Dodoma. Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina amelitaka Bunge kupitisha Azimio la kuifuta Wizara ya Viwanda na Biashara inayoongozwa na Dk Seleman Jafo, akisema imekuwa mwiba wa kuua biashara.
Hata hivyo, mwenye mamlaka ya kufuta au kuanzisha wizara ni Rais wa nchi hivyo Bunge halina mamlaka ya kufuta wizara kama alivyopendekeza waziri huyo wa zamani wa mifugo na uvuvi.
Mpina ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 14, 2025 wakati akichangia kwenye hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2025/26 ambayo ililiomba Bunge kuiidhinishia Sh135.7 bilioni.
Mbunge huyo amesema kama haitawezekana kuifuta wizara, basi watumishi na wasimamizi wake wajitathimini au waondolewe.
“Wizara hii ilitegemewa kuwa kimbilio la wafanyabiashara, kimbilio la waanzishaji wa biashara lakini imekuwa ikihalalisha kuuawa kwa biashara za watu, kama wizara haina uwezo basi ifutwe,” amesema Mpina.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, kuna fedha nyingi zinatengwa kwenye wizara lakini utendaji wake hauna tija.
Katika hatua nyingine, Mpina ameungana na wabunge wengine kulalamikia uingizwaji wa bidhaa zisizokidhi vigezo ambazo ziko chini ya viwango ikiwemo vifaa vya ujenzi.
Amesema kuna nondo zinazoingizwa na kwenda kujenga madaraja na vituo vya afya ambavyo baada ya muda hubomoka.

Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina wakati akizungumza bungeni, leo Mei 14, 2025 .
Hata hivyo, Mbunge wa Bunda (CCM), Mwita Getere kama amemjibu Mpina kinamna hasa aliposema hakuna waziri anayeweza kumaliza matatizo yake yote huku akimtaja aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Katika Serikali ya awamu ya nne, Mpina alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambapo aliingia katika mzozo wa upimaji wa samaki kwa rula pamoja na ukamataji wa nyavu na makokoro na utaifishaji wa vyombo vya wavuvi.
“Hakuna waziri ambaye anaweza kusema kamaliza matatizo yake, alikuwepo Waziri wa Mifugo na Uvuvi mmoja hapa, alikamata makokoro ya watu na nyavu nchi nzima lakini hakumaliza matatizo yote,” amesema Getere.
Ameunga mkono mpango wa waziri katika kupambana na wafanyabiashara kutoka nje wanaofanya biashara kwa mtaji unaoweza kufanywa na wazawa.
Alichokisema Jafo
Akihitimisha hoja yake, Waziri Jafo pamoja na kutoa ufafanuzi wa maelezo mbalimbali amemjibu Mpina akisema mtu anayepinga kila jambo kuna uwezekano akawa na matatizo.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo wakati akijibu maswali ya wabunge leo Mei 14, 2025 bungeni, Dodoma .
“Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu na kijana mwenzangu Mpina yeye anapinga kila kitu hapa inawezekana kuna tatizo mahala,” amesema Jafo.
Waziri amesema mara kadhaa Mpina amekuwa hakubali wala kuunga mkono jambo lolote jambo ambalo linamshangaza, lakini akasema mbunge huyo ni mtani wake anapaswa kujitathimini.