadhiwa Hospitali ya Temeke, bado kuna shida ya upatikanaji wa matibabu. Kituo kinachotegemewa chenye uhakika ni Zakhem, ambacho muda mwingine kinazidiwa,” amesema.

Viongozi wa kisiasa

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamedi, amesema chama chake kimepokea uamuzi huo kwa mikono miwili na kinajipanga kutoa mgombea mwenye uwezo kuipeleka mbele Bariadi Mjini.

“Ni hatua nzuri kwa sababu idadi ya watu Bariadi imeongezeka. Kugawanywa kwa jimbo ni jambo la msingi kwa ajili ya uwiano wa maendeleo,” amesema.

Katibu wa ADA-Tadea Mkoa wa Simiyu, Omari Iddi, amesema kuanzishwa kwa jimbo hilo ni fursa kwa vyama vya upinzani kuwasiliana kwa karibu na wananchi na kusikiliza mahitaji yao.

“Tunataka uchaguzi huru na wa haki katika jimbo hili jipya. Ile thamani ya kura kwa wananchi ionekane; wagombea washinde kupitia kura kwenye boksi na si vinginevyo,” amesema Iddi.

Katibu wa Chadema mkoani Mbeya, Hamad Mbeyale, amesema wamejipanga kusimamisha wagombea majimbo yote yaliyopitishwa na INEC, japokuwa wanasubiri msimamo wa chama Taifa kuhusu mabadiliko wanayohitaji.

“Tuna orodha ndefu sana kila jimbo, watia nia ni wengi na Chadema tumejipanga. Kimsingi, tuna mahitaji yetu kwenye uchaguzi, hasa mabadiliko ya kimfumo na uchaguzi huru,” amesema Mbeyale.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *