
Unguja. Wakati taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameonya matumizi mabaya ya vikosi vya SMZ katika uchaguzi huo.
Hayo yamejiri leo Jumanne Mei 13, 2025 wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalumu za SMZ.
Mwakilishi wa Kojani, Hassan Hamad Omar (ACT Wazalendo) amesema kumekuwapo na utaratibu wa matumizi mabaya ya vikosi vya SMZ wakati wa uchaguzi jambo linalochangia kuvuruga chaguzi na kuvunja amani.
Amesema mara nyingi wananchi hawana shida lakini dhamana hiyo inabebwa na viongozi hivyo waone haja kuendendesha uhaguzi wa haki bila kuvitumikisha vikosi vya SMZ.
“Tunaomba vikosi hivi vya SMZ visitumike vibaya wakati uchaguzi, wananchi wetu hawana shida lakini wanafuata mambo yanayotolewa na viongozi wetu, lazima tutangulize amani ufanyike uchaguzi mzuri, amesema mwakilishi huyo.
Pia, amesema wanapokuwa ndani ya baraza wanaoneshwa ushirikiano mzuri na kuahidiwa kutekeleza wanayoyasema lakini hali inakuwa tofauti wanapokuwa nje ya baraza hilo.
“Humu ndani tukielezana mambo tunaelewana na tunakubalina lakini tukienda nje utekelezaji wa tunayokubalina hayatekelezwi, hili sio jambo jema,” amesema mwakilishi huyo.
Mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad amesema licha ya Jeshi la Kujenga uchumi (JKU) kutekeleza miradi mizuri ya kimaendeleo lakini kikosi hicho kinatumika vibaya.
Pia, ametaka jeshi hilo kumaliza mgogoro wa shamba la Msahani ambao umekuwa wa muda mrefu lakini ikiangaliwa wananchi wana haki kwani hilo ni shmba lao lakini JKU wanatumia nguvu na mabavu kuwaondoa.
Amesema Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) amesema kuna mgogoro wa shamba la Msahani umekuwa a muda mrefu kwa hiyo wananchi wakichezewa sana wanaweza kuchukua hatua.
“Msahani ni shamba la wananchi jeshi liliwafuata kwa hiyo, tusione wananchi wamenyamaza lakini wanaponewa wanaweza kufanya mengine na hatuombei yafike huko, tuache uonevu,” amesema.
“Tunaomba jeshi hili lisitumike vibaya kama kuna wakati linatumika vibaya basi iwe mwisho, yapo mambo mengi yanayofanyika mbayo yanachafua jeshi hili kwa hiyo halipaswi kuendelea nayo,” amesema.
Kuhusu vitambulisho vya mpiga kura, amesema vipo vitambulisho vingi vimezalishwa lakini havijawafikia walengwa na kwenye hotuba ya wizara hakuna bajeti kwa ajili ya mpango huo hivyo kuitaka wizara ije na mkakati maalumu kuwafikishia walengwa vitambulisho vyao.
Profesa Fakih amezungumzia pia suala la Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrisa Kitwana Mustafa la kuwataka watumishi wawasilishe vitambulisho vya mpigakura kwake avikague akisema hana shida na hilo lakini angetumia nguvu hizo kuhakikisha watu wanapata vitambulisho.
Kwa mujibu wa mwakilishi huyo, wapo wananchi wengi wameshindwa kujiandikisha hivyo angetumia nguvu hiyo kuhakikisha watu wengi wanapata vitambulisho badala ya kuhangaikia vitambulisho ambavyo vipo tayari.
“Sawa Mkuu wa mkoa kuwasilisha vitambulisho hata kama na mimi ningekuwa mwananchi wako ningekuletea, lakini inashangaza kuhangaikia watu ambao tayari wana vitambulisho badala ya kuangaikia watu waliokosa vitambulisho, kwahiyo naomba hawa watu waangaliwe waliokosa kuandikishwa wapate haki yao” amesema Profesa Fakih.
Mwakilishi wa Tumbe Said Saleh Salim licha ya kupongeza hatua zinazoendelea za kujenga ofisi za masheha na wakuu wa wilaya, lakini amesema mara nyingi ofisi hizo zinachakaa na kuondosha thamani ya majengo hayo.
“Kujenga ni kitu kimoja lakini kutunzwa ni kitu kingine, tumekuwa na kasumba kutotunza majengo yanachakaa, kwa hiyo hili ni muhimu kuliendelea,” amesema.