
Arusha. Katika safu hii ya gazeti la Mwananchi inayoitwa Elimu na Maadili, nimeandika makala zaidi ya 200 kuanzia mwaka 2021 hadi sasa.
Ninavyoendelea kuandika kuhusu hoja hizo mbili, nimejikuta mara nyingi nashindwa kuzitofautisha, nikijiuliza hivi kweli unaweza kuzungumza juu ya elimu bila kugusa maadili, au inawezekana kujadili maadili bila kujadili elimu?
Tukumbuke hapa kwamba natumia neno “elimu” katika mapana yake, hivyo kwamba mtu anayefikiri kwa kina atagundua kwamba wanadamu wote wa karne zote, wa mataifa yote, wamekuwa na mtindo wao wa kuishi kiroho, kiutu, kifamilia, kimaadili, kijamii, kiuchumi, kimazingira, na kadhalika.
Hivyo wakajenga kile tunachokiita utamaduni au mila au falsafa yao ya maisha.
Utamaduni huo ulikuwa kwao hazina ya maisha, waliurithi kutoka kwa mababu zao kisha wakaurithisha kwa watoto na wajukuu wao.
Hiyo tunaweza kuiita ndiyo iliyokuwa elimu yao ambayo walihakikisha kwamba watoto wao na wajukuu zao waliirithi.
Kwa mtazamo huu, itakuwa ni makosa kufikiri kwamba hapa kwetu elimu ililetwa na wakoloni miaka miaka 100 na ushei uliyopita.
Walipovamia nchi zetu na kuzitawala kimabavu walituambia sisi tulikuwa washenzi tusiojua lolote, tusiokuwa na elimu au falsafa yoyote, hivyo wakajenga hoja kwamba wametuletea elimu kwa mara ya kwanza. Ni uongo na ujinga wa ajabu.
Tunaofikiri kwa kina tunatambua kwamba mababu zetu walituachia elimu iliyolimbikizwa kutoka vizazi na vizazi, na elimu hiyo iliwafanya wamudu maisha yao vizuri.
Katika elimu hiyo tuliyorithi kwa mababu zetu, na ukiangalia historia za falsafa zote za binadamu, utagundua kwamba hawakutenganisha elimu hiyo, au tamaduni hizo, au falsafa hizo na maadili.
Uelewa huo wa maisha ya binadamu yanayozingatia misingi ya maisha ya binadamu umeelezwa vizuri na mwanafalsafa wa Kigiriki Plato (428-348 B.C.) aliyesema:
“Kiini au msingi wa kila hoja, kila maarifa, ni maadili” Ni katika msingi huu wa hoja, ni katika uelewa wa aina hii, napata ujasiri wa kujenga hoja katika makala haya kwamba elimu na maadili ni watoto pacha. Huwezi kuwatenganisha.
Huwezi kutenganisha
Ukiwatenganisha utakuwa umembomoa binadamu na kumwacha hoi kabisa. Je, hapa kwetu tumetanganisha elimu na maadili? Jibu sahihi ni ndiyo.
Tumefanya hivyo tangu tuige mfumo wa elimu wa wakoloni, na matokeo yake yako wazi mbele yetu. Na si kwamba tulitenganisha elimu na maadili, ni kwamba tuliacha kabisa kufundisha somo la maadili shuleni.
Ni baada ya wachache wetu kupiga kelele sana nimeona mwaka huu kitabu cha darasa la tatu na la nne kinachoitwa Historia ya Tanzania na Maadili.
Baada ya kuona kitabu hicho na kikisoma, nikaandika makala katika gazeti hili kupinga somo la maadili kufundishwa na somo la Historia ya Tanzania, nikajenga hoja kwamba somo la maadili ni somo mama hivyo linapaswa kusimama lenyewe.
Ukitafakari maneno ya mwanafalsafa Plato tuliyoyasoma hapo huu utaona kwamba kila somo linapaswa lifundishwe katika msingi wa maadili.
Yaani ni kusema: ukifundisha somo lolote lile, maadili iwe msingi wa somo hilo. Tumeona hapo juu kwamba mababu zetu hawakutenganisha
mtindo wao wa kuishi kiroho, kiutu, kifamilia, kimaadili, kijamii, kiuchumi, kimazingira, na kadhalika.
Hii ndiyo elimu waliyoturithisha sisi. Ni elimu ambayo haikutenganisha maadili na maarifa mengine.
Ni sahihi kusema kwamba kwao maadili yalikuwa msingi wa kila fani ya maisha.
Athari kutenganisha maadili
Yapi matokeo ya kuacha kabisa kufundisha somo la maadili shuleni, yapi ni matokeo ya kufundisha somo lolote bila kulihusisha na maadili?
Matokeo hayo tunayaona sasa hivi katika nchi yetu.Tunashuhudia ubinafsi usioelezeka.Tunaona ufisadi na ulafi unaongamiza uchumi wetu. Tunaona haki za watu zikiporwa katika nyanja mbalimbali za maisha ya kila siku.
Nani hajaona mvutano wa kisiasa unaoangamiza amani yetu? Ni nani haoni tulivyogawanyika kama taifa? Tumefikaje hapa?
Jibu ni rahisi tu: elimu yetu kwa miaka mia na zaidi haikuzingatia maadili kama somo mama.
Tulidanganywa na wakoloni kwamba maarifa ya mababu zetu yalikuwa ya kishenzi, kama ilivyoonyeshwa na kitabu cha Through the Dark Continent, kitabu kilichoandikwa na Henry Morton Stanley (1841-1904).
Huyu alikuwa Mwingereza aliyeamini kwamba bara la Afrika lilitopea katika giza la kukosa elimu, maarifa, na falsafa yoyote ile.
Hata wale waliotuletea dini zao kutoka mabara mengine, hawakutambua kwamba tulikuwa na hazina ya falsafa nzuri na njema kama ya mataifa mengine.
Hawakutambua kwamba tulikuwa na dini inayomtambua Mungu Mwenyezi, dini ambayo ilifundisha kwamba mwanadamu na ulimwengu wote ni matunda ya Mungu Muumbaji.
Ndiyo maana wakatuita sisi ni washenzi wasio na dini, wakatumia madaraka ya dini kufuta majina yetu ya asili kwa sababu yalikuwa ya kishenzi.
Nasi tukakumbatia hilo, tukaamini hivyo, tukadharau mila na falsafa zetu, tukakumbatia kila litokalo kwa wakoloni kwamba ni bora kuliko letu.
Tunaendelea kupuuza lugha yetu ya Kiswahili. Tumeshindwa kutumia Kiswahili katika elimu kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.
Tumefika mahali tunajidharau kuliko wakoloni walivyotudharau na wanavyoendelea kutudharau.
Majuzi tu hapa Arusha yalifanyika marekebisho makubwa na ya kutukuka katika hospitali ya Mkoa ya Mlima Meru (Mt. Meru Hospital), na ajabu ya Musa, maandishi yote mapya katika hospitali hiyo ni kwa lugha ya Kiingereza.
Nimeandika juu ya ukoloni huu, nimeandika kuhusu sisi kuendelea kujidharau kwa kiwango hiki, na naona hiyo ni kelele tu isiyowafikia wahusika na wadau wengine.
Hii inanifanya niamini kwamba mtu akielimishwa katika elimu isiyo na maadili kama msingi wake, si tu kwamba atawadharau na kuwahadaa wengine, lakini pia atajidharau mwenyewe.
Ndiyo maana tunaona ni vema zaidi kutumia Kiingereza kutambulisha biashara zetu na majengo yetu na kadhalika.
Tufanyeje?
Sasa tufanyeje? Kwanza tutambue kwamba tupo shimoni kwa sababu hatujatoa kipaumbele katika somo la maadili katika elimu yetu kwa miaka 100 na zaidi.
Tumechelewa lakini tunaweza kujirekebisha. Tuelewe kwamba elimu na maadili vikitenganishwa tutakuwa tumejiangamiza wenyewe.
Tutoke huku tulipokwama, turudi katika njia sahihi. Wamarekani wa asili wana msemo huu: ni kichaa tu hufikiri kwa akili yake.
Aliye na busara hufikiri kwa akili na kwa moyo wake. Ni katika kukuza na kulea moyo, tunakuwa waadilifu.