Mwanga. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa, amesisitiza kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea uhaguzi mkuu, Watanzania wanapaswa kuwa wasikivu na kusikiliza kwa umakini, ili kuhakikisha nchi inaendelea kuimarika na kuwa na maendeleo endelevu.

Malasusa ameyasema hayo leo, Mei 13, 2025, wakati akihitimisha ibada ya mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Cleopa Msuya, iliyofanyika katika Usharika wa Usangi Kivindu, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Msuya, ambaye alizaliwa mwaka 1931 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, alifariki dunia Mei 7, 2025, kutokana na ugonjwa wa moyo wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena, iliyopo Jijini Dar es Salaam. Amezikwa leo, Mei 13, 2025, katika makaburi ya familia.
Rais Samia Suluhu Hassan aliongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi hayo ya Mzee Msuya, ambapo pia viongozi mbalimbali wa Serikali, dini na siasa walishiriki.
“Mwaka huu ni wa uchaguzi tusiache kuliombea Taifa hili liendelee kuwa na amani na uchaguzi usifanye Tanzania ikabadilika bali iendelee kuimarika zaidi, tuendelee kujiandaa kama Watanzania na kusikiliza maelekezo ambayo Mungu ametupa watu wa kutuekeza na tuwe wasikivu,” amesema Malasusa.
Aidha amesema Mzee Msuya alikuwa ni mtu wa kuunganisha watu bila kujali dini na kuwataka watanzania kumuenzi kwa kuimarisha umoja na mshikamano.
“Huyu Mzee aliwaunganisha Wakristo na Waislamu ndugu zangu tusije hata siku moja kujaribu kuchonganishana na yoyote kwa njia ya dini,” amesema.
Akitoa salamu za rambirambi, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ameeleza baadhi ya maagizo aliyoyapata kutoka kwa Msuya enzi za uhai wake, akimkumbusha kuwa viongozi wanapaswa kwenda walipo wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.

“Mara ya mwisho nilipomtembelea pale Mwanga mjini, kati ya mambo aliyonikumbusha niwaambie viongozi wenzangu tujitahidi sana kuwafuata wananchi kule walipo, tukawasikilize tujue changamoto zao na tufanye jitihada kuzitatua.”
Ameongeza kuwa “Na alinipa maelekezo kwamba Wapare wanakaa milimani kwa hiyo mpande milimani kwenda kuwasikiliza wananchi na kutatua kero zao. Nalisema hili kwa sababu bahati mbaya sana sikupata hiyo nafasi ya kutii hayo maelekezo yake, lakini kwa kuwa viongozi mko hapa basi hili ni jambo la msingi.”
Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Benki ya Mwanga Hakika, Projest Massawe amesema watamkumbuka Mzee Msuya kwa namna alivyopambania benki hiyo na kuwahimiza wafanyakazi kuhakikisha inakua na kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii.
“Wakati tunamuaga Msuya, tunamkumbuka kama muasisi wa Benki ya Mwanga, ambayo baadaye ilijiunga na benki nyingine na kuwa Mwanga Hakika Benki.

“Hadi kifo kinamkuta, alikuwa mshauri wa benki na alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha tunafikia watu wengi zaidi, huku benki ikielekea katika mwelekeo wa kidijitali zaidi,” amesema Massawe.
“Tutamuenzi Msuya kwa kuhakikisha benki inakua na kufikia wananchi wengi zaidi, pia alituasa tuwafikie wananchi wa kawaida kwa mikopo ya riba nafuu ili kuwakwamua kiuchumi na hili tutalitekeleza.”