
Dar es Salaam. Kampuni inayoongoza duniani katika malipo ya kidijitali, imemteua Victor Makere kuwa Meneja mpya wa nchi za Tanzania, Uganda, Burundi na Rwanda.
Victor ambaye ni raia wa Tanzania atakuwa na jukumu la kuongoza ukuaji wa kimkakati wa Visa, kuboresha uhusiano na wateja, na kupanua suluhisho za malipo ya kidijitali katika masoko hayo muhimu.
Kufuatia uteuzi huo Makamu wa Rais na Meneja Mkuu wa Ukanda wa Afrika Mashariki katika Visa, Chad Pollock, amesema, “tunayo furaha kumkaribisha Victor katika timu ya uongozi ya Visa Afrika Mashariki. Kwa rekodi yake iliyotukuka katika huduma za kifedha za kidijitali na maendeleo ya biashara, kimkakati, tunatarajia mchango wake mkubwa katika juhudi za Visa za kukuza ujumuishaji wa kifedha na kupanua biashara ya kidijitali Tanzania, Uganda, Burundi na Rwanda”
Akizungumzia uteuzi huo, Victor amesema: “Nina furaha kujiunga na Visa na kushiriki kikamilifu katika kuongeza kasi ya ukuaji wa malipo ya kidijitali kwenye nchi za Tanzania, Uganda, Burundi na Rwanda. Dhamira ya Visa katika ubunifu wa kifedha na ujumuishaji wa kifedha inaendana kikamilifu na maono yangu ya kubadilisha mandhari ya malipo. Natarajia kushirikiana na wateja wetu, washirika na wadau ili kuleta suluhisho za malipo za kisasa, salama na rahisi zinazochochea ukuaji wa uchumi na kuwawezesha wafanyabiashara na watumiaji katika ukanda huu.”
Kabla ya kutua Visa Victor, alikuwa Mkuu wa Idara ya Malipo ya Wafanyabiashara wa Airtel Money Tanzania, aliyeongoza kampuni katika mwelekeo wa kimkakati wa malipo ya simu na ya wafanyabiashara. Pia amewahi kushika nyadhifa za juu kwenye benki za CRDB na Standard Chartered, ambako aliongoza mageuzi ya huduma za kidijitali.
Akiwa CRDB, Victor, kama mmoja wa wajumbe waliowakilisha benki kupitia Chama cha Mabenki Tanzania (TBA), alichangia kwa kiasi kikubwa katika kuhamasisha sekta yote kukubali suluhisho za malipo bunifu.
Alisukuma mbele suala la mwingiliano wa mitandao na taasisi za kifedha, na hivyo kuboresha kwa kiwango kikubwa mazingira ya malipo ya kidijitali nchini Tanzania.