
Unguja. Awamu ya pili ya utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) inapoelekea ukingoni, maandalizi ya awamu mpya yanayoanza Oktoba mwaka huu yanaendelea.
Kipaumbele kikubwa kitawekwa kwenye miradi ya ajira za muda na ustawi wa kaya zinazolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza kipato kwa wananchi.
Pamoja na kwamba vipengele vya ajira za muda na ustawi wa kaya vitajielekeza zaidi kwenye kutatua changamoto za mazingira, kipengele cha uhawilishaji wa fedha kitaendelea kutolewa kwa walengwa ambao, kwa sababu mbalimbali kama uzee, ugonjwa au udhaifu wa kimwili, hawawezi kushiriki katika miradi hiyo.
Hayo yameelezwa leo Jumanne, Mei 13, 2025, wakati ujumbe wa Benki ya Dunia ukiongozwa na Claudia Zambra Taibo, ulipotembelea baadhi ya wanufaika wa mradi wa upandaji miti uliobuniwa na walengwa katika eneo la Bungi, Mkoa wa Kusini Unguja.
Meneja wa Miradi ya Ajira za Muda na Uendelezaji wa Miundombinu kutoka Tasaf, Paul Kijazi amesema wako katika hatua ya kufanya tathmini ya mafanikio ya awamu inayomalizika ili kubaini maeneo ya kuboresha katika awamu ijayo.
“Tunapojipanga kwa ajili ya awamu inayofuata, ni muhimu kutathmini mafanikio yaliyopatikana hadi sasa. Tumeona miradi ya kuhifadhi mazingira imeleta tija kwa jamii na taifa, hasa ikizingatiwa changamoto kubwa za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Kijazi.
Ameongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi yamesababisha athari nyingi ikiwemo mafuriko na ukame katika maeneo mbalimbali, hivyo awamu mpya ya Tasaf italenga miradi inayosaidia jamii kukabiliana na hali hiyo.
Hata hivyo, Kijazi amebainisha kuwa si kila mtu atashiriki moja kwa moja katika miradi hiyo, kwani wapo ambao hawawezi kutokana na sababu mbalimbali. Kwa hiyo, kundi hilo litaendelea kufikiwa kupitia uhawilishaji wa fedha.
Baadhi ya wanufaika wa Tasaf waliotoa ushuhuda wa mafanikio ni pamoja na Dawa Haji Ali kutoka Shehia ya Bungi, ambaye amesema kupitia mafunzo ya mradi wamejifunza kupanda miti ya matunda na kulima mbogamboga kwa ajili ya kipato na utunzaji wa mazingira.
“Nimepanda miembe, michungwa na migomba kule shambani na kwenye pwani nalima mwani ambao naouza hadi kufikia Sh500,000 kulingana na msimu,” amesema Dawa.
Suleiman Haji amesema kabla ya kusaidiwa na Tasaf, alikuwa ana maisha magumu, lakini baada ya kupata msaada alianza kuvua kwa kutumia boti ndogo aliyoinunua kwa Sh200,000, na hatimaye akafanikiwa kununua ngalawa kubwa.
Mnufaika mwingine, Ashura Mzee Matabi, amesema alianza kushiriki Tasaf miaka 10 iliyopita akiwa hana makazi ya kudumu, lakini sasa ameweza kujenga nyumba kwa kutumia mapato ya kilimo cha mwani.
“Nilipata Sh500,000 kupitia mradi, nikaanza kulima mwani na sasa nauza na kupata kipato kinachoniwezesha kuendesha maisha yangu,” amesema Ashura.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Salhina Mwita Ameir amesema mradi wa shamba la miti ulioanzishwa na jamii ni mfano bora wa miradi midogo ya mazingira ambayo inaweza kutekelezwa na jamii nyingine kwa lengo la kupata kipato na kulinda mazingira yao.
Claudia Zambra kutoka Benki ya Dunia ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyopiga kupitia Tasaf na kusema kwamba miradi hiyo imeonyesha mafanikio halisi kwa wananchi.
Ameahidi kuwa Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza na kuimarisha miradi hiyo ili kusaidia jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.