
Walianza kwa kuandika barua, kisha wakatoka na kuzungumza na vyombo vya habari. Walidai kwamba msingi wa wao kutoka hadharani ni baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kudonyoa baadhi ya hoja za barua yao na kuzijibu hadharani.
Mambo mengi yanayozungumzwa ni kinogesho tu. Chanzo kikuu cha mtafaruku ni msimamo wa uongozi wa juu wa chama wa kutoshiriki uchaguzi mpaka mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi yafanyike (No Reforms, No Election).
Hata hivyo, chanzo ni hicho, lakini kuna asili ya mgogoro; ni Uchaguzi Mkuu Chadema uliofanyika Januari 21, 2025.
Tuzungumze kwa kituo; wanachama wa Chadema, ambao wengi wao walikuwa viongozi wa chama hicho katika ngazi mbalimbali za kuchaguliwa na kuteuliwa, baada ya kutupwa nje na uongozi mpya, wakajikuta ndani ya kundi linaloitwa G55. Msimamo wa G55 ni kushiriki uchaguzi, kinyume na shinikizo la uongozi.
Mtazamo wa uongozi haukuegemea hoja za G55, ukawatazama wanachama hao kama watu wenye vinyongo, kwamba walikuwa chini ya uongozi ulioangushwa wa Freeman Mbowe (mwenyekiti aliyepita). Hoja za G55 zilibebwa na viongozi wapya wa Chadema na kutafsiriwa kuwa ni “wapinga Lissu”.
Tujikite kwenye hali halisi; Lissu yupo mahabusu, akikabiliwa na mashitaka ya uhaini na uchochezi. G55 wametangaza kujivua uanachama wa Chadema. Uchambuzi unapaswa kupita kila upande kuona nani ananufaika na yupi anapoteza? Kuanza na mnufaikaji, hakuna. Si G55, Lissu na timu yake ya uongozi wala chama.
Yupi anapoteza? Jibu ni Chadema bila shaka. Kundi la G55 linaundwa kwa sehemu kubwa na viongozi waliokuwepo kipindi cha uongozi wa Mbowe, vilevile kuna wajumbe wa Baraza Kuu Chadema ambao wamejivua uanachama. Mtaji wa chama cha siasa ni watu. Kuondokewa na watu si afya kwa chama.
Chama kinapoondokewa na viongozi, tena kwa makundi, ni hatari. Tabaka la uongozi, kwa kawaida hutambua siri nyingi za uendeshaji wa taasisi. G55, kwa kuwaheshimu au kuwapuuza, haitaondoa ukweli kwamba wanatambua udhaifu na uimara wa Chadema. Hizo ni silaha watakazokwenda kuzitumia waendako.
Lenzi ya hisabati
Kipimo ni uamuzi wa G55, mazingira ya kisiasa, je, wana hasara au faida? Upande wa Lissu na timu yake ya uongozi wana hasara ya kuondokewa na wenzao, vilevile kudhoofika kwa chama chao, lakini wanalo la kujitetea. Huo ndio mtaji. Lissu yupo mahabusu, nyuma yake watu ambao wangepaswa kusimama naye, wanahama chama.
Bila kuingilia mchakato wa kisheria wala uhuru wa mahakama, kitendo cha Lissu kuwa mahabusu hivi sasa, kina athari kubwa kwa maisha yake, familia na chama, lakini ipo faida ambayo anaivuna akiwa hafanyi chochote. Kuwepo ndani ya kuta za jela ni faida kubwa kwake kisiasa.
Lissu anavuna huruma ya umma. Anguko lolote la Chadema, hatalaumiwa, na ikitokea mtu akimshutumu, atajitetea haraka kwamba lilitokea akiwa anashikiliwa mahabusu. Utetezi wake utakuwa na ujazo mkubwa, maana hakuwepo uraiani kukabiliana na kila dhoruba dhidi ya chama.
Uamuzi wa kumweka jela Lissu haukipendelei Chama cha Mapinduzi (CCM). Ishara zilikuwa wazi kwamba Lissu alikuwa kwenye wakati mgumu kufanikisha azimio la “No Reforms, No Election”. Hana fedha, wito wa michango ya “Tone Tone”, haujawa na matokeo ya kuridhisha.
Kipindi ambacho alikuwa akipata tabu kusimamia maneno yake, na kuudhihirishia umma kwamba yeye ndiye kiboko ya dola, anakamatwa na kuwekwa mahabusu. Lenzi ya hisabati kisiasa, inatafsiri picha kuwa kumkamata Lissu na kumshikilia, imekuwa sawa na kumtupia boya mfamaji baharini. Lissu amepewa fursa ya kupumua. Amepata neno la kujitetea.
Lenzi ya hisabati kisiasa, inawaweka G55 kwenye kundi ambalo linashindwa kufanya uamuzi sahihi kulingana na wakati mwafaka. Kitendo cha kujivua uanachama wakati Mwenyekiti Lissu yupo mahabusu, kinawafanya waonekane ni wenye papara, wasiojua namna ya kusoma alama za nyakati.
Moja ya hoja za G55 ni udikteta wa Lissu. Yupo mtu atauliza; Lissu yupo mahabusu, huo udikteta amewatendeaje akiwa nyuma ya nondo? Mwingine anaweza kuwahukumu G55 kuwa ni wabinafsi, wameamua kushikilia matakwa yao kisiasa, kuliko kumfikiria kiongozi wao aliye mahabusu. Hitimisho lake litakuwa kwamba G55 hawana ubinadamu.
Lissu alitangazwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema Januari 22, 2025. Ameongoza chama kwa miezi miwili, kisha akakamatwa na kuwekwa mahabusu. Akili ya kawaida tu, inaweza kuhoiji, ikiwa G55 walishindwa kuhimili vishindo vya kisiasa vya miezi miwili, je, watakuwa imara kiasi gani kukabiliana na viongozi wenye mkono wa chuma siku zijazo, japo kwa mwaka mmoja. Nimekuwa nikiandika mara kwa mara kuhusu azimio la “No Reforms, No Election”, lisivyo na vigezo vya kisayansi. Eneo hili nipo kwenye mtazamo wa pamoja na G55, ambao wanasema agenda hiyo ya kuzuia uchaguzi haitekelezeki. Haihitaji sayansi ya roketi kung’amua kwamba No Reforms, No Election, ni wimbo wenye kiitikio kizuri, pasipo beti zenye mantiki.
G55 wangeacha papara, wangetulia na kupiga hesabu zao vizuri, wangekuwa kwenye nafasi nzuri ya kumuumbua Lissu, kwa huo udikteta wanaousema, vilevile na misimamo yake isiyo na nguzo wala mizizi. Kuhama kwao, kunasababisha watazamwe tofauti. Sibashiri, ila ndiyo sayansi ya siasa yenyewe, G55, watapata wakati mgumu kila watakapoyaendea majukwaa ya kisiasa. Maana wanapishana na upepo wa kisiasa unavyovuma.
Kuna mtu atanipinga kwamba uamuzi bora kisiasa haupaswi kutegemea upepo. Jibu langu kwake ni kwamba kisiasa, bora kukaa kimya ili muda utoe hukumu, kuliko kusimama kushindana na upepo wa kisiasa, madhara yake ni makubwa. Unaweza kujikuta unachukia siasa jumla.