Ally Mayay apendekeza suluhu sakata la Dabi

Gwiji wa zamani wa Yanga, Taifa Stars na mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay Tembele, amesema alitarajia sakata la kuahirishwa kwa Dabi ya Kariakoo iliyopangwa kuchezwa Machi 8, 2025, lingetatuliwa mapema kutokana na majukumu ya kimataifa yanayolikabili taifa.

Mayay amebainisha kuwa Tanzania ni mwenyeji wa michuano ya CHAN 2025, hivyo ni muhimu suala la dabi kumalizwa haraka ili kutoa nafasi ya maandalizi ya kitaifa kufanyika kwa ufanisi.

Amependekeza kuwa suluhu ya kudumu ni kuzingatia na kusimamia kanuni, sheria na taratibu zilizowekwa, ili kulinda hadhi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

ALLY MAYAY APENDEKEZA SULUHU KALI KUMALIZA SAKATA LA DABI YA KARIAKOO

Ikumbukwe kuwa Machi 7 mwaka huu, Simba ilizuiwa kufanya mazoezi ya mwisho na mabausa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, hali iliyosababisha wagome kushiriki mechi. Yanga nayo ikajibu mapigo ya kutocheza tena hadi ilipeleka kesi CAS ikarejeshwa katika mamlaka za soka nchini. Kutokana na uamuzi wa CAS, Bodi ya Ligi imepanga mechi hiyo ichezwe Juni 15, 2025, lakini Yanga imeendelea kusisitiza haitashiriki, jambo linaloibua mashaka na kuathiri taswira ya ligi.

Mayay amesema mjadala huo umepamba moto hadi kwenye makundi ya mitandao ya kijamii, jambo linalodhihirisha jinsi gani sakata hilo limegusa hisia za watu wengi Duniani.

“Ubora wa Ligi Kuu ya Tanzania unaweza kuwavutia wawekezaji wa kimataifa, lakini hali kama hii inaweza kuwatisha na kuwafanya waogope kupoteza fedha zao. Ni muhimu suala hili litafutiwe suluhu ya haraka kwa mustakabali wa soka letu,” amesema Mayay.

Aidha, ameongeza kuwa katika enzi zao za uchezaji, hakuwahi kushuhudia mgogoro wa dabi kuwa mkubwa kama ilivyo sasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *