Dar es Salaam. Siku moja baada ya kumsimamisha mkandarasi anayejenga barabara ya Mkange hadi Bagamoyo (Makurunge) mkoani Pwani, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ameunda timu ya wataalamu na kuchunguza changamoto za mara kwa mara katika Kivuko cha MV TANGA.
Kivuko hicho kilichopo wilayani Pangani mkoani Pwani, baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu kusuasua kwa utendaji kwenye kivuko hicho.
Ulega ambaye yuko ziarani kukagua utelekezaji wa miradi ya barabara, madaraja na vivuko, ametoa agizo hilo leo Jumanne Mei 13, 2025, pia amemtaka mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga barabara ya Tanga – Pangani – Mkwaja – Bagamoyo (Makurunge) sehemu ya Tungamaa – Mkwaja – Mkange, kuilipa Serikali fidia kutokana na uzembe uliosababisha mradi huo kutokamilika kwa wakati.
Amesema kwa upande wa Serikali ilitimiza masharti yote ya mkataba ikiwemo kumlipa mkandarasi kwa wakati.
Ulega amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanya jitihada kubwa za ukarabati na ununuzi wa vivuko ili kurahisisha maisha ya wananchi na kwamba, Watanzania hawapaswi kupata shida wakati miundombinu ipo.
Kivuko ambacho kimeundiwa kamati ya uchunguzi kinatoa huduma kati ya Pangani na Bweni, ambapo Ulega amesema lengo ni kuhakikisha kinafanya kazi kwa wakati wote kama ilivyokusudiwa.
“Naunda timu ya watu watatu, mmoja kutoka Ofisi ya Rais na wawili Katibu Mkuu wa Ujenzi atawateua kutoka wizarani ili watuambie kuna kitu gani kinaendelea hapa Pangani, haiwezi ikawa kila siku wananchi wanapata usumbufu wakati kuna watu tumewapa jukumu la kusimamia huduma bora,” amesema Ulega.

Uamuzi huo wa Ulega unakuja kutokana na MV TANGA kushindwa kufanya kazi kwa siku nne huku watendaji na wasimamizi wakishindwa kufanya maamuzi ya haraka ya upatikanaji wa vipuli vya kufungwa katika kivuko hicho na kusisitiza kuwa, endapo itabainika kuna hujuma hatua kali za kinidhamu zitafuata.
Awali, Mbunge wa Pangani ambaye pia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alimuomba waziri huyo kushughulikia changamoto ya usafiri wa Kivuko cha MV TANGA ambacho ni muhimu na msaada kwa wananchi wa Pangani.
Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amekagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 na kuridhishwa na hatua zilizofikiwa
Kwenye eneo la barabara, Ulega ameeleza kutofurahishwa na mwenendo wa mkandarasi wa Kampuni ya China Railway 15 Bureua Group aliyeshindwa kumaliza ujenzi kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.
Kutokana na kusuasua huko, Ulega amemuagiza Katibu Mkuu wa Ujenzi, Mhandisi Aisha Amour, kuondoa kilometa 25 za barabara hiyo ambazo hajazifanyiwa kazi na badala yake itangazwe zabuni mpya kumpata mwenye uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa weledi na kwa wakati.

Kufuatia agizo hilo, sasa kilometa 25 za barabara hiyo inayoanzia Mkange hadi Bagamoyo (Makurunge) zitaunganishwa kwenye zabuni ili apatikane mkandarasi wa kuijenga. Serikali imekwishamlipa mkandarasi Sh47 bilioni huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 48 tu.
“Mkandarasi huyu ametuangusha, hapa hadai hata senti kwani tushamlipa zaidi ya Sh40 bilioni, yupo nyuma ya muda, vifaa hajavileta vyote, wafanyakazi hawajawaleta, hivyo nimechukua uamuzi wa kumnyang’anya sehemu ya kazi ya mradi ili mradi huu ukamilike kwa wakati kumaliza kilio cha wananchi wa Pangani,” amesisitiza Ulega na kuongeza kuwa: “Mkandarasi huyu anatakiwa kuilipia fidia Serikali kwa kuchelewesha mradi. Timu ya wataalamu wetu watachambua mkataba na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.”
Pia, Ulega amemwagiza Katibu Mkuu kumweka mkandarasi huyo katika orodha ya wasiofanya kazi vizuri katika miradi ya ujenzi ili siku za usoni kufanya uamuzi sahihi.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Julius Msofe amesema hadi sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 47.82 ikilinganishwa na mpango kazi wa asilimia 100.