Tulia Ackson aeleza sababu ya kutoimba wimbo akimuaga Msuya

Mwanga. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameeleza sababu ya kutouimba wimbo wa “Moyo Wangu Una Furaha ya Kwenda Mbinguni” katika mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Cleopa Msuya, baada ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa kuwataka waamini na waombolezaji kushirikiana naye kuimba.

Akiwa anatoa salamu za rambirambi katika ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la KKKT, Usharika wa Usangi Kivindu, Dk Tulia amesema aliamua kutoimba wimbo huo kutokana na kutafakari uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka 2025.

Awali, wakati akihubiri Askofu Malasusa aliwaalika waumini kuimba wimbo huo wa 157, fungu la tatu, kutoka katika kitabu cha “Tumwabudu Mungu Wetu.”

Hata hivyo, Spika Tulia alibainisha kuwa aliitikia kwa kusikiliza kwa makini badala ya kuimba.

“Kuna wakati unasikia wimbo unagusa nafsi yako moja kwa moja. Mimi nimeamua kuusikiliza kwa makini sana ule wimbo uliokuwa unasema ‘mbinguni tunao utayari’,” amesema Dk Tulia.

Hata hivyo amesema; “Nakushukuru Askofu kwa kuturuhusu sisi ambao hatuko tayari tusiimbe. Sio kwamba hatutaki kwenda mbinguni, tunataka kwenda, lakini si sasa. Sisi ambao tuna uchaguzi mwaka 2025 bado tuna majukumu ambayo tunafikiria.”

Amesema viongozi waliopo sasa, akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan, wana matarajio na dhamira ya kuendelea kuhudumia wananchi, hivyo kuimba wimbo huo kwa sasa kungeweza kuonekana kama ishara ya kutotamani kuendelea na majukumu yao.

Akimzungumzia marehemu Msuya, Dk Tulia alimtaja kuwa kiongozi aliyesimama katika misingi ya hekima, busara, uvumilivu na upendo kwa watu wote.

Amesema hata baada ya kustaafu, Msuya aliendelea kuwa mshauri na kiongozi mwenye busara kubwa na akibaki kuwa mfano bora wa kuigwa.

“Bunge la Tanzania linatambua mchango mkubwa wa mzee huyu. Alitoa huduma akiwa mbunge, waziri, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais. Alituachia somo kubwa la uongozi wa hekima, na ni vyema kila mmoja wetu ajifunze kutoka kwenye maisha yake,” amesema.

Cleopa Msuya alizaliwa mwaka 1931 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro. Alifariki dunia Mei 7, 2025, kutokana na ugonjwa wa moyo akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam. Maziko yake yamefanyika leo, Mei 13, 2025, katika makaburi ya familia nyumbani kwake Usangi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *